Zingatio: Liwapi Chozi?

 

Naaswir Haamid


Giza litakapotanda ndani ya kaburi lako, hakuna mwengine wa kuja kukusaidia. Upo peke yako, kule chini kabisa, chini ya ardhi, hakuna anayesikia sauti yako zaidi ya Mola wako. Ulimkimbia sasa Amekutia Mkononi.

 

Ulikuwa ni chembe ya manii, Mola Akakupatia umbo zuri, sasa unaliringia na hutaki kumsujidia? Sasa ndio unalitumia sikio kwa kusikilizia miziki? Subhaana Llaah, wapi utaipata rehema za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)?

 

Roho itakapovutwa mfano wa zizi lisilotaka kung’oka. Malaika wamepewa amri wala hawaikaidi. Nao wataitoa roho kwa kuikomoa tena kwa nguvu. Namna ulivyomuasi Mola wako ndivyo uchungu utakavyozidi. Je umewahi kufikiria uchungu wa maumivu wa mwanaadamu aliyechunwa ngozi yake, kisha akagaragizwa katika mchanga umoto? Hiyo ndio hali ya kutolewa roho.

 

{{La, hasha! (Roho) itakapofikia kwenye mafupa ya koo; Na pakasemwa: Nani wa kumganga? Na mwenyewe akajua kwa hakika kuwa huko ndiko kufariki; Na utapoambatishwa muundi kwa muundi; Siku hiyo ndiyo kuchungwa kupelekwa kwa Mola wako Mlezi!}} [Tafsiri ya Suratul-Qiyaamah: 26-30]

 

Unamwita mama/baba... yuwapi kukusaidia? Unamwangalia mkeo... yuwapi kukuliwaza? Unamwita mwanao... yuwapi kukufadhili? Waite ndugu zako, rafiki, maraisi, mapolisi na wengineo, hakuna wa kukusaidia. Dakika zako za kuishi zimekwisha ndugu yangu. Pumzi na riziki zako zimeshafikia sifuri. Huna kitu tena. Leo ndio siku yako ambayo ulikuwa unaikimbia, nayo imefika kwani ahadi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni kweli.

 

Wapi basi unakimbilia ewe ndugu yangu Muislamu? Hiyo ndio nyumba yako ya muda ukisubiri kufufuliwa kwenda kuhisabiwa. Hakuna kwengine isipokuwa ni Moto ama Pepo. Motoni ndimo wengi wa viumbe watamalizikia. Ya Allaah tunaomba hifadhi Yako.

 

Wala bado mambo hayajaanza, kivumbi kipo siku ya kufufuliwa hiyo ya Qiyaamah. Iwapo wakati wa kutolewa roho ulikuwa ukitaka msaada wa ndugu, basi wakati huo ndio {{siku ambayo mtu atamkimbia nduguye; Na mamaye na babaye; Na mkewe na wanawe; Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha.}} [Tafsiri ya Suratul-‘Abasa: 34-37]

 

Ni khasara iliyoje, kwa kutumia wakati katika mambo ya upuuzi na ya uzushi. Uliambiwa hichi usifanye ni haramu, ukajibu “ni makruhu tu, sio haramu.” ama “kila mmoja na kaburi lake.” Ukasisitizwa kutenda mema, nawe ukajibu “usinifuatilie wakati wangu.”

 

Uendapo hupajui khatari yake, bado unadhani utaishi milele hapa duniani. Wako wapi wafalme na matajiri waliosifika kutoka kila pembe ya dunia? Wako wapi wabadhirifu waliobadili maumbo yao? Hakuna mwengine wa kukusaidia zaidi ya Mola Mwenyezi. Kama ulimkana duniani, wala usitaraji rehema zake.

 

Hiyo ndio siku ambayo itakugