Atekeleze Fardhi Ya Hijja Kwanza Au Aoe?

SWALI:

 

Kwanza sina budi kumshukuru m/mungu ambae ameumba mbingu na arthi, na yeye ni mjuzi wa kila kiu. Vile vile natuma salamu zangu kwako kwa kusema ASSALAMU ALYKUM.

 

Mwalimu naomba kuuliza swali langu kama ifuatavyo;

Kwa mujibu wa dini ya Kiislamu neno Ndowa ni sunna, na vile vile ukitizama neno  hijja ni nguzo ya tano ya Uislam na pia ni Fardhi. Sasa je mwalimu mimi nnapesa taslimu za kunitoshelezea kwenda kuhiji, lakini mimi ni kijana ambaye sina mke, sasa je nnaweza kuhijji kwa kuwa Hijja ni fardhi au kwanza nifunge ndowa? Natumai swali langu litajibiwa vizuri na kwa ufasaha zaidi.

 

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ima kutekeleza faradhi ya Hijja mwanzo au kuoa.

 

Mara nyingi huchanganyikiwa kuhusu mas-ala ya ndoa kwani wengi wetu huchukua kuwa ni Sunnah tu, hivyo mtu aweza kuoa au kuacha kufanya hivyo. Uhakika wa mambo sivyo kabisa kwani Allaah Aliyetukuka Ametoa amri kwetu tuoe na Akaileta kwa njia ya lazima. Hiyo ni,

Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu” (24: 32).

 

Naye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Yeyote mwenye kukengeuka na Sunnah yangu si katika mimi” (Al-Bukhaariy na Muslim). Ndoa ikiwa ndani yake.

 

 

Kwa minajili hiyo, wanazuoni wamegawanya ndoa katika sehemu tatu:

 

1.     Faradhi kwa yule asiyeweza kujizuia.

2.     Sunnah iliyohimizwa kwa Muislamu anayejiweza.

3.     Haramu kwa asiyeweza kumuweka mke ima kwa kutoweza kumtimizia tendo la ndoa na kadhalika.

 

Kuhusu kadhiya yako inategemea uko katika kundi gani. Ikiwa uko katika kundi la mwanzo itakuwa ni aula mwanzo uoe ili usiingie katika zinaa baadaye utakwenda Hijjah. Ama ukiwa katika aina ya pili au ya tatu, utahitajika mwanzo kwenda Hijjah, kisha uoe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share