007-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Kwanza

 

SURA YA KWANZA

 

UTANGULIZI

 

 

Mamlaka Ya Kutoa Amri Na Hukumu

 

Qur-aan Tukufu inasema:

 

{{Haikuwa hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu.}} [12:40]

 

Aayah hii inatuonesha wazi kwamba mamlaka ya kutoa amri na hukumu ni ya Kwake pekee Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Amri hii sio tu kwenye sheria, lakini pia inagusa nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutawala. Yeye Allaah Ndiye Pekee wa kutoa amri na kanuni za kila kitu. Qur-aan inasema:

 

{{Fahamuni kwamba (ni Kwake tu Mwenyezi Mungu) na amri zote ni Zake (Mwenyezi Mungu) Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.}} [7:54]

 

Bila ya shaka yoyote, mamlaka ambayo Qur-aan imeeleza kwa Allaah, sio tu kwenye utawala, bali hata kwa sheria. Qur-aan inaeleza hili:

 

{{Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.}} [5:44]

 

 

Nukuu Ndani Ya Baadhi Ya Vitabu

 

Dhana hii ya mamlaka ya Allaah katika sheria ndio msingi mkuu wa Uislamu. Hakika wanachuoni wote wa Kiislamu wanakubaliana kwamba mamlaka ya sheria ni ya Kwake pekee Allaah. Hivyo, kwa mfano ndani ya kitabu chake maarufu: Al-Ihkaam fiy Usuul al-Ahkaam, ambacho kinahusu misingi ya Fiqh, mwanachuoni Amidiy ameandika kama ifuatavyo:

 

"Tambua kwamba, hakuna isipokuwa Allaah ndiye Mtawala na hamna amri inayofaa zaidi kutekelezwa ila iliyotolewa na Yeye"

 

Shaykh Muhammad Khadhiri, mwanachuoni wa Kimisri kwenye Misingi ya Shari’ah ya Kiislamu, anasema ndani ya kitabu chake cha Uswuul al-Fiqhi:

 

"Kwa vile amri ni za Kwake pekee Allaah, hakuna anayepaswa kutoa Amri ila Yeye. Hii ni nukta ambayo Waislamu wote wanakubaliana nayo."

 

Profesa Twaaha al-'Alwaaniy amenukuliwa akisema yafuatayo ndani ya kitabu chake cha Uswuul al-Fiqhi al-Islaamiy:

 

"Kuanzisha vifungu vya Shari’ah, kuamuru sheria kufuatwa, kuweka kanuni na amri, na kufasili mifumo; ni kazi ambayo ni maalumu kwa Allaah pekee. Yeyote anayejipa na kuandikia kazi hizi zaidi ya Allaah, ametenda dhambi ya shirk. Kwani, kufanya hivyo amekwenda kinyume kabisa na imani ya Upweke wa Allaah Tawhiyd." 

Shari’ah Dhidi Ya Sheria

 

Ulimwengu wa leo una Shari’ah na Sheria. Shari’ah ni zile sheria za Kiislamu na Sheria ni zile zinazotungwa na mwanaadamu zisizo na msingi wa dini.

 

Kwa upande wa kesi, kuna kesi za madai (civil) na kesi za jinai (criminal). Kesi za madai ni migogoro baina ya pande mbili zilizofungua kesi. Kawaida kesi hizi hufunguliwa na wananchi wenyewe. Mfano A amemtukana jirani yake na pia rafiki yake wa enzi aitwae B. Hapa kama B amekasirishwa na maneno ya A, atafungua kesi dhidi ya A kuhusiana na madai yake.

 

Ama kesi za jinai, ni makosa dhidi ya Serikali, hivyo hufunguliwa na kusimamiwa kesi hizi na Serikali yenyewe. Kwa mfano makosa ya jinai kama wizi, ubakaji, ujambazi, utapeli, ulaji rushwa na mengineo.

 

Tumetoa maelezo haya ili kuonesha tofauti baina ya neno Shari’ah na Sheria ambayo tunayatumia kwenye kitabu hiki. Ni vyema pia tukiweka wazi kwamba kitabu chetu kitajikita zaidi kwenye mwenendo wa kesi za madai (civil procedure).

