Hadiyth: مَنْ سَنَّ فِي الْإِسْلَامِ سُنَّةً حَسَنَةً Atakayefanya Sunnah Nzuri: Ufafanuzi Wake

SWALI:

 

Naomba nielezwe vilivyo juu ya Hadiyth ya Mtume (s.A.W) inayo sema juu ya {Man Sanna Sunnat Hassan na Man Sanna Sunnat Sayiah}  ni nini maana ya neno Sunna hapa, inaonekana kama kwamba anawaze akafanza Sunna katika mzingara ya Hadiyth hii.

 

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ufafanuzi wa Man sanna fil Islaami Sunnatan hasanah...’ Hakika Hadiyth hii haijafahamika vizuri kiasi ambacho wengi hilo limewapelekea katika kuteleza. Ili kuifahamu vizuri Hadiyth hiyo, hatuna budi kufasiri yote. Kwa hakika makosa yanafanyika kwa sababu ya watu kuchukua kipande kidogo cha Hadiyth na kuacha sababu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuzungumza maneno hayo.

 

Hebu tuitazame Hadiyth hiy kwa ukamilifu wake:

 

Jariyr bin ‘Abdillaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Tulikuwa tumeketi na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katikati ya mchana, akajiwa na watu waliokuwa wamevalia nguo za sufi zenye michoro ya boriti, wamejifunga kibwebwe panga zao, wote ni wa kabila la Mudhar. Uso wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukabadilika kutokana na ufukara aliowaona nao. Akaingia nyumbani mwake kisha akatoka. Akamwamuru Bilaal akaadhini na akakimu, kisha (Mtume) akaswalisha watu na akawakhutubia: ‘Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi Aliyewaumba katika nafsi (asili) moja. Na Akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na Akaeneza wanaume na wanawake wengi kutoka katika wawili hao. Na mcheni Allaah ambaye Kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa, hakika Allaah ni Mlinzi juu yenu’ (an-Nisaa’ [4]: 1), na akawasomea Aayah nyingine ilio mwisho wa Suratul Hashr (59): ‘Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah; na kila mtu atazame anayoyatanguliza ka ajili ya Kesho (Akhera) …’ (59: 18). Mtu na atoe sadaka dinari yake, dirhamu yake, nguo yake, pishi yake ya ngano au ya tende. Hata akasema japo mtu atoe kipande cha tende. Mtu mmoja katika Answaar akaleta mfuko uliomshinda kuubeba, halafu watu nao wakafuatia (kuleta sadaka zao), mpaka nikaona mirundiko miwili ya vyakula na nguo; nikauona uso wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukimeremeta kama kwamba umepakwa rangi ya dhahabu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: (Man sanna fil Islaami Sunnatan hasanah...) Atakayeweka (atakayetenda) mwendo mwema katika Uislamu, basi atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda mwendo huo baada yake bila ya wao kupunguziwa chochote katika ujira wao. Na atakayeweka mwendo mbaya, atapata dhambi zake na dhambi za atakayetenda baada yake bila ya wao kupunguziwa chochote katika dhambi zao’” (Muslim). Hii ni Hadiyth ambayo Imaam an-Nawawiy ameiweka katika Kitabu chake cha Riyaadhw asw-Swalihiyn, mlango wa 19 wenye kichwa cha habari: “Atakaeweka Mwendo Mwema au Mbaya”.

 

Hadiyth hii ni inatufundisha kuwa lengo la Sunnatan Hasanah ni kama kile kitendo cha yule Swahaba ambaye alikuja na mzigo ule aliokuja nao kwa ajili ya kutoa sadaka. Na kwa sababu hiyo ukafunguka mlango wa sadaka na akafuatwa na watu wengi baada yake, hivyo akawa mfunguzi wa kheri kwa ihsani yake hiyo. Na tunapotazama alichofanya Swahaba huyu tunaona kuwa hiyo sadaka aliyotoa ni jambo liko katika shari’ah wala hakuleta jipya lolote au kuzua kama wanavyoitumia wengine Hadiyth hii vibaya kwa malengo yao ya kutetea bid’ah. Upeo wa jambo ni kuwa alipata ubora na fadhila katika kuwatanabahisha Maswahaba na kuwahimiza kwa kitendo chake hicho – cha kutoa sadaka. Kwa hiyo, muradi wa Sunnatan Hasanah katika Hadiyth: Ni kutenda na kutekeleza Sunnah, hasa wanapoghafilika watu au kuiacha. Na ufahamu huo unapanuka kwa maana ya ibara hiyo kujumlisha kila jambo katika mlango wa kheri ambayo imeelezewa na shari’ah na kuhimizwa kwa sharti iwe kwa lengo la kishari’ah la kufuata.

 

Kwa upande wa pili, hii kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Man sanna fil Islaam Sunnatan hasanah” haiwezi kabisa kuchukuliwa kuwa ni kuzua, kwani kule kuwa ni Sunnatan hasanah au sayi-ah haitatambuliwa ila kwa kuafikiana na shari’ah au kwenda kinyume nacho. Hivyo, inayoafikiana na shari’ah na maamrisho yake katika Sunnatan hasanah, na maana ya Hadiyth ni dalili kwa hayo.

 

Na jambo linasemekana kuwa ni Sunnatan Sayi-ah kwa vipengele viwili:

 

1.   Kuzua maasiya na uovu kama katika Hadiyth ya Binaadamu wa kwanza: “Hakuna nafsi yeyote inayouliwa kwa dhulma isipokuwa yule mwanaadamu wa kwanza (Qaabil) ana sehemu ya dhambi katika damu ile; kwa sababu yeye ndiye mtu wa kwanza aliyeweka mwendo wa kuua” (Ahmad, al-Bukhaariy na Muslim)

 

 

2.   Hiyo ni kuzua na kuleta uzushi katika Dini: Na pia lau ingeswihi kuichukua hii Hadiyth kuwa ipo Bid‘ah nzuri kishari’ah ingepingana na Hadiyth nyingi za kijumla zinazotufahamisha kuwa Bid‘ah zote ni upotevu. Na zinapopingana dalili za kijumla ‘Aam’ na hususi ‘khaasw’, hiyo ya hususi huwa haichukuliwi (Tazama al-I‘tiswaam cha ash-Shaatwibiy, mj. 1, uk. 181 na baada yake). Na Hadiyth nyingine ambazo zimegawanya Bid‘ah nzuri na mbaya ambazo ni hususi kama ile ya Bilaal bin al-Haarith (Radhiya Allaahu ‘anhu) na ndani yake ipo ibara: “Na mwenye kuzua Bid‘ah mbaya …” (at-Tirmidhiy). Hadiyth hii haiwezi kutolewa hoja kwani ni dhaifu, kwa sababu ni riwaya ya Kathiyr bin ‘Abdillaah bin ‘Amr bin ‘Awf al-Muzaniy, ambaye ni mmoja mwenye kuachwa, aliyejeruhiwa hivyo kutochukuliwa Hadiyth zake. Ahmad amesema: Analeta Hadiyth Munkar, hivyo si chochote. Na Abu Daawuud amesema: Ni mmoja miongoni mwa waongo. Na mfano wa maneno hayo amesema Imaam ash-Shaafi‘iy. Amesema Ibn Hibbaan: Alikuwa anapokea Hadiyth za kutunga.

 

Kadhalika, kwa faida zaidi unaweza pia kusoma uchambuzi wa mwanachuoni Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz kuhusu Hadiyth hiyo:

 

Imaam Ibn Baaz: Atakayetenda Sunnatun-Hasanah Atapata Ujira Na Ujira Wa Atakayeitenda

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share