Anamuwekea Pesa Benki Mtoto Aliyezaliwa Nje Ya Ndoa Kwa Khofu Kuwa Hatorithi Mali Yake

SWALI:

  

Asalaam aleykum

 

Mimi ni mke wa ndoa lakin mume wangu kabla ya kunioa alikuwa ana mwanamke mwingine ambaye amezaa naye  mtoto wa kiume, kwa ufinyu wa elimu nilionao najua mtoto wa nje ya ndoa hana haki ya kurithi ktk mali za baba yake, sasa baba yake amekuwa akimlimbikizia mali mtoto huyo katika account za watoto na pia amekuwa akimfanyia mambo ambayo hata watoto alozaa katika ndoa hawafanyii hivyo kwa kigezo cha kusema kuwa yule wa nje hana haki ya kurithi iwapo atakufa naomba mnisaidie na pia tumsaidie huyu mume wangu kama anavyofanya ni hakhi au la. Wabillahi Tawfiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kumlimbikizia mtoto wa nje ya ndoa pesa benki.

 

Kigezo cha hicho kitendo ni makosa kwa mume anayefanya hivyo. Hili ndilo tatizo kubwa tunalokumbana nalo katika maisha yetu ya hapa duniani. Mtu hufanya kosa kisha akataka kurekebisha kosa kwa kosa jingine. Hivyo, mtu kama huyo anakuwa na makosa mawili kwa mpigo.

 

Huu ni wakati wake yeye kurudi kwa Mola wake Mlezi na kuacha makosa, ikiwemo dhulma kwa namna moja au nyingine. Mumeo amefanya kosa la kuzini ambalo anatakiwa atubie kikweli kweli kwa Mwenyezi Mungu na kujuta pamoja na kufuatisha mema. Baada ya hapo kwa mujibu wa swali lako ni kuwa mumeo anajua kuwa huyo mtoto wake wa kwanza ambaye kwa sheria hajulikani kuwa ni mtoto wake hawezi kurithi kabisa japokuwa baba huyo wa kibayolijia anaweza kumfanyia hisani kama kumfanyia mema mtoto yeyote ambaye hajiwezi. Hata hivyo, haifai kwake kumfanyia wema namna hiyo hadi kuwadhulumu watoto wake wa halali. Ikiwa ni kweli alijua kuwa atakufa siku moja na lau atazini mtoto anayezaliwa hatokuwa wake wala hatomrithi ni lipi lililompelekea kuzini?

 

Kwa hiyo, hayo mengi anayomfanyia mtoto huyo si haki, bali ni dhulma na ikiwa hatojirekebisha basi atapata hasara kesho Akhera. Hiyo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Ogopeni dhulma, kwani dhulma ni kiza Siku ya Qiyaamah” (Muslim). Hivyo, unatakiwa kumsaidia mumeo asiingie katika dhulma. Watu wa mwanzo kufanyiwa ihsani ni wazazi, mke ana watoto wa halali. Anatakiwa abadilike kabla hajachelewa katika hilo kwani kifo kinakuja ghafla. 

 

Hajakatazwa na sheria kumsaidia mtoto huyo wa nje ya ndoa lakini hiyo itakuwa ni baada ya kuwashughulikia watoto wake wa halali na isiwe ni zaidi ya watoto wa halali. 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share