Faida Ya Taqwa (Uchaji Allaah)

Faida ya Taqwa (Uchaji Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا﴿٢﴾ وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا﴿٣﴾

 

Na watakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema, au farikianeni nao kwa wema, na mshuhudishe mashahidi wawili wenye uadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah.  Hivyo ndivyo anavyowaidhiwa anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani). Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. Hakika Allaah Anatimiza kusudio Lake. Allaah Amejaalia kwa kila kitu makadirio. [At-Twalaaq: 2-3]

 

 

Hizo ni kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Kitabu Chake Qur-aan Tukufu, ambayo ni Mwongozo kamili wa mwana-Adam.  Kitabu kisichokuwa na shaka wala batili mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye Hikma Mwenye kuhimidiwa. 

 

Maneno yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Kauli za haki kama Anavosema:

 

وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ حَدِيثًا﴿٨٧﴾

“Na ni nani mkweli Zaidi katika maneno kuliko Allaah?”.  [An-Nisaa: 87] 

 

Aayah hizo za Suwrah At-Twalaaq zimetanguliza sharti za kupatikana yale Aliyoyaahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Sharti hiyo ni kuwa na taqwa (Kumcha Allaah) ili jazaa yake iwe ni kujaaliwa njia (upenyo, kivuko) na kuruzukiwa kutoka njia asiyoitegemea wala kuidhania mtu. Pindi litakapopatikana sharti hilo, basi ndipo yatapatikana hayo yaliyoahidiwa.

 

 

Maswali yafuatayo ya kujiuliza: (i) Nini maana ya taqwa? (ii) Vipi kupata taqwa? Majibu yanapatikana kutoka katika sentensi ifuatayo:  "Kutekeleza yaliyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Rasuli Wake  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kujiepusha makatazo Yao na kubakia katika mipaka ya Shariy’ah ya Dini hii tukufu ya Kiislam.". Hapo ndipo itakapopatikana taqwa.  Na kuwa na taqwa ndio sababu ya furaha na kufuzu duniani na Aakhirah, na pia ni sababu ya kuondoshewa shida na dhiki zote.

 

 

Taqwa ni wasiya wa watu wa mwanzo na wa mwisho na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwausia Swahaba wake katika Hadiyth:

 

 

 عن أبي ذَرٍّ جُنْدُب بِن جُنَادَة، وأبي عبد الرحمن مُعَاذ بِن جَبَلٍ رضي الله عنهما، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((اتق الله حيثما كنت، وأَتْبِعِ السَّيئةَ الحسنةَ تَمْحُها، وخالقِ الناسَ بخُلُقٍ حسنٍ)).  رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ   وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ، وَفِي بَعْضِ النُّسَخِ: حَسَنٌ صَحِيحٌ.

Kutoka kwa Abu Dharr Jundub Ibn Junaadah na Abu AbdirRahmaan Mu'aadh Ibn Jabal Radhwiya-Allaahu ‘anhum ambao wamesimulia kwamba Nabiy  (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wa sallam ) amesema: ((Mche Allaah popote pale ulipo, na fuatisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri kitafuta (kitendo kibaya), na ishi na watu kwa uzuri))  [At-Tirmidhiy na kasema kuwa ni Hadiyth Hasan na katika maandiko mengine imesemwa kuwa ni Hasan Swahiyh]

 

 

Na Taqwa haihitajii kuhakikishwa kuwa mahali fulani au wakati fulani, bali taqwa ya hakika  ni pale mtu anapokua yuko peke yake, akajiepusha na yaliyo haraam japokuwa hakuna mtu anayemuona. Na ndipo aliposema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa “Taqwa iko hapa.” akiashiria kwenye kifua chake palipo na moyo na kusema mara tatu.

 

 

 

Share