Zingatio: Maafa

Zingatio: Maafa

 

Na: Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

Maafa ya Tsunami yalipoikumba dunia, hawakuacha wataalamu kutuambia kwamba yametokana na mtetemeko baharini. Sasa ni vyema nigeuke kwa walio wengi ambao wamepata kuiona bahari imetulia tuli kabisa. Linganisha utulivu huo kwa kuvuta fikra zako vizuri ili uchore picha ya namna bahari ilivyonyanyuka ikaja juu hadi ikagharakisha nyumba za chini mpaka ghorofa, sehemu za pwani mpaka barani. Mwisho malizia na kauli ya: Allaahu Akbar!

 

Wala tusibabaishane kwamba Tsunami ilitokana na mtetemeko au kukosa teknolojia ya kuizuia. Ni sawa tu na kusema mgonjwa amefariki kutokana na homa ya malaria, lakini ukweli unabaki kwamba mtoaji wa hiyo roho ni Allaah kwa kumuamrisha Malaika wa Mauti kutekeleza kazi hiyo. Kwa hivyo, bado Mtoaji amri wa yote Anabaki kuwa ni Yeye tu Pekee. Vyengine vyote vyabaki kuwa ni sababu tu ya hilo tokeo.

 

Kwa bahati mbaya, wataalamu wanaotumiwa leo, wengi wao ni wasio na elimu ya Qur-aan wala Sunnah. Hata kama wanaielewa vizuri, wanaikanyaga chini ya viatu vyao, wakijidai kutoitambua. Ukweli ni kwamba, hayo yote yameshaelezwa ndani ya masomo hayo. Ukitaka usitake, huo ndio ukweli.

 

Nani kati yetu, anabisha ya kwamba, zinaa imetapakaa, udhalimu umeongezeka, mayatima wanadhalilishwa na mengineyo mengi tu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametueleza kuwa; itakapofika zama za watu kujihalalishia madhambi kama vile ulevi na muziki, wajitayarishe na maafa yatakayokuja kwa kupokezana moja baada ya jengine. Hadiyth hiyo (kwa tafsiri) ni kama ifuatayo:

 

“…watakapojitokeza waimbaji wanawake wakiwa na ala zenye nyuzi, ulevi kunywewa, na wafuasi wa mwisho wa watu hawa wanawalaani wa mwanzo, angalia wakati huo kwa kutokea upepo mkali, mtetemeko wa ardhi, kumezwa na ardhi, badiliko la umbo, mvua kubwa mno, na alama zinazofuata moja baada ya nyengine kama vipande vya mkufu vinavyoanguka kimoja baada ya chengine pindi nyuzi zake zinapokatwa.” [at-Tirmidhiy]

 

Isome kwa kuzingatia vizuri, kisha tuiingize Hadiyth hiyo hapo juu ndani ya hali halisi ya mwaka 2008. Homa iitwayo ‘dengue’ imeikumba Brazil na kuua watu 80 tokea Januari hadi Aprili. Mafuriko yaliyoanza Texas hadi Pennsylvania – Marekani na kuua watu 13 mnamo Machi ya 17-19. Kimbunga kibaya chajeruhi watu 30 huko jimbo la Georgia na Atlanta – Marekani, mnamo Machi ya 14-15. Ndege yagonga mlima wa Andean huko Venezuela na kuua abiria wote 46 mnamo Februari ya 21. Mitetemeko miwili ya ardhi iliyo na nguvu yaikumba nchi ya Demokrasia ya Kongo na kuua watu 45 na kujeruhi zaidi ya 450, mnamo Februari ya 3. Mianguko mibaya ya theluji huko kusini mwa China imeacha watu 24 wakiwa wamefariki na kuathiri watu milioni 78, wakiwemo 827,000 waliohama nyumba zao., mnamo Januari ya 28. Takriban nusu ya majimbo yameachwa bila ya umeme, ambao umesababisha gari moshi za abiria kusimamisha usafiri, na kiasi cha viwanja vya ndege 19 kufungwa. Athari ya uchumi nchini China kutokana na maafa hayo yalikisiwa kufikia dola bilioni 3.2.

 

Ee ndugu yangu, basi kaa kitako ufikirie wapi ulipotoka, wapi ulipo na wapi unaelekea. Kumbuka ulikuwa hupo duniani na itafika wakati utakuwa hupo tena. Ukiambiwa soma Qur-aan na Sunnah, zingatia uzisome kwa makini bila ya kuzua. Waislamu wanapokwenda darsa sahihi, jiunge nao. Achana na laghai za dunia hii ambazo hazitakusaidia kitu mbele ya Muumba zaidi ya maafa kama hayo na ghadhabu Zake Allaah siku ya Qiyaamah.

 

Share