Mashairi: Chunga Kiapo Chako

 

          ‘Abdallah Bin Eifan

       (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salaam zifike kwako, ndugu yangu Mhariri,

Hapa nakaa kitako, niwatungie shairi,

Tumeshaona vituko, kuapa ovyo hatari,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Uchunge kiapo chako, Muumini tahadhari,

Uape kwa Mungu wako, kwa Jina Lake Qahari,

Jina lingine ni mwiko, ushirikina dhahiri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Kuwe na misukosuko, mikubwa kama bahari,

Useme ukweli wako, uongo wa makafiri,

Ukumbuke uendako, mbele kwa Mola Jabbari,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Usiape kwa uongo, mwisho utapata shari,

Hata upigwe magongo, ukweli usighairi,

Ukweli ni lake lengo, Muumini husubiri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Kiapo kitu muhimu, kaa ukitafakari,

Ona uongo haramu, moto mbele ya safari,

Mbele ya Mungu Adhimu, usutwe utahayari,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Kiapo si masikhara, usifanye ujeuri,

Sikiliza mihadhara, Mashekhe wanahubiri,

Wanaeleza madhara, wapate kukunawiri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Tazama usikufuru, apa kiapo vizuri,

Kwa Jina Lake Ghafuru, kiapo cha dasturi,

Hivyo Ametuamuru, Mungu tutii Yake amri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

 

Ukisoma Qur-aani, wazi kwenye misitari,

Utaona Rahmani, Ameeleza dhahiri, (Al-Maidah: 89)

Kwa hivyo zingatieni, na mwisho wake ni kheri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Usidharau kiapo, ukajifanya hodari,

Na popote uendapo, chunga ulimi vizuri,

Akhera kuna malipo, utakwisha ujeuri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Beti kumi zinatosha, ninatia msumari,

Nimesema vya kutosha, wazi sikuficha siri,

Shari Atatuepusha, Mungu Atatusitiri,

Muumini tahadhari, uchunge kiapo chako.

 

Share