Kwa Nini Haiwezekani Mke Na Mume Kurudiana Baada Ya Talaka Tatu?

 

SWALI:

 

Aslm alkm

 

Swali langu ni kwa nini tumeamrishwa na mola kuwa ukishatowa talaka tatu hufai kumregea mtalaka wako mpaka aolewe na mume mwengine kisha apewe takala ndio wewe uweze kumuowa tena? Asante.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu sababu ya kutowezekana kumrudia mke baada ya talaka tatu.

Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo kuhusu hilo:

Talaka ni mara mbili. Kisha ni kumuweka kwa wema au kumwacha kwa ihsani...Na kama amempa talaka (ya tatu) basi mwanamke huyo si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine” (al-Baqarah [2]: 229 – 230).

 

Inafahamika kuwa kila Dini au ideolojia yoyote ina nidhamu yake ya kuendesha maisha kwa hali na njia iliyo nzuri. Bila ya nidhamu basi mahusiano hayatakuwa mema wala mazuri.

 

Kukiwa hakuna nidhamu na sheria madhubuti, mara nyingi itakuwa ni kuchezeana na katika kufanya hivyo mwanamke ndiye atakayeumia zaidi. Ili kumlinda mwanamke asiwe ni mwenye kuchezewa na mwanamme, ndio ikawekwa nidhamu kuwa talaka ni mara tatu tu.

 

Mara nyingi mume huwa anamwambia mkewe kuwa yeye anampenda sana lakini kwa kosa dogo tu huwa tayari ametoa talaka. Kwa minajili hiyo Uislamu ukaweka kuwa hakuna dhihaka katika talaka, hata ukiitoa katika dhihaka talaka itakuwa imepita. Hekima ya kuweka kiwango hicho cha talaka ni kama ifuatavyo:

 

1.     Kuchunga nidhamu ya Dini na maadili yake.

 

2.     Kuweka muruwa, heshima na mahusiano baina ya wanandoa.

 

3.     Mume awe ni mwenye kujichunga asiwe ni mwenye kutoa talaka ovyo ovyo.

 

 

4.     Kumchungia haki yule mwanamke aliye katika ndoa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share