010-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Nne

 

SURA YA NNE

 

 

KUSIKILIZA KESI

 

 

 

Sehemu Ya Mahkama

 

Sehemu yoyote inaweza kutangazwa kama ni Mahkama ya Hakimu ikiwa ni eneo lililo wazi na rahisi kuingilika kwa jamii (open court). Utawala wa haki unaweza kufanywa Msikitini kwa mujibu wa wanachuoni wa Hanafi. Lakini ash-Shafi’iy halikubali wazo hili, ana fikra za wale watu waliokuwa ni wanafiki na wanawake walio ndani ya kipindi chao cha hedhi. Al-Kasam na al-Marghinani, wakilipinga wazo la Hanafi, wametoa hoja zao kwamba; ni vyema ikatengwa sehemu nyengine isiyokuwa Msikiti kuwa ni Mahkama ya Hakimu.[1]

 

Kwa upande mwengine, Sheria inaeleza kwamba ni lazima kesi isikilizwe kwenye Mahkama ya wazi[2] isipokuwa pale Mahkama inaporidhika ya kwamba haitotenda haki iwapo kesi itasikilizwa humo.[3] Hivyo, Mahkama itakuwa na uwezo wa kusiliza kesi sehemu nyengine yoyote baada ya kuweka kumbukumbu za hoja na sababu ya kutosililiza kesi hiyo Mahkama ya wazi.

 

 

Hamna Hukumu Bila Ya Kusikilizwa

 

Lengo kuu la hapa ni kuwapa haki ya kusikilizwa pande zote mbili za kesi (mdai na mdaiwa) ili kuondosha hukumu itakayotolewa kwa maelezo ya upande mmoja. Kanuni hii imechukuliwa kutoka Hadiyth iliyotolewa na ‘Aliy bin Abii Twaalib (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipopatiwa muongozo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mnasaba wa uteuzi wake nchini Yemen kushikilia mamlaka ya kutoa hukumu:

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpeleka (Sayyidna ‘Aliy) Yemenkama ni Qaadhi. Nilisema: “Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Umenipeleka mimi na bado mdogo na sina elimu kuhusu qadhiya (kesi)”. Akasema: “Allaah Atakuongoza kutamka hukumu sahihi. Pande mbili zenye khitilafu zinapokutana mbele yako usihukumu kwa mmoja mpaka umsikilize mwengine. Huenda, kwa kutumia mwenendo huu, sababu za hukumu zitakuwa wazi juu yako” ‘Aliy akasema, baada ya kufuata muongozo huu, sikupata kuwa na shaka yoyote kuhusu hukumu niliyotoa.”[4]

 

Sheria inaeleza kwamba hakuna ruhusa ya kutoa hukumu kwa upande mmoja hadi pale hati ya taarifa inapotolewa kwa upande ulioshindwa kuhudhuria. Hii itampa nafasi kwa mara nyengine kuhudhuria Mahkamani.[5]

 

 

Hukumu Dhidi Ya Upande Mmoja - Al-Qadhaa ‘Alaa al-Ghaib

 

Ibn Qudaamah ambaye ni mwanachuoni wa Hanbali ana maelezo ya kwamba hukumu kuhusiana na haki za wanaadamu zaweza kutolewa dhidi ya aliyeshindwa kuhudhuria Mahkamani. Ametumia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Hind alisema: “Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Abu Sufyaan ni mtu bakhili na hanipatii kitakachonitosheleza mimi na watoto wangu” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Chukua kitakachokutosheleza wewe na mtoto wako wa kiume kulingana na mahitaji (yenu).”[6]

 

Pia Qudaamah anaeleza kwamba; hukumu ambayo imetolewa ya upande mmoja na bila ya kumpatia nafasi ya kumsikiliza mdaiwa iwekwe pembeni ikiwa tu, kamaghaaib (asiyekuwepo Mahkamani) atatokezea Mahkamani na kuthibitisha kwamba ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, haukubaliki kwa Mahkama.

 

Ibn Qudaamah pia anaeleza kwamba, kwa mujibu wa wanachuoni walio wengi kuwa, hukumu iliyotolewa upande mmoja sio sahihi ikiwa mdaiwa yupo ndani ya mji.[7]

 

Hadiyth aliyotumia Ibn Qudaamah sio amri ya kisheria iliyotolewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kipande cha ushauri wa Kishari’ah na maelezo ya dini ili kuwapatia Waislamu muongozo kuhusiana na wale ambao hawapo tayari kufika Mahkamani kutoa ushahidi wao kwa kuegemea sababu zisizo msingi. Maelezo ya Ibn Qudaamah yanakataliwa kwa kutumia Hadiyth ifuatayo:

 

