Mashairi 5: Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi

 

 

Mashairi 5: Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

      ‘Abdallah Bin Eifan (Rahimahu-Allaah)

 

 Alhidaaya.com

  

 

 

 

Wote Salaamu Alaykum, jogoo ameshawika,

Sasa tuanze saum, ndio kumepambazuka,

Msizorote kaum, na siku zinakatika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Kumi la tatu rafiki, karibu litatufika,

Tunaomba tawfiki, na moto kuuepuka,

Na Allah Atubariki, tukhitimu kwa baraka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Fadhila zake ni nyingi, zinazovuka mipaka,

Tujitahidi kwa wingi, kamba ya Mola kushika,

Na Swalah ndio msingi, wa dini yetu hakika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Kufunga bila kuswali, bure unahangaika,

Saumu yako batili, ya nini unasumbuka,

Huo ndio ujahili, kukosa kuelimika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Na watu kutukanana, na ugomvi kutendeka,

Kufunga haina maana, madhambi yanachumika,

Tujitahadhari sana, saumu kuharibika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Subira huleta kheri, na Mwezi kuadhimika,

Uepukane na shari, wabaya kuwaepuka,

Isigeuke dosari, na thawabu kufutika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Walofunga kwa imani, kweli wamefaidika,

Itawafaa mbeleni, akiba wameiweka,

Watafurahi yakini, siku wanapofufuka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Kila kitu huandikwa, wapo nasi malaika,

Hakuna kinachokoswa, dogo, kubwa, huandika,

Tutunze amali sawa, zisipate kudondoka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Macho pia yanafunga, na ulimi kadhalika,

Tuwe sana tunachunga, tabia kubadilika,

Tusije “kumwaga unga,” na patupu tukatoka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Mwezi ukimalizika, wengi tutahuzunika,

Mwezi uliosifika, tutabaki kukumbuka,

Mwezi ulonawirika, mema mengi kufanyika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Mwezi huu ndio fursa, thawabu kukusanyika,

Kutengeneza makosa, tabia kurekebika,

Uwe umeshatakasa, mwezi ukishaondoka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

 

Uliza madaktari, mengi yatafahamika,

Wengi wao wamekiri, tumbo linapumzika,

Inaondoa hatari, saumu methibitika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Kama kufunga huwezi, ruhusa mewajibika

Ikimalizika mwezi, deni limesajilika,

Kama kulipa huwezi, masikini utalisha,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Dini yetu ni nyepesi, huwezi ukadhurika,

Usikalifishe nafsi, Kakataza Mtukuka,

Mola katupa nafasi, na ruhusa Ameweka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

 

Uislamu ndio dini, Mola Amesharidhika,

Kitabu cha Qur-ani, milele tahifadhika,

Makosa ndani huoni, tafuta na utachoka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Dini yetu imenyoka, safi imesafishika,

Sawasawa ukishika, huwezi ukasumbuka,

Na imani ukiweka, huwezi kutingishika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Kumi la Tatu la mwisho, ndio moto kuokoka,

Tuombe tutokwe jasho, tusikubali kuchoka,

Hatujuwi mpaka kesho, tupo au tumeruka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Sana na tuombe sana, si usiku si mchana,

Huenda tukapambana, na usiku wa Maana,

Laylatul Qadri amana, ni kumi za mwisho ona,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Na tujiweke tayari, tuanze kutoa Zaka,

Tutafute mafakiri, wenye nguo za viraka,

Hakuna cha kusubiri, tena tufanye haraka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Mola Moto Tuepushe, ona tunahangaika,

Dua Usizirudishe, au tutahalikika,

Viumbe wote wakeshe, Kukuomba Msifika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Tunakuomba Jabari, Peke Yako Mtajika,

Waislamu tunakiri, Wewe Huna Mshirika,

Tukinge na makafiri, Wavunje watavunjika,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

Tuepushe Jahanamu, moto unaolipuka,

Kubali yetu saumu, tusije kuporomoka,

Ninawaaga kaumu, na mimi ninaondoka,

Ramadhani Inaaga, Mola Tusamehe Dhambi.

 

 

 

 

 

 

Share