Kuvaa Nguo Ya Kijani Katika Kutimiza Fardhi Ya Hajj Ni Sunnah?

 

Kuvaa Nguo Ya  Kijani Katika Kutimiza Fardhi Ya Hajj Ni Sunnah?

 

 

SWALI  

 

Asalam aleykum

Mimi nakwenda hajj mwaka huu, napenda kuuliza kuhusu nguo ya kijani, maana nimeambiwa kuwa nivae nguo ya kijani baada ya kumaliza hajj yaani siku ya sikukuu, na hivyo ndivyo wanavyofanya watu wetu wanaokwenda hajj kuwa wote wanavaa nguo ya kijani siku ya sikukuu. Je, hii ni Sunna kufanya hivyo?

Nitafurahi kupata jibu mapema

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakuna dalili yoyote inayutupa mafunzo kuwa tuvae nguo za kijani katika ibada ya Hajj.  Imetajwa tu rangi ya kijani  katika Qur-aan kuwa ni nguo ambazo watakazovishwa watu wa peponi:

((عَالِيَهُمْ ثِيَابُ سُندُسٍ خُضْرٌ وَإِسْتَبْرَقٌ وَحُلُّوا أَسَاوِرَ مِن فِضَّةٍ وَسَقَاهُمْ رَبُّهُمْ شَرَابًا طَهُورًا))

((Juu yao zipo nguo za hariri laini za kijani kibichi, na hariri nzito ya atilasi. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao Atawanywesha kinywaji safi kabisa)) Al-Insaan: 21]

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ مَنْ أَحْسَنَ عَمَلًا ﴿30 أُوْلَئِكَ لَهُمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَيَلْبَسُونَ ثِيَابًا خُضْرًا مِّن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَّكِئِينَ فِيهَا عَلَى الْأَرَائِكِ نِعْمَ الثَّوَابُ وَحَسُنَتْ مُرْتَفَقًا ﴿31

30.  Hakika wale walioamini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anayetenda mema  

31. Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na atilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia! [Al-Kahf:30-31]

 

Juu ya hivyo, kuvaa nguo za kijani baada ya kumaliza Hajj kunaleta picha kwamba Mahujaji hao wamekubaliwa Hijjah zao na kuwa wameshakuwa ni watu wa Peponi. Hivyo sio sawa kwani Muumini  anatakiwa anapotenda vitendo vyema awe baina ya khofu na mategemeo (ya kukubaliwa vitendo). Na khofu iwe zaidi kuliko mategemeo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ))  

)(Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao)) [Al-Muuminuun:60]  

Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allahu 'anhaa) alimuuliza Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilipoteremshwa Aaya hii: "Ewe Mjume wa Allaah, je, hawa ni wale wale ambao wanaoiba, wanazini na kulewa huku wakimkhofu Allah?"Akajibu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ((Sio ewe bint Abu Bakr, Bintis-swiddiyq! Hao ni wanaoswali, wanafunga, wanatoa sadaka na huku wanamkhofu Allaah 'Azza wa Jalla (Mola Mtukufu)).  [Ahmad]

 

Hayo yote ni kujikalifisha tu kutafuta nguo haswa ya kijani, kwani kama mtu hana, inambidi ahangaike kutafuta na hali mtu anaweza kuvaa nguo yoyote ile.  Dini yetu ni nyepesi lakini sisi wenyewe tunajikalifisha kwa kufanya mambo yasiyo na dalili.  

Kwa maelezo zaidi bonyeza hapa kwenye Swali lenye kuhusu maudhui hii:

 NGUO ZA RANGI YA KIJANI ZINA MAANA GANI?

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share