Ibn ‘Abbaas amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kama watu watapewa kulingana na misingi ya madai yao, watadai damu na mali za wengine, lakini jukumu la kiapo ni juu ya mdaiwa”[8]

 

Kwa upande wa madhehebu ya Hanafi, mwanachuoni wa Kihanafi aitwae Al-Marghinani anakubali kwamba hukumu ya upande mmoja sio sahihi isipokuwa iwe mbele ya wakala wa yule asiyehudhuria.[9] Ibn Farhaan na Maaliki wote wanakubali mawazo ya Ibn Qudaamah.[10]

 

Al-Mawardi ametenga kurasa kadhaa kuhusiana na hili na kutoa mjadala mrefu chini ya mada inayoitwa Al-Qadhaa ‘Alaa al-Ghaib – Hukumu Dhidi ya asiyekuwepo. Al-Mawardi ambaye anafuata misimamo ya ash-Shafi’iy, ana mawazo ya kwamba hukumu dhidi ya mtu asiyekuwepo Mahkamani ni sahihi, ikiwa ni kwa qadhiya ya mali inayo au isiyo hamishika. Cha muhimu, ni hiyo hukumu iwe ndani ya misingi ya haki za binaadamu.[11]

 

Kwa Maalik, hukumu kama hiyo ni sahihi katika mali inayohamishika na batili kwa mali zisizohamishika.[12]

 

Hukumu dhidi ya asiyekuwepo Mahkamani lakini yupo ndani ya mji sio sahihi kwa mafundisho ya ash-Shafi’iy. Lakini hukumu hiyo hiyo ni sahihi kwa mujibu wa Ibn  Shubrumah, Ahmad na Is-haaq kama ilivyotolewa maelezo na Al-Mawardi bin Shubrumah ambaye amesema kwa mujibu wa al-Mawardi: “Nitatoa hukumu dhidi ya mtu aliyekuwa nyuma ya ukuta mwengine na ambaye hayupo mbele yangu.”[13]

 

Al-Mawardi baada ya kutoa maelezo ya wanachuoni wakubwa wakubwa, amekubaliana na mawazo ya ash-Shafi’iy kwamba; kama ushahidi mzuri utakaotolewa dhidi ya asiyekuwepo Mahkamani, haki ikathibitika, kutolea hukumu kesi hiyo ni sahihi.

 

Azad ambaye ni mwanachuoni wa Kihanafi ameeleza kwamba pande zote ni lazima ziwepo Mahkamani. Amenukuu kwa kuikataa hoja za watu wa ash-Shafi’iy kwa kutumia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba walikwenda watu wawili kufanya ahadi mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kutimiza malengo yao kwenye siku fulani. Mmoja wao hakutimiza ahadi hii, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoa hukumu na amri dhidi ya yule aliyeshindwa kutimiza ahadi. Azad ameitolea maelezo Hadiyth kuwa haina mnasaba wa hoja za al-Mawardi.[14]

 

Azad anaendelea kutoa hoja kuwa mawazo ya al-Mawardi hayakubaliki kwa karne ya leo. Kwani kipindi cha wanachuoni wa mwanzo, msafara wa mji mmoja kwenda mwengine ulikuwa ni mgumu. Hivyo wanachuoni wakaegemea kwa hukumu kwa aliye mbali (qadhaa ‘ala al-ghaibu) ili kufikia haki. Mahanafi wameingiza na kutumia mwenendo mwengine kwamba pale mdaiwa anaishi kwa muda au maisha yake yote ni maeneo ya mbali na Mahkama, mdai anaruhusika kuiwasilisha kesi yake na kutoa ushahidi na kuangalia kwa makini kuhusiana na ukweli wa ushahidi, atapeleka kumbukumbu za ushahidi wa kesi kwa Hakimu ambaye huyo mdaiwa anaishi.[15]

 

Azad anamaliza kwa kusema kuwa hukumu ya upande mmoja (kama ikishindikana hizo taratibu hapo juu) inaweza kutolewa ikiwa mdaiwa yupo nje ya mji na ameondoka wala hakusudii kurudi siku za mbele. Hata hivyo, mdai ataamrishwa kuweka dhamana (rehani) kama mdaiwa atatokea siku za mbele na kuthibitisha sababu na uhalali wake.[16]

 

Sheria kwa upande wake inaeleza kuwa pale ambapo mdai amefika Mahkamani lakini mdaiwa hakufika, Mahkama inaweza kuendelea na kesi kwa kumsikiliza mdai na kutolea uamuzi wa upande mmoja iwapo tu mdaiwa alipata wito wa kumuita Mahkamani. Ikiwa haikuthibiti kwamba hati ya wito ilipelekwa, Mahkama itaamuru kutolewa kwa hati ya pili ya kumuita mdai. Mahkama pia inaweza kuakhirisha kesi iwapo mdaiwa hakupatiwa muda muafaka wa taarifa ya kufika Mahkamani.[17]

