Inapasa Kutoa Zakaah Katika Mshahara Na Kodi Ya Nyumba?

SWALI:

Assallam Allaykum,

Huu ni mwisho wa mwaka wa kiislam, tunatakiwa kupiga mahesabu ili kutoa zakah.

Nauliza je ni vipi nitoe zakah katika mshahara wangu na pili ikiwa nina nyumba ya kupangisha na ninapata kodi ya pango kwa wakati tufauti na hiyo kodi ya pango sehemu kubwa bado katika nairudisha kumalizia nyumba hiyo. Je nini wajibu wangu katika kutoa zakah na ikiwa nawajibika kuto niitoe vipi? Namuomba M/Mungu awajalie mnipatie jibu ili nijue wajibu wangu

Ni ndugu yenu katika Uislam


 



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum) na watangu wema mpaka siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako zuri na hii ni dalili ya kuonyesha kuwa Ummah huu uko hai na hautakufa daima. Na dalili kubwa zaidi ni jinsi sisi Waislamu tunavyojitokeza na kujitahidi katika kutekeleza majukumu tuliyopatiwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake.

Tunataka hapa kukumbusha kuwa kutoa Zakah si lazima iwe ni mwisho wa mwaka wa Kiislamu, kwani kila mmoja anaweza kuwa na wakati wake wa kutoa. Masharti makubwa ya Zakah ni: -

      Kufikiwa na niswaab (kiwango cha chini kabisa cha akiba ya hela).

      Kupitiwa hela hizo na Hawl (mwaka katika kalenda ya Kiislamu).

Sasa ikiwa niswaab yako imefika katika mwezi wa Dhul Hijjah na ikabaki katika kiwango hicho mpaka Dhul Hijjah ya mwaka unaofuata kufika itabidi ukitolee Zakah. Ikiwa ni katika mwezi mwengine kama Ramadhaan, au Muharram, Rabi'iul Awwal au mwengine wowote basi unapofika mwezi huo itabidi utoe Zakah.

Kuhusu suala la mshahara wako utatolewa Zakah tu wakati akiba yako imefika niswaab. Ikiwa masurufu yako ni mengi na akiba unayoweka ni kidogo basi Zakah itakuwa haijakupasa mpaka wakati itakapofika kiwango hicho cha chini na kisha kipitiwe na mwaka mzima. Kuhusu Zakah ya nyumba, wanachuoni wametofautiana katika rai mbili za msingi:

Ya Kwanza: Bei ya nyumba uliyonayo ikiwa inafika niswaab, basi unapopita mwaka inabidi ujumlishe na akiba ya kodi uliyopata kwa mwaka ule kisha utoe 2.5% kama Zakah.

Ya Pili: Kinachotolewa Zakah ni akiba ya kodi unayopata kwa mwaka na ikawa imefika niswaab na kupitiwa na Hawl. Hii ndio rai ya Jamhuur kama alivyoeleza Sheikh Dkt. Fawzaan ibn Fawzaan.

Hivyo, wajibu wako ni kutizama ile akiba ambayo uko nayo katika hela ya mshahara wako na kodi ya nyumba unayopata. Wakati akiba hiyo itakapofikia niswaab ambayo ni takriban gramu 82.5 za dhahabu (fanya hesabu kuangalia hiyo itakuwa ni pesa ngapi kutegemea bei ya dhahabu). Wakati ambapo akiba yako itakuwa imefikia hiyo niswaab utangoja mpaka mwaka mzima katika kalenda ya Kiislamu upite na hapo utatoa Zakah ya 2½% kwa akiba uliyo nayo. Ikiwa bado unajenga Zakah itakupasa tu kwa ile akiba na ikiwa hela zote za kodi zinaenda katika kuijenga hiyo nyumba na akiba uliyonayo haijafika niswaab basi hutalazimika kutoa Zakah.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share