Talaka Inasihi Ikiwa Uume Wa Mume Ni Mdogo Sana Au Uke Wa Mke Ni Mkubwa Sana

 

SWALI:

 

Asalam alaykem?

 

Mimi ni kijana wa kitanzania lakini kwa sasa nipo nje ya nchi, hapa tulipo kidogo tuna swali letu kidogo lina tutatiza kwa hiyo sheikh tulikuwa tunaswali letu.

 

Na swali lenjewe ni je kuna ushahidi wowote kwenye quraan au hadithi inayosema kwamba je kama umeoa na bahati mbaya sehemu zako "nyeti" ni ndogo sanaa, je mkeo anaweza kudai talaka? Au mkeo sehemu zake nyeti ni kubwa sana je ufanye nini? Umpe talaka? Samahani sana kama nitakuwa nimekosa lakini ninataka kujua ukweli kwani hapa tunatofautiana sana.

 

Ahsante sheikh!!!!!!!!!!!!

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kusihi kwa talaka kwa ajili ya uume kuwa mdogo au sehemu nyeti za mwanamke kuwa kubwa.

Zipo sababu ambazo zinachukuliwa kutokana na ufahamu wa Qur-aan na Hadiyth ambazo zinamruhusu mke kutaka talaka. Hakika ni kuwa kunatakiwa kuwe na masikilizano katika ndoa.

 

Na mapenzi hupatikana kwa kupatikana uwiano baina ya wanandoa. Wakati uwiano huo ukikosekana basi ndoa ile haiwezi kudumu ila kupatikane suluhu ya kudumu baina yao kwa wakati mwengine kuwashirikisha wazazi wao.

 

Upo wakati mwengine mume anakuwa na tatizo, hivyo kwa sababu moja au nyingine kutoweza kumtimizia mke wake, hasa kitandani. Kutoweza hilo ni sababu inayokubalika kishari’ah kwa mke kutaka talaka bila ya kumrudishia mahari. Sababu ni kuwa hiyo ni ‘Ibaadah na unapata thawabu kama anavyotueleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) {Muslim}. Katika sababu za aina hizo kama walivyoelezea wanachuoni wa Kiislamu ni Inniyn (kushindwa kufanya tendo la ndoa), Mahjuub (ukosefu wa sehemu zake nyeti), Khussiy (ukosefu wa konde), Shakkaaz (kutoa manii kabla ya tendo la ndoa), na kadhalika.

 

Ama kwa mwanamke ni kuwa na mfupa kwenye sehemu zake za siri, kumea kinyama, kuwa na harufu mbaya kutoka katika sehemu hizo, au sehemu hiyo kuwa kubwa sana na kadhalika.

 

Kwa kuwa tatizo hilo litamfanya mume asiweze kumstarehesha mke na mke kumstarehesha mumewe, ni sababu ya Qaadhi kuwatenganisha kwa talaka. Hata hivyo, kwa mwanamme kuwa na dhakari ndogo anaweza kuifanya ndoa yake ikaendelea ikiwa atajua kuitumia vizuri hadi mke akastarehe na kuridhika hadi asifikie kudai talaka. Na katika ALHIDAAYA uko mhadhara wa Malezi ya Kijinisia ambapo Shaykh Muhammad Swaalih ameweza kutoa mafunzo jinsi ya mume kumtimizia mkewe katika hali hiyo. Video za mhadhara huo zinapatikana hapa:

 

MUHAMMAD SWAALIH -Malezi Ya Kijinsia Sehemu Ya 1

 

MUHAMMAD SWAALIH - Malezi Ya Kijinsia Sehemu Ya 2

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share