Kaka Analewa, Anampiga Dada Yake Wafanyeje?

SWALI:

 

Assalaamu aleykum,

Je inakubaliwa kaka kumpiga dada yake vita mwilini? Jambo hili limefanyika, wazazi wafanye nini? Kijana akikanywa hasikii, bado anampiga ndugu yake wa kike na wote wawili ni wakubwa si watoto. Tafadhani nijibu na kama kuna aya na Hadiyth pia naomba uzinukuu. Ahsante.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kaka anayelewa kumpiga dada yake.

Mwanzo kabisa ni makosa ya wazazi kumweka kijana wao mkubwa anayelewa ndani ya nyumba. Wazazi wanapata madhambi kwa hilo kwani wanamsaidia kijana wao na kumpatia nafasi ya kuzidi kumdhulumu binti yao. Kwa hiyo, mwanzo wazazi wanatakiwa wamshauri na wamsomee kijana wao asiwe ni mwenye kufanya hivyo na lau atafanya basi waweke vijana wa kumchapa huyo mlevi ambaye ni ‘asi mbele ya Dini.

Ikiwa atarekebisha maisha yake itakuwa vyema sana kwake, na lau hatajirekebisha basi itabidi wazazi wamtoe katika nyumba yao aende akaishi kivyake.

Licha ya kuwa huyo dada yake ni mkubwa hata akiwa ni mdogo aliye chini ya wazazi wake ni jukumu la wazazi kumtia adabu binti yao akikosea na sio kaka yake. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam):

Waamrisheni watoto Swalah wakiwa na umri wa miaka saba na wapigeni kwa sababu ya kuacha Swalah wakiwa na umri wa miaka kumi” (at-Tirmidhiy na al-Haakim).

Na kauli nyingine ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Je, mnajua muflis?” Wakasema: “Ni yule asiyekuwa na Dirham (pesa taslimu) wala Diynaar (au samani katika riwaya nyingine)”. Akasema: “Muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah akiwa na Swalah, Funga na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kula mali ya huyu, kumwaga damu ya huyu, kumpiga huyu na kumsingizia mwanamke mtwaharifu. Thawabu zake zitachukuliwa na kupewa huyu na zikimaliza yatachukuliwa madhambi ya huyu na kupewa yeye. Baada ya hapo ataingizwa Motoni” (Muslim).

Pia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia katika Hija yake ya kuaga kuwafanyia wema wanawake na kuwapiga si katika wema. Katika Aayah nyingi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuagizia tusiwe ni wenye kumdhulumu yeyote hata mnyama. Na kumpiga dada ni katika dhuluma kubwa ambayo inaweza kumuingiza mtu katika Moto wa Jahanamu. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuepushe na hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share