 

Iwapo Mahkama imetoa amri ya kusikilizwa upande mmoja, mdaiwa anaweza kupinga hukumu hiyo[18] au kutoa sababu ya msingi ya kutohudhuria kwake na Mahkama ikamuamuru kusikilizwa kesi yake kana kwamba alikuwepo siku ya mwanzo.[19]

 

Mdai anaposhindwa kufika Mahkamani lakini mdaiwa amefika, Mahkama inaweza kulifuta dai lake (mdai) na hataruhusiwa kufungua dai jengine jipya kama hilo. Hata hivyo, mdai anapowasilisha sababu ya msingi ya kutohudhuria kwake, amri ya kulifuta dai la mdai linaweza kuwekwa upande.[20]

 

Kwa upande wa kesi yenye mdai au mdaiwa zaidi ya mmoja, na baadhi yao tu wamehudhuria, Mahkama itaendelea na kesi kama vile wapo Mahkamani.[21] Na iwapo mdai na mdaiwa kwa pamoja wameshindwa kufika Mahkamani bila ya sababu ya msingi, Mahkama itaamua kuifuta kesi ama kuwapatia wito mwengine ama kuwalazimisha kufika Mahkamani.[22]

 

 

Mdaiwa Kukataa Kujibu

 

Wanachuoni wa Hanafi wanasema kwamba pale mdaiwa anapoitwa na kuukubali wito wa kufika Mahkamani, lakini akakataa kuzungumza mbele ya Mahkama (kudharau) na kukataa kujibu madai ya mdai, Hakimu atampeleka jela mpaka pale atakapokuwa tayari kujibu madai ya mdai. Ama wanachuoni wa Kishafi’iy kwa mujibu wa al-Mawardi, wanasema kwamba mdaiwa hatofungwa, lakini hukumu itatolewa dhidi yake.

 

Utaratibu wa kutolea hukumu dhidi ya anayeshindwa kuwasilisha majibu ya madai unaenda sambamba ndani ya Sheria. Kwani mdaiwa anaposhindwa kuyawasilisha majibu yake ndani ya muda aliopatiwa, Mahkama itatoa amri kwa upande mmoja.[23]

 

 

Kukubaliana Na Madai (Admission)

 

Kwa ujumla, Mahkama inakubali mdaiwa kukariri madai (kukubali ukweli wa mdai) bila ya kuhitaji ushahidi mwengine kutoka kwa mdai. Lakini kukubali huko kwa mdaiwa kuwe kumefanywa kwa hiari. Hata kama kumefanywa kwa kutumia nguvu, haitokuwa na nguvu mbele ya Shari'ah. Wala isiwe imefanywa kwa ubishi au mzaha.

 

Pale mdaiwa anapokubali madai ya mdai na ukweli wake wa mdai, Hakimu atatoa amri ya hukumu itakayompendelea mdai.

 

Sheria pia inakubaliana na upande wowote kukubali madai ya upande wa pili.[24] Kwa mfano mdaiwa anaweza kukubaliana na madai kwamba alishindwa kulilipa deni la mdai. Baada ya Mahkama kupokea hati inayoonesha upande mmoja kukubaliana na madai ya upande mwengine, Hakimu atatoa hukumu inayoona inafaa.[25]

 

 

Kusikiliza Dai

 

Kanuni zinaweka wazi kuhusiana na kulisikiliza dai. Kanuni muhimu na ya moja kwa moja kwa suala hili ni kwamba dai lazima lisikilizwe mbele ya wadaawa au wawakilishi wao. Mdai, kama ataweza, anaweza kumleta mdaiwa pamoja naye mbele ya Mahkama pale tu anapoleta dai lake. Kama hatoweza kumleta mdaiwa, Mahkama ni lazima itoe hati ya kumuita ili afike Mahkamani. Kama mdaiwa atakataa kufika, atapelekewa hati ya wito mara tatu pamoja na hati ya madai katika nyakati tofauti na kama tu bado hajafika, ataarifiwa kwamba Mahkama itateuwa wakala kwa niaba yake na dai likiwa na ushahidi litasikilizwa. Kama bado tu hajafika wala kumleta mwakilishi wake, basi Mahkama yenyewe itateuwa mtu kuangalia faida yake, na baada ya kulisikiliza dai na ushahidi mbele ya pande hizo, pamoja na kuangalia vyema ushahidi, itatoa maamuzi. Ama akitokea wakati pale inapotolewa hukumu dhidi ya upande mmoja (ex-parte), na kupinga usahihi wa maamuzi, ataruhusiwa kujibu dai, na utetezi wake utasikilizwa. Kama madai yake yatakubaliwa, maamuzi yatawekwa pembeni.

