Hukmu Ya Kumsomea Qur-aan Maiti Akishazikwa

 

SWALI:

Nauliza jee maiti akeshazikwa inafaa kumuombea dua hapo kaburini au kumsomea qurani hasa ikhlas mara 11 au yaasiin? Asante.

 

 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 Shukrani kwa ndugu yetu kwa swali lako muhimu katika mambo ambayo yafaa kufanywa na yanayokatazwa kufanywa pindi mtu anapozikwa.

 

Ili sisi tuweze kumfaidisha maiti aliyekufa inabidi tufuate muongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwenda kinyume na maagizo yake ni kujibebesha mzigo wa madhambi ya bure. Ada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza kuzika alikuwa anasimama kaburini na husema: “Muombeeni msamaha ndugu yenu kwa Allaah na amfanye thabiti kwani hivi sasa anahojiwa” (Abu Daawuud).

 

Tunajifunza kutokana na Hadiyth ya hapo juu makosa mbali mbali yenye kufanywa na watu wengi wanaposimama makaburini mmoja wao anasimama na kuanza kuomba dua kwa sauti kubwa na wengine kuitikia Aamiyn. Au baada ya maiti kufukiwa anatokeza mtu na kijitabu chake cha Talaqini na kumsomea Talaqini!

 

Ilivyo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wamtakie maghfira maiti wao kila mmoja katika nafsi yake na kila mmoja amuombe Allaah aliyetukuka Amthibitishe huyo maiti kwa kauli thabiti pindi atakapoulizwa na Malaika wawili.

 

Pia ni makosa kumlakinia maiti majibu atakayoulizwa na Malaika kaburini. Hili ni jambo ambalo halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Kwa hiyo, tusiwe ni wenye kufanya mambo ambayo ni kinyume na ilivyofundisha Dini yetu Tukufu.

 

Pia ni jambo ambalo limezoeleka kwetu sisi wengi kusema: al-Faatihah kwa roho ya fulani au kusoma Suratu Yaasiyn (Surah ya 36) katika kaburi la maiti au kusoma Suratul Ikhlaasw (Qul Huwa Allaahu Ahad) mara 11, au baadhi ya ayah au Surah katika Qur-aan. Hapana shaka kuwa mambo haya ni kinyume kabisa na sheria ya Dini ya Allaah Aliyetukuka. Hakika hakuna Hadiyth hata moja inayoruhusu kusomwa kwa Suratul Faatihah kumi na moja au Suratul Ikhlaasw au Suratu Yaasin kaburini. Nasaha yetu kwa ndugu zetu waachane na hilo kabisa kwani ni kwenda kinyume na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mambo ambayo yanamfaa maiti ni:

1.       Kwa watoto wake wema kumuombea duaa.

2.      Ikiwa ana deni kwa wanadamu alipiwe.

3.      Ikiwa adaiwa funga ya faradhi watu wake wamfungie.

4.      Watu wake wamtolee sadaka kwa niaba yake.

5.      Ikiwa aliweka nadhiri ya kufanya jambo la halali na hakuweza  kulifanya basi watu wake wamtekelezee.

6.      Kumfanyia Hajj au ‘Umrah ikiwa hakufanya.

7.     Waislamu kwa jumla wawe wanaombeana duaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share