Kuua Wadudu Wanaoleta Uchafu Na Madhara Inafaa?

 

SWALI:

 

Assalam Alaikum wa Rahmatullah wa Barakatuh,

Naomba Fatwa juu ya haya masuala ya kuua wadudu kama sisimizi, mende, siafu, nzi, na pia wanyama wadogo kama vile panya, mjusi na wengineo. Utakuta hao ni wachafu na watia kero sana. Je sheria inaruhusu kuwaua  kwa kutumia INSECTICIDE ama sumu za kuwaua. Naomba ufafanuzi...shukran na Jazakumullah kheir... 

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwaua wadudu au pia wanyama wenye kuleta uchafu na madhara katika jamii. Hakika hilo ni suala ambalo limezungumziwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake tofauti kuwa inafaa kuwaua baadhi ya wanyama wenye kuleta madhara. Hivyo, kwa kutumia Qiyaas (kulinganisha) hawa wadudu wengine nao itakuwa inafaa kuwaua ili wasilete madhara katika jamii kwa njia moja au nyingine.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ameruhusu kuuliwa kwa nyoka na nge (Abu Daawuud). Na amekwenda zaidi (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa idhini kuuliwa baadhi ya wanyama hata Muislamu akiwa katika Ihraam na katika eneo tukufu la Msikiti wa Haram sehemu ambayo hairuhusiwi kuuliwa kwa wanyama. Amesema (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam): “Mnaweza kuwaua nyoka, nge, panya, mbwa mwenye kuuma, kipanga na wanyama pori wenye kuwavamia wanadamu” (Abu Daawuud). Na katika riwaya ya al-Bukhaariy: “Mnaweza kuwaaua panya, nge, kipanga, kurabu na mbwa mwenye kichaa mkiwa katika Ihraam”. Na ikamjulimsha nyoka katika riwaya nyingine.

 

Kwa hiyo, wanyama au wadudu wenye kuleta madhara wanaweza kuuliwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share