Kijana Kaweka Ahadi Na Msichana Kuoana, Posa Imekuja Msichana Kakataa, Inafaa Hivyo?

SWALI LA KWANZA:

 

Assalamu alamualaykum,

Mimi ni kijana wa kiume ambae sijawahi kuoa, lakini inshaallah ninayo matarajio hayo. Imetokezea kuzungumza na msichana fulani kuhusu mas-ala ya kuoana baada ya muda fulani, ambapo mimi nitakuwa nishajitayarisha na jambo hilo, lakini wakati tunasubiri mimi na huyo msichana huo muda ufike pametokea posa nyengine kabla ya mimi na hapo msichana huyo alikataa katakata kuolewa na mtu huyo na alipoulizwa jee unae mtu ambae mmekubaliana akasema ndio na akanieleza mimi na mimi nikakubali kufanya mawasiliano na wazee wake na wakakubali jambo hilo, lakini huo muda wetu haujafika. Jee mimi nilifanya kosa katika hali kama hiyo niliyoieleza ukizingatia hatujawahi kufanya zina, na msichana huyo kafikia umri wa kuolewa? Na jee katika uislamu inakubalika kuweka ahadi za kuoana kama hivi nilivyo fanya mimi ilimradi msifanye zina?

 

Na pia wazee hao katika hali kama hiyo ni haki kwa wao kumlazimisha mtoto wao mume alokuwa hamtaki na hali ya kuwa huyoanomtaka ana sifa zile alizozitaja mtume?

 

SWALI LA PILI:

 

Mwanamke kaposwa lakini kakataa kwa sababu anamchumba wake wameahidiana kuoana, na alipoulizwa amlete huyo kijana alikwenda na kazungumza na wazee wa msichana na wakakubali lakini alitaka apewe muda wa miaka 2 ili ajitayarishe. Swali ni: Jee kijana huyu alikosea kufanya hivyo na hali ya kuwa hawakufanya matendo machafu? Na jee katika uislamu inafaa kueke ahadi kama hizi?

 


 

 

JIBU

 

:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kijana kumposa msichana na kuomba muda ili ajitayarishe.

 

 

Posa kama hiyo haina tatizo kabisa kukiwa na udhibiti kwa hao walioposana kulingana na Shari’ah. Udhibiti huo ni kutowasiliana wala kukutana mukiwa peke yenu, wala kutembea pamoja, wachumba wawe wakweli kati yao na kujiepusha na hayo ni kujiweka mbali na zinaa au uchafu mwengine wowote.

 

Msichana ana haki ya kumkataa mvulana mwengine kwa sababu moja au nyingine – kama kutompenda, kuwa tayari ameahidiana na kijana mwengine au sababu nyingine yoyote. Na katika hali hiyo wazazi wake hawana haki ya kumlazimisha binti yao kuolewa na asiyemtaka. Hata hivyo, wazee wakiona kuwa huyo kijana ana sifa zinazotakikana kisheria wanaweza kuzungumza naye kwa njia nzuri ili aweze kumkubali huyo kijana.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimposa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na kumuoa baada ya miaka mitatu. Kwa hiyo, posa na kupatiana muda hakuna tatizo kabisa katika Shari’ah. Hivyo, ahadi kama hizo hazina tatizo katika Dini lakini muweze kutekeleza hilo bila kudanganyana wala kuchezeana na kupotezeana wakati. Na kusiwe na mawasiliano yasiyo ya dharura na yasiyohusiana na ndoa hiyo, na mawasiliano hayo yawe yanajulikana na wazazi wa msichana na yawe kwa idhini yao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share