Kwenda Hajj Na Wazazi Ikiwa Mume Hataki Inafaa?

 

Kwenda Hajj Na Wazazi Ikiwa Mume Hataki Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Swali:

 

Assalam Allaykum;

 

Mimi Mwanamke Mwenye Mume Na Nina Ya Kwenda Hijja Lakini Kila Nikimshauri Mume Wangu Kuhusu Hilo Anaonekana Ni Mzito Na Uwezo Anao. Sasa Itakuwa Vibaya Kama Nitakwenda Mimi Na Wazazi Wangu?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna ubaya kabisa kwenda kutekeleza nguzo yako ukifuatana na wazazi wako. Bila shaka utakuwa umekusudia baba na mama yako, hivyo baba yako anakutosheleza kuwa ni mahram wako na ni jambo jema kabisa.

 

Kilichokuwa muhimu ni upate ruhusa ya mume vilevile jitahidi kumpa makala za Hajj zilizokuwemo Alhidaaya   apate kusoma atambue umuhimu wa kutekeleza ibada hiyo na atambue kuwa kudharau amri za Rabb wake na hali anao uwezo ni maasi makubwa ya kupelekea ukafiri, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Anasema:

 

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwa walimwengu. [Aal-‘Imraan 96-97]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allahu 'anhu), Mujaahid na wengineo wamesema kuhusu Aayah hiyo kwamba: "Yeyote mwenye kukanusha umuhimu wa Hajj anakuwa ni kafiri na Allaah yuko mbali naye kabisa (Hamuhitajii kwa chochote)" [Tafsiyr Ibn Kathiyr]. 

 

Muislamu asitegemee kupewa umri zaidi, hakuna ajuaye lini ataondoka duniani na kama alivyosema  'Umar ibn Khatwtwwaab (Radhwiya Allahu 'anhu) "Yeyote mwenye uwezo wa kutekeleza Hajj kisha asitekeleze, atakapofariki hatokuwa na tofauti baina yake na Yahudi au Naswara" [Hii ina isnaad sahihi inayofika kwa 'Umar – Al-Hilya 9:252 – imenukuliwa katika Tafsiyr ya Ibn Kathiry]

 

Kwa hiyo tunaona hatari ya kudharau kutekeleza nguzo hii kwa mwenye uwezo kuwa atakapofariki hatokuwa katika Dini ya Uislamu, bila shaka hakuna mmoja wetu atakayependa kuwa na hatima mbaya kama hiyo.

 

Utakapojaaliwa kufika huko umuombee sana mumeo Allaah ('Azza wa Jalla)  Ampe imani ya kupenda kutekeleza tuliyoamrishwa katika Dini yetu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share