 

 

Mwenendo Wa Kesi Za Madai

 

Mwenendo wa kesi ni utaratibu wa hatua baada ya hatua katika kusuluhisha migogoro baina ya pande mbili kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa. Utawala wa haki unapatikana kutokana na mwenendo huru wenye maridhiano. Hivyo, pale mwenendo wa kesi utakapoegemezwa kwenye upendeleo, rushwa, ujinga wa kutoifuata sheria, basi hapo hapatakuwa na utawala wa haki.

 

Utawala wa haki chini ya Uislamu unaweza tu kutambuliwa na kusifiwa kwa watu wanaofahamu Qur-aan na Sunnah pamoja na maelezo ya Fiqhi. Kuna tofauti na yapo mengine yamefanana baina ya mwenendo wa Sheria na Shari’ah.

 

Maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hiki yanachambua zaidi kuonesha uwiano uliopo baina ya pande hizi mbili za sheria. Lengo kuu likiwa ni kutenda haki na uadilifu kupitia mwenendo wa kesi.

 

 

Masharti Ya UteuziWaHakimuWa Kiislamu

 

Ama kuhusu sifa za kuteuliwa kushikilia nafasi ya Hakimu wa Kiislamu, maelezo yafuatayo yanapatikana ndani ya Qur-aan na Sunnah:

 

a) {{Hakika Mwenyezi Mungu Anakuamrisheni kuzirudisha amana kwa wenyewe (wanaozistahiki). Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa haki.}} [4:58]

 

b) {{Hakika wale waliosema: "Mola wetu ni Mwenyezi Mungu," kisha wakatengenea, hawatakuwa na hofu (siku ya kufa kwao wala baadaye) wala hawatahuzunika).}} [46:13]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

a) "Viongozi wenu walio bora ni wale muwapendao na wanaokupendeni na muwaombeao (kheri) na wanaokuombeeni (kheri), (lakini) viongozi wenu waovu kabisa ni muwachukiao na wanaokuchukieni na munaowalaani na wanaokulaanini" (Muslim)

 

b) "Naapa kwa Allaah, hatumpatii yeyote, shughuli za serikali yetu kwa yeyote anayeomba (dhamana) hiyo au aliye na uchu wa (dhamana) hiyo." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

c) "Tunawatambua wanaoomba cheo (cha kutoa haki na dhamana) kama ni asiye muaminifu." (Abu Daauud)

 

Sio tu Qur-aan na Sunnah, lakini pia taariykh yetu inathibitisha kwamba Uislamu haukubaliani na fikra ya mtu kuomba dhamana ya uongozi. Hivyo tunaelezwa na Qalqashandi:

 

"Imesimuliwa na Abu Bakr kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na uteuzi wa dhamana za uadilifu na haki. Alijibu: "Hivyo ni vya wale wasioshabikia navyo na wasio na uchu navyo; hivyo ni kwa wale wanaovikimbia mbali na sio wale wanaovikimbilia; hivyo ni kwa wale wanaopatiwa (bila ya kuviomba) na sio kwa wale wanaodai kuwa ni haki yao." [1]

 

Qur-aan inaeleza kwamba:

 

{{Wale ambao Tukiwamakinisha, (Tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Swalah na wakatoa Zakaah na wakaamrisha yaliyo mema na wakakataza yaliyo mabaya. Na marejeo ya mambo ni kwa Mwenyezi Mungu.}} [22:41]

 

Aayah hiyo hapo juu inafafanua vipengele muhimu vya uadilifu kwa viongozi na wananchi pia. Vipengele hivyo muhimu ni kama vifuatavyo:

 

1. Waislamu wanawajibika kumtii Allaah na Mtume Wake, mmoja mmoja na kwa pamoja pia, na utiifu huu upewe kipaumbele kwa kila mtu mwengine. Bila shaka, utiifu kwa watu wengine unakuja baada ya kumtii Allaah na Mtume na sio kabla, na hili ni la lazima sio hiari.