 

Hakuna utaratibu wa Mahkama kuteua wakala kusimamia kesi ya yule anayeshindwa kufika Mahkamani kwa upande wa Sheria.

 

 

Kuakhirisha Na Kuchelewesha Haki

 

Aidha, ujio wa kesi ulikuwa ni mchache kwenye kipindi cha wanachuoni wa mwanzo ama kwa sababu nyenginezo, ndio maana hawakusema kitu kuhusiana na kuakhirisha kesi hivyo kuchelewesha katika kutenda uadilifu.

 

Katika barua ya ‘Umar kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhuma), kama ilivyoelezwa awali, tunaweza kusema kwamba Hakimu atumie akili yake na hekima zake zote katika kesi ambayo ni yenye ujanja na ugumu na anaweza kuakhirisha tamko la hukumu hadi afikie hitimisho lililokuwa sahihi.

 

Pale ambapo mdai hana mashahidi wake, wanachuoni wamesema kwamba Hakimu anaweza kusubiri mpaka wafike mashahidi mbele yake kwa muda wa siku tatu.[26]

 

Ama kwa Sheria ni lazima ziwepo sababu za msingi kabla ya kuakhirisha kesi. Kwani haki inayocheleweshwa kutolewa inasababisha haki kukosekana (justice delayed is justice denied). Hata hivyo, Hakimu amepewa nguvu ya kuakhirisha kesi hadi wakati anapoona inafaa. Mahkama inaweza kuakhirisha kuisikiliza kesi mara kwa mara. Katika kila siku inayoikhirishwa kesi, ni lazima Mahkama ipange tarehe nyengine kwa ajili ya pande za kesi kufika kusikiliza kesi yao. Hakutakuwa na ruhusa kwa Mahkama kuakhirisha kesi iwapo imeanza kusikilizwa hadi mashahidi wote wapatiwe haki ya kusikilizwa. Hata hivyo, Mahkama inapokuwa na sababu ya msingi, inaweza kuakhirisha kusikiliza mashahidi hadi siku inayofuata na ni lazima iweke kumbukumbu ya sababu ya kuakhirisha huku.[27]

 

Iwapo muda muwafaka umetolewa na Mahkama, hakutakuwa na ruhusa ya kuakhirisha kesi kwa upande ulioshindwa kuwasilisha ushahidi, au mashahidi au kufanya jambo lolote aliloamrishwa.[28]

 

Upande wowote utakaoshindwa kujibu masuala yaliyoulizwa, na ambayo Mahkama inaamini anaweza kujibu, Mahkama inaweza kuakhirisha kesi hadi siku nyengine, na kutoa muongozo wa mtu huyo aliyeshindwa kujibu kufika Mahkamani.[29] Iwapo hakufika siku iliyotajwa bila ya sababu ya msingi, Mahkama inaweza kutamka hukumu, au kutoa amri yoyote inayoona inafaa.[30]

 

[1] Azad, Judicial System In Islam, uk. 96.

[2] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 5

[3] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXX. r. 6.

[4] Al-Bayhaqiy, as-Sunan al-Kubra, X, uk. 137. Pia angalia al-Jami’, I, uk. 171 na Mishkaat al-Masaabih, al-Khaatib at-Tibirizi, uk. 325.

[5] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 15.

[6] Al-Mughni, IX, uk 109, uk. 110.

[7] Al-Mughni, IX, uk. 109-111.

[8] Muslim, Sahiih.

[9] (a) Al-Murghinani, al-Hidaaya, II, uk. 142 (b) Pia angalia Ibn Qudaamah, Akhbaar al-Qudhaati, IX, uk. 109.

[10] (a) Ibn Farhuun, Tasbiirah, I, uk. 86-88 (b) Al-Hilli, Sharai’ al-Islaam.

[11] Al-Mardhi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 304-326.

[12] Al-Mawardi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 307.

[13] Al-Mawardi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 311.

[14] Azad, Judicial System of Islam, uk. 78-79.

[15] (a) Azad, Judicial System of Islam, uk. 80 (b) Angalia pia kitabu cha Kitaab al-Qaadhi ilaa al-Qaadhi kuhusiana na kumbukumbu za kesi kwa Hakimu mwengine.

[16] Azad, Judicial System of Islam, uk. 80.

[17] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 6.

[18] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 14

[19] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 8.

[20] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 9 – 10.

[21] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 11 – 12.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 13.

[23] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VIII, r. 10.

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XIV, r. 1

[25] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XIV, r. 6.

[26] Kwa mifano, angalia al-Marghinani; al-Hidayah, III, mjadala kuhusiana na Shahadah, uk. 155-156.

[27] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XX, r. 1.

[28] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XX, r. 3.

[29] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XII, r. 4 (1)

[30] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XII, r. 4 (2)

 

Share