Nimeachika Mume Hamhudumii Mtoto Wake Ananiachia Mimi Akidai Kuwa Nnafanya Kazi. Je Yeye Hana Wajib Kumwangalia?

SWALI:

 

ASALAMU ALEIKUM.

Swali langu ni ipi kuwa hukmu ya baba kwa kutomuangalia mwanawe? Me nilikua nimeolewa na nikajaliwa mtoto, lakini nikaja nikawachana na meme wangu, mimi naishi na mtoto lakini baba hajishughulishi na mtoto, hata ikiwa ni mashala ya ugonjwa na skuli, ukimuuliza anasema kuwa hamwangali mtoto kwa sababu anajua mtoto hawezi kudhalilika kwa sababu mimi nafanya kazi. tafadhali nomba mnieleweshe kuhusu jambo hili. 

JAZAKAHLLAHU KHAIR.


 

JIBU: 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Shukrani kwa swali lako kuhusu baba kutomwangalia mtoto wake na hukmu yake katika Dini yetu.

Hakika hakuna adhabu maalumu ambayo shari’ah imetoa kuhusiana na suala hilo. Katika shari’ah tofauti, baba anaadhibiwa kwa kutowaangalia watoto wake ambao ana jukumu juu yao kuhusu hilo. Na katika shari’ah ya Kiislamu pia, lau baba atashitakiwa kwa Qaadhi basi Qaadhi mwanzo atamlazimisha awatunze na kuwahudumia. Kushindwa kufanya hivyo itabidi achukuliwe hatua kwa Qaadhi kutoa adhabu ya ta’ziyr kulingana na dhulma yenyewe.  

Ama Kesho Akhera, adhabu yake itakuwa kubwa kwani hilo huingia katika dhulma. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ogopeni dhulma kwani dhulma ni kiza Siku ya Qiyaamah” (Muslim). 

Ni makosa kwa baba kuacha majukumu yake ya kumtazama mtoto kwa kila jambo la mahitaji yake hata ikiwa mama yake anafanya kazi. Linalohitajika ni mama kufanya bidii kupata haki za mtoto wake ambaye yuko kwake. Njia ya kwanza ni mama kujaribu kuzungumza na mtalaka wake kuhusiana na hilo na umuhimu wake yeye kutekeleza jukumu lake la uangalizi. 

Ikiwa hakufanikiwa basi ajaribu kuwasiliana na wazazi wake mama na kuwe na kikao baina yake, yeye, wazazi wake mtalaka na wazazi wako kujadili suala hilo na kufikia muafaka kuhusu haki za mtoto. Ikiwa hamkufanikiwa katika kikao hicho basi itabidi upeleke kesi kwa Qaadhi au Shaykh wa eneo hilo na wala asiiachilie haki za mtoto zikakiukwa. 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Afanikishe kuweza kupatikana haki hizo za mtoto na Amlainishe moyo mtalaka wake ili ajue wajibu wake kidini na kuutekeleza.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share