Baada Ya Kuniingilia Kinyume Na Maumbile Amechukua Pesa Zangu Wazazi Wangu Wanasema Watanitolea Radhi Nisiporudiana Naye

 

SWALI:

Assalam alaykum warahmatullah wabaraqatuh. Kwanza natanguliza shukran zangu za dhati kwenu kuweza kuyajibu masuali yangu. Mashekhe zangu ni vyema kuyakemea haya mambo katika website, huyu niliekushtakieni anatumia alhidaya pia.

Nimefahamu vizuri na nimeridhishwa na majibu yenu ni kweli nilikua nampenda na nilimpa vitu vyangu kama password na kadhalika kwa kua akinitolea pesa kutoka bank account moja kunitilia nyengine anapokua mjini. niliridhia kwa kuchukua pesa zangu kwa matumizi ambayo yalimpasa yeye atoe pesa zake lakini sikujali. kwakweli nilijaribu kuhifadhi pesa zangu ili kusaidia familia yangu. kaka yangu ni mfanya biashara kule afrika na nilielewana na kaka yangu zikifikia kiasi kadhaa nimtumie ili tujiimarishe biashara. Mume wangu hakunisupport nilipokuwa nikimshauri katika mambo haya. hata hivyo nilipoona zimefikia idadi tuliyoitaka na kuamua kwenda bank ndipo nilipoona kweupe, zaidi ya elfu tatu ……..3000. kwakweli nilikasirishwa sana lakini hata hivyo nilivumilia. Na kabla ya hapo aliwahi kunichukulia zinazokaribia elfu tatu ambazo nilikuwa sikulipwa kwa zaidi ya mwaka tokea nilipoclaim hata hivyo nilivumilia pia. kipindi ambacho tuna ugomvi pia amenichukulia elfu nne na mia sita 4600 anajiimarisha yeye huko kwao afrika anataka nife masikini.

Ilipokuja kesi hii ya kuniingilia kinguvu alitumia hadaa na kunishawishi nijaribu alipoona siko tayari ndipo aliponiingilia kinguvu. sio kama nataka niyaseme haya lakini yamenijaa katika roho. Baada ya siku hiyo kuona nimechukia na kulia alilinyamazia baadae akaja kunifanyia tena. alipoona namchukia na sikua na hamu nae tena ndipo yalifika kwa wazee. amejaribu kujivutia upande wake na wazee wangu walinishikilia ni lazima nikae nae. nilikubali bila ya ridhaa yangu lakini sikuweza kuthubutu kulala nae na niliamua kuhamia chumba chengine na wanangu.

Mambo sio hayo tuu nimeamua sasa kutengana nae na sasa nipo katika nyumba yangu. ananifuata sana na nimemtishia kumuitia police. nimedai talaka yangu hataki kunipa anasema yeye ana haki kuwaona watoto wake. mimi sina tatizo yeye kuwaona watoto lakini anipe haki yangu na tupange vipi aweze kuonana nao kwa kuheshimiana sitaki aweze kuniingilia katika nyumba yangu simuamini. dada yangu ambae yupo ……..  na mume wake ambaye ni rafiki wa huyu mume wamenishikilia nirudi na hivi sasa nakuandikieni hii email wazee wangu wapo tayari uniachisha radhi kama sitorudi kwa huyo mume. namuomba Mungu sana naamka usiku kumuomba yeye, najiona kama nipo katika shimo sina wa kunisupport mimi nimekua sina haki mimi nimekosa nini mimi. hapa sijui kama ipo mahakama ya kadhi inshallah niombeeni dua na kama mpo hapa …………  nawaomba mnihukumie hili jambo. nitawapa address yangu na Mungu atawalipa mema duniani na akhera. kwakweli nahitaji msaada sana. ni mengi kusimulia lakini namalizia. nawaomba samahani sana kueleza yote haya. nimevumilia sana bila kuwaambia nyumbani yalichukua muda mrefu kudai talaka yangu bila kuyataja hayo machafu. nimefanya hivyo bila budi. Mungu atatulipia

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ndugu yetu hutakiwi kuomba talaka kwa sababu zisizokubalika lakini wewe kama uko mkweli katika malalamiko yako basi unayo haki ya kuomba talaka tena ni haki uliyopewa na Uislam na sisi hapa hatuna cha kukueleza sisi sio ma-Mufti wala Maulamaa lakini tunatoa tulichonacho kutokana na maelezo yako na kama unayoyasema si ya kweli basi hukumu ni juu yako; unaweza kuomba talaka sehemu zinazohusika ikiwa sababu zako ni za msingi kama ambavyo umeeleza, kwani kama sababu sio za msingi, basi soma Hadiyth ifuatayo:

Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote atakayeomba talaka kwa mume wake bila ya sababu (inayokubalika) basi Allaah Atamuharamishia kunusa harufu ya Pepo” Imepokelewa na Al-Haakim, kitabu cha twalaaq, amesema hadiythi hii ni sahihi kwa sharti ya Shaykhayn.

 

Kama huko tayari kuchukua hatua hiyo na huna lolole lile na huyo mumeo zaidi ya kumchukia na kuwa unaogopa kutiwa motoni kwa kuwa utashindwa kumtimizia haki yake ya mume na mke sio nyengine kama hizo ulizozitaja; basi unayo haki ya kujikomboa ‘Khul’u’ nako ni kumrejeshea haki yake aliyokupa wakati wa kukuoa na kuwa huru naye na yeye hatokuwa na haki ya kukurejea kwani umejikomboa.

Wazee hawana radhi za kukuachia wala chochote hayo ni maneno tu, mwenye radhi ni Allaah na kama uko na heshima na unawahudumia wazee wako kama Anavyotaka Allaah basi radhi zao atakupa Allaah kwani Yeye ndiye mwenye kutoa na kuwachia radhi sio wazee wala mtu yeyote.

Huyo bwana atakuwa na haki ya kuwaona watoto na watoto watakuwa na haki ya kumuona baba yao na kumjua katika maisha yao kwani hawana baba isipokuwa huyo na wewe na Mola wako ndio wanaoelewa vizuri nani hasa baba yao. Hivyo usijitie madhambi kwa kumzuilia kuwaona watoto au watoto kumjua baba yao na kupata haki zao. Kama humuamini kuja ndani ya nyumba yako usimfungulie mlango ukiwa pekee yako bali jaribu pawepo na watu wengine wenye uwezo wa kumzuia wakati anapojiwa na Shaytwaan wake na pia unaweza kutoa taarifa kwa wahusika kama Polisi kama utahisi kuwa hafahamu lugha ya kuwa asije kwako.

Hivvyo basi usidai talaka bali Jikomboe kutoka kwake na hilo pia umepewa na Uislam.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share