 

Aayah na Hadiyth zifuatazo zinathibitisha hilo lisemwalo juu:

 

a) {{Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri hilo. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa).}} [33:36]

 

b) {{Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri …Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu …Na wasiohukumu kwa (kufuata) yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio waasi.}} [5: 44, 45, 47]

 

c) "Muislamu ni lazima asikilize na amtii mtawala iwapo atakubaliana kwa aliloamrishwa na atalikataa, alimuradi tu hakuamrishwa kutenda dhambi. Kwa hali hiyo, asimsikilize wala asimtii." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

d) "Hata kama mtumwa aliye na sura mbaya atachaguliwa kuwa mtawala wenu na akatekeleza matakwa yenu kwa mujibu wa mafundisho ya Kitabu na Sunnah, ni lazima mumsikilize na mumtii." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

e) "Hakuna utiifu mbele ya dhambi…" (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

f) "Hakuna utiifu kwa wanaomuasi Allaah" (Atw-Twabaraaniy)

 

Vipengele vilivyotajwa hapo juu kutoka Qur-aan na Sunnah vinaonesha wazi kwamba Mahakimu hawana haki ya kutoa hukumu kinyume na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah na kama watafanya hivyo, Waislamu hawana ulazima kuwatii. Sio hilo tu, ukweli ni kwamba watakuwa wapo kwenye msimamo sahihi iwapo hawatowatii na wala hawatakuwa wametenda dhambi. Juu ya hivyo, iwapo jambo lolote litathibitishwa kuwa sahihi kwa mujibu wa muongozo wa Qur-aan na Sunnah haliwezi kutupwa na Hakimu wala kiongozi yeyote wa Serikali au sheria ya nchi.

 

Kwa maana hiyo, ni amri au sheria iliyopitishwa ndio yenye kugongana na Shari’ah – na sio Shari’ah – hilo liwekwe pembeni na litamkwe kuwa ni lenye kwenda kinyume – batili ultra vires.

 

2. Wakati huo huo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe ameeleza ni wakati gani vipengele hivi vinaweza kuwekwa pembeni. Anasema:

 

a) "Pale watu wanapofanya hivi (yaani, wakisimama imara katika utawala wa Allaah na ukweli wa Utume, wakasimamisha Swalah na kutoa Zakaah), watahifadhiwa maisha yao kutokana na mimi (yaani Mahkama/Dola) isipokuwa wanapotenda kosa la jinai dhidi ya Shari'ah ya Kiislamu. Ama kwa uchambuzi wa nia zao, Allaah pekee Anaweza kuwa Hakimu." (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

b) "Yeyeote anayeitamka (Kalimah ya Tawhiyd) analazimika kuhifadhiwa maisha na mali yake, alimuradi tu hajiwajibishi kwa madhambi mbele ya (Shari'ah za) Allaah, na Allaah Pekee ndio Mwenye kuhukumu niyah." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Hadiyth hizi zinahakikisha hifadhi ya maisha, mali na heshima ndani ya mipaka ya Shari’ah na fikra zake. Mipaka ya hifadhi hii chini ya Shari’ah inapanuliwa hata kwa wasio Waislamu wote, ambao wanaishi chini ya himaya ya Dola la Kiislamu, hupatiwa haki sawa ambazo Waislamu wanazipata.

 

3. Ama kwa upande wa utaratibu au mwenendo wa kufuata kutimiza haki, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kanuni ifuatayo:

 

"Watu wawili wanapofikisha mgogoro kwako kwa kutolewa maamuzi, usitoe hukumu isipokuwa tu pale utakapowasikiliza sawa sawa wote." (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ahmad).

 

Katika kesi aliyohukumu Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ametengeneza kanuni ifuatayo:

 

"Kwa mujibu wa Shari’ah ya Kiislamu, hakuna atakayefungwa bila ya kutenda haki (kisawasawa kwake)." (Maalik; Muwatta)

 

Tunajifunza kutoka maelezo yaliyomo ndani ya Muwatta kwamba, katika sehemu mpya zilizotekwa za Iraaq, baadhi ya watu walianza kufitinisha na kutengeneza tuhuma za uongo mmoja dhidi ya mwengine, na kwa mtindo huu, waliweza kuwapeleka wengi jela. Malalamiko hayo yalipofikishwa mbele ya Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu), alitoa amri hiyo hapo juu. Ina maana kwamba hakuna mtu atakayefungwa bila ya utaratibu maalum wa mwenendo wa kesi ndani ya Mahkama na bila ya kumpatia fursa nzima ya kujitetea.

 

4. Pale Khawaarij wasioamini Dola yoyote walipoibuka kutaka kufanya mapinduzi wakati wa ukhalifa wa Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu), aliwaandikia:

 

"Mnaweza kuishi na kuhama sehemu yoyote muipendayo, alimuradi tu hamumwagi damu na kueneza migogoro na kuhifadhi uhaini. Lakini mukitiwa hatiani kwa kosa lolote miongoni mwa haya, nitapigana vita dhidi yenu." (Ash-Shawkaaniy, Nayl al-Awtaar)

 

Kutokana na maelezo haya, inaonekana wazi kwamba dhana ya uadilifu ya Kiislamu hairuhusu Hakimu kupewa mamlaka ya kukamata au kufunga au kuua au kutoa haki za imani, maoni, mawazo ya mtu yeyote bila ya kufuata Shari'ah madhubuti zinazokutana kwenye uadilifu.

 

Juu ya hivyo, tunajifunza kutokana na vyanzo sahihi kwamba Uislamu hauruhusu ubaguzi baina ya Hakimu na watu wa kesi kwa mnasaba wa Shari'ah, haki na uadilifu. Kunatakiwa kuwepo na ibakie kuwepo sheria iliyo sawa, mwenendo sawa na Mahkama sawa kwa hao wote. Kabla ya kifo chake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijiwasilisha yeye mwenyewe kwa kuridhia dai lolote ambalo mtu anawezekana kuwa nalo dhidi yake. Halikadhalika, Sayyidna 'Umar alimlazimisha Jabalah bin Aiham Ghassani, mkuu wa kabila, kuthibitisha dai la mtu dhidi yake. Pia, alikataa kukubaliana na ombi la 'Amr bin al-'Aas kwenye kugawa kategoria (kuweka ubaguzi) kwa lengo la kulinda heshima za watawala. Sio hilo tu, mtawala alimpatia kila mtu haki ya kumfungulia kesi ndani ya Mahkama ya kawaida.

 

 

Wajibu Wa Hakimu

 

Lengo kuu la ofisi ya Hakimu ni kutenda haki kwa uwazi na azma njema. Mwenendo ulioelezwa humu ni msaada wa wanachuoni mbalimbali ili kuwanufaisha wale wenye kiu ya elimu ya haki na uadilifu kwa mujibu wa Shari’ah. Sio lengo kabisa kwa Hakimu wa Kiislamu kuwa mjinga, mpokea rushwa na asiyetenda haki.

 

Ni vyema tukabainisha ya kwamba hamna utaratibu na mwenendo rasmi wa kesi utakaoelezwa moja kwa moja, isipokuwa njia yoyote itakayopelekea haki kutendeka na kuwatosheleza pande mbili zenye kudai haki, basi hio njia tutaikamata na kuibainisha kuwa ni sahihi kwa Uislamu. Bila ya shaka, Hakimu anateuliwa akiwa ni mjuzi wa mambo, hivyo yafaa kutumia hukumu zilizopita precedence kwenye uamuzi wa migogoro mipya.

 

Mengi yameelezwa na wanachuoni wetu kuhusu Hakimu wa Kiislamu, lakini ni machache yaliyoelezwa kuhusiana na taratibu za kazi yake ya Ki-Shari’ah. Huenda hili lilitendeka kwa sababu mbili. Kwanza, wanachuoni walielekeza nguvu zaidi katika Shari’ah na sio mwenendo wa Shari’ah kwa kuwanufaisha wanajamii na Hakimu. Pili, jamii ya enzi za Maswahaba na Matabi'ina ni tofauti sana na ya kwetu. Sasa, idadi ya watu imeongezeka, matatizo yamezidi kuwa magumu kutokana na siasa za kutungwa na misimamo ya uchumi yenye uoni wa mambo ya anasa. Ni kwa sababu hizo, mwenendo wa kesi za sasa katika Shari’ah ni wenye kupatiwa maelezo ya kina, uchambuzi na fafanuzi za jumla jamala ili kuondosha migogoro, dhana mbovu na itikadi au mila zisizo sahihi.

 

Pamoja na kuangalia mahitaji ya karne yetu hii, kitabu hiki kimekusanya muongozo wa Qur-aan, Sunnah, majadiliano na fafanuzi za wanachuoni, kwa kuchukua maelezo ya hapa na pale ili ipatikane picha nzuri ya namna Hakimu wa Kiislamu anavyotakiwa kutenda na kupambanua baina ya mwenendo wa kesi za Shari’ah na Sheria.

 

Mifano mingi iliyoelezwa humu, yaweza kwa kiasi kikubwa kutendeka chini ya Taifa la Kiislamu liliopo zama za awali za Uislamu. Hata hivyo, mengi yaweza kufanyiwa kazi kwa Hakimu wa Kiislamu hata kama akiwa ameteuliwa kushikilia wadhifa huo akiwa yupo ndani ya taifa lisilo la Kiislamu. Ingawa hiyo Sheria anayoisimamia haina msingi wa maadili bora wala kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), lakini lengo la Shari’ah na Sheria linafanana kuwa ni kutenda haki na uadilifu. Kinachoharibu upande wa Sheria ni kubeza taratibu za Shari’ah pamoja na kutengua maadili kama mzizi wa sheria.

 

Kuna faida kubwa ya kuitafsiri barua ya Sayyidna ‘Umar kwa Abu Muusa al-Ash’ari (Radhiya Allaahu ‘Anhuma). Barua hii itatusaidia sana kuchora ramani ya kitabu hiki:

 

1.     Hakika Hakimu ana majukumu mazito na njia yake inayofanana kwa vitendo.

2.     Elewa mgogoro ulioletwa mbele yako, kwa sababu kuitamka hukumu iliyo ya haki bila ya kuifanyia kazi haitokuwa na maana.

3.     Waone wote walio mbele yako ni sawa, wakusanye Mahkamani na hukumu (itolewe wazi) ili aliye juu asiwe na matumaini ya dhulma, na aliye chini asikose imani ya hukumu yake.

4.     Wajibu wa kuthibitisha ni kwa yule aliyedai au kutuhumu, na kiapo ni kwa yule anayekataa.

5.     Suluhisho baina ya Waislamu ni halali, isipokuwa kwa suluhisho litakalofanya halali kuwa haramu na haramu kuwa halali.

6.     Yule ambaye anaelemea ushahidi usiokuwepo, muwekee muda; kama ataleta ushahidi wake ndani ya kipindi hicho, mpe haki yake iwapo anastahiki, kama akishindwa kufanya hivyo, igeuze hukumu dhidi yake. Hili ni ombi la mwisho na uwazi utakaoondosha giza.

7.     Jiepushe na hukumu yako ya jana ambayo baadaye umetanabahi kwenye akili yako na ukaongozwa njia sahihi kurudi kwenye hukumu ya haki, kwa sababu haki inasimamishwa (daima), na hakuna chochote kinachobatilisha kilicho haki, kwa sababu ni bora kurejea kwenye usahihi kuliko kuendelea na lisilo sahihi.

8.     Ushahidi wa Waislamu wote unatumika kwenye kesi ya mtu mwengine yeyote, isipokuwa ushahidi wa aliyetumikia hukumu ya kesi ya huduud[2] au amewahi kujaribu kutoa ushahidi wa uongo, au ushahidi wa yule anayeshukiwa kuwa ni jamaa au anayehusiana naye.

9.     Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaelewa siri zilizofichikana ndani ya nafsi za waja Wake na Ameweka gamba juu yao kwenye huduud, isipokuwa litakalodhihirika kupitia ushahidi au kiapo.[3]

 

 

Fafanuzi Za Maneno

 

Shari’ah: Ni vyanzo vya sheria vinavyotokana na misingi mikuu ya sheria za Kiislamu kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah pamoja na vyanzo vyengine vidogo kama Qiyaas, Ijma’ na vyenginevyo.

 

Sheria: Kwa mnasaba wa kitabu hiki, tunalifasili neno hili kuwa: Ni sheria ambazo zimetungwa na mwanaadamu zinazodai kuwa hazina uhusiano wa dini yoyote kwa ajili ya kuweka misingi na kanuni za maisha ya mwanaadamu hapa duniani. Neno hili "Sheria" limeanza kutumika zaidi kuanzia Sura ya Pili ili kupambanua baina ya sheria za Kiislamu na zile zinazotungwa na mwanaadamu.

 

Hakimu: Ni mtu mwenye mamlaka ya kubainisha wapi ilipo haki, kuisimamia na kuifanyia kazi hiyo haki. Neno 'Hakimu' ndani ya kitabu hiki linaenda sambamba na neno 'Mahkama'. Kwa mfano tunaposema 'Mahkama itaamrisha….' ina maana ya 'Hakimu ataamrisha…'

Pia 'Hakimu' lina maana sawa na 'Qaadhi' ingawa 'Qaadhi' linatumika sana kwa Mahkama za Kiislamu kinyume na 'Hakimu' ambalo linatumika katika Mahkama mbalimbali nchini Tanzania. Ni vyema tukaeleza kwamba 'Qaadhi' sio tamko lililo takatifu kutoka Qur-aan Tukufu. Taariykh inaonesha kuwa 'Qaadhi' ilianza kipindi cha utawala wa Ufalme wa Umayyah (Umayyad Dynasty) na kazi zake zilikuwa ni kusimamisha haki na kutoa ufafanuzi kwenye vipengele vya Sháriah. 'Qaadhi' waliwajibika kutumia Qur-aan na Sunnah.

Dai (Da’wa): Inatafsiriwa kama ni kuomba kwa nguvu za Ki-Shari’ah kutoka kwa yule mtu anayedai kuwa na haki dhidi ya mwengine mbele ya Hakimu.

 

Mdai (Muddai’i): Mtu anayefanya maombi anaitwa mdai. Pia huitwa Mlalamikaji.

 

Mdaiwa (Muddaa’ ‘alayhi): Yule mtu anayefanyiwa dhidi yake hayo maombi anaitwa mdaiwa. Pia anaitwa Mlalamikiwa.

 

Wadaawa: Mdai na mdaiwa wanapounganishwa kwa kuwaelezea pamoja, hutumika neno la wadaawa. Hivyo, wadaawa ni mdai/wadai pamoja na mdaiwa/wadaiwa.

 

Kwa uwazi, anayedai ndie mdai, anayedaiwa ni mdaiwa na hicho kinachodaiwa ndio dai. Kwa mfano A ametukanwa na B, A atafungua kesi ya kutukanwa kutoka kwa B. Hivyo, A ni mdai (aliyetukanwa), B ni mdaiwa (aliyetukana), na tendo la kutukanwa ndio dai lenyewe.

 

Kwa maana nyengine, anayedai ni mtu anayewajibika kuacha dai (kufuta kesi) kama akipenda na mdaiwa ni mtu asiyeweza kufanya hivyo kwa mapenzi yake kukimbia shauri lililowekwa mbele ya Hakimu. Hivyo, mdaiwa ni mtu aliyekuwa na uwezekano wa kukubali madai bila ya kuwasilisha ushahidi.

 

[1] Qalqashandi, Subh al-A'sha, J. 1, uk. 240.

[2] Kesi za jinai katika Shari’ah kama wizi, zinaa, unywaji pombe n.k.

[3] Angalia Al-Bayhaqiy; As-Sunan Al-Kubraa, X, uk. 150.

Share