Zingatio: Tuwaheshimu Wazee Wetu

Naaswir Haamid

 

 

Wazazi wawili ni sababu ya kuwepo kiumbe baada ya kukutana baba na mama pamoja katika maisha ya kihalali. Basi ni wajibu wa kila Muislamu mwenye kumuamini Mola na Mtume wake awe na adabu njema mbele ya wazazi wake wawili waliomzaa (baba na mama).

 

Ni haki ya wazee kutiiwa na wajibu huo ni wa mwana kumtii mzee. Haki hii inaendelea kwa mzee hata iwapo yupo chini ya kaburi kwa kumuombea du'aa pamoja na kuunga undugu na kuwatembelea rafiki zake wema.

Utiifu kwa wazee ni wasia Wake Mola kwa wanaadamu wote kwani wamepata shida, taabu na mateso yasiyoelezeka katika kumlea mwana. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuusia:

 

{{Na Tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni Kwangu Mimi ndiyo marudio.}} [Suratu-Luqmaan: 14]

 

Na iwapo mzee atakutaka umshirikishe Mola Asiye na mshirika, basi hutakuwa na wajibu wa kumtii. Hata hivyo unatakiwa umfanyie ihsaani kwa kukaa nae kwa wema huku ukimtafutia njia na kumuombea du'aa za kumuongoza. Qur-aan inatufafanulia kuhusu hili:

 

{{Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea Kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.}} [Suratu-Luqmaan: 15]

 

Na kwa mama ana nafasi tatu kinyume na baba mwenye nafasi moja. Kwani: "uchungu wa mwana aujuae mzazi." Uchungu anaoupata mama hadi anapomzaa mwanawe hauwezi kusimuliwa. Kwa maana nyengine, ni uchungu huu ndio unaojenga msingi wa mapenzi na mtoto wake na ndio sababu ya kumuhifadhi kutokana na madhara yoyote.

Iwapo Waislamu tunaitaka Pepo kwa dhati kabisa, basi hatuna budi kuwatii wazee wetu kwa wema na ihsaan. Haswa pale wanapofikia umri wa utu uzima (uzee), hapo ndipo pa kukaza kamba na kustahamilia mitihani ya mzee wako. Kwani huo ndio wakati wa kutunukiwa Pepo kutoka kwa Mwingi wa Rahma. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza yafuatayo:

 

“Amenijia Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) na kuniambia kuwa: … yuko mbali na Rahma za Allaah yule ambaye amejaaliwa kuwakuta wazazi wake wawili au mmoja wao na akashindwa kuingia peponi!, - nilinyamaza kimya, Jibriyl akanitaka niitikie kwa kusema Aamiyn, nikasema Aamiyn”. [Imepokelewa na Ibnu Khuzaymah]

 

Basi ni hasara iliyoje kwa Muislamu kuikosa Pepo kutokana na kutowatii wazee? Leo Muislamu anafikia hatua ya kumuita mzee wake kwa jina lake halisi "Fulani leo hajaja kwangu" akimaanisha kuwa ni mzee wake!! Ulipokuwa mdogo mbona ulitambua kumuita: "Baba/Mama" leo umekuwa ndio unamuita kwa jina lake??! Wengine wanafurutu ada kwa kuwaita wazee wao: "dingi" au "madha"!! Subhaana Llaah! Heshima haipo kabisa na ni aibu na fedheha kabisa kwa Muislamu kuyatamka maneno kama hayo. Kwani kuna ubaya gani kwa aliye baaligh kumuita mzee wake: "Baba/Mama" au "Abiy/Ummiy"?

 

Wahenga wanatwambia: "mama ni mama hata kama ni rikwama", kwa hivyo hata kama mzee amekonga na kuzeeka, hata kama ni mvuta bangi na ni mlevi wa kupindukia, tafadhalini tena tafadhalini tujitahidi kuwaita kwa lafdhi za adabu na heshima. Kwani hadhi yake inabaki kuwa ni mzee wako.

 

Kwa kumalizia, ni vyema tukaelewa kwamba sio adabu kwetu kupandisha sauti zikawa juu kuliko wazee wetu pale tunapozungumza nao. Halikadhalika, tunapofuatana nao, tuwape heshima ya kututangulia kabla yetu sisi.

 

Mola wetu! Umekienea kila kitu kwa rahma na 'ilmu kwa kujua kila kitu. Basi tughufirie madhambi yetu na wazazi wetu na wanaoamini.

 

 

 

Share