Mashairi: Bid'ah (Uzushi Katika Dini)

  Bid'ah (Uzushi Katika Dini)

‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

Salaam kwenye ukumbi, ndugu nisikilizeni,

Nina madogo maombi, masikio yategeni,

Yasitukumbe mawimbi, kama vile baharini,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Ina madhambi tazama, nyongeza katika dini,

Ni kujitwika lawama, na dhambi kwenye mizani,

Nyongeza nani kasema, mashekhe wa aina gani ?

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Dini imekamilika, aya ipo isomeni,

Mungu (Allaah) Ameshatamka, ipo kwenye Qur-aani,

Ya kuwa Ameridhika, na dini yetu oneni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Mambo mengi tunaona, sio sawa abadani,

Vituko vya kila aina, tunayaona machoni,

Kwenye vitabu hakuna, hayakuwepo zamani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Mungu (Allaah) Mitume Katuma, kutufundisha yakini,

Na ukweli tumesoma, maneno toka mbinguni,

Ametimiza kalima, Mola wetu Rahmani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Mapambo kuyaongeza, aliwaambia nani ?

Wakati tunapoteza, kwa mapambo ya shetani,

Na wengine wanacheza, wakidhikiri njiani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Kama vile maulidi, na kuimba hadharani,

Hujikusanya makundi, na maqasida hewani,

Hujifanya ndio fundi, kwa kuimba uwanjani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Ukimuomba dalili, kama ipo vitabuni,

Atajibu kijahili, eti kosa halioni,

Ukianza kujadili, hana jibu mdomoni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Kumuomba binadamu, eti walii kaburini,

Huu ni wendawazimu, kumsemesha shimoni,

ni Kumshiriki Rahimu, mwisho wake ni motoni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Au kufanya hirizi, kuitundika shingoni,

Au kupakwa masizi, eti kinga ya machoni,

Au kombe na mizizi, huondosha kisirani!

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Na tambiko na mikosi, ni mambo ya ujingani,

Ni mambo ya iblisi, Mungu (Allaah) Ameshamlaani,

Kwa hivyo fanya upesi, na utubu kwa Manani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Na khitma wanaisoma, misahafu mikononi,

Kwa maiti wanasema, itamfika shimoni,

Na yote hayo si mema, ni uzushi ikhwani,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Masufi ndio mabingwa, wanaifanya kwa fani,

Ukisema utapingwa, kwa matusi ya kihuni,

Na pia utaambiwa, huyu Wahabi oneni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Dini wanaiharibu, kuingiza ya kigeni,

Eti ndio ustaarabu, kufanya “modifikesheni,”

Hakuna kwenye vitabu, uliza wanazuoni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Dini inapigwa vita, ndugu zangu amkeni,

Mashia wanatuita, kwenye dini ya Irani,

Masufi wanatuita, kwenye BID’AH tazameni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Hapa nafunga shairi, kwenda mbele natamani,

Mungu (Allaah) Atatusitiri, tunusurike mwishoni,

Tuwashinde Marafidhi, na Masufi wapingeni,

Nyongeza katika dini, ni BID’AH yenye madhambi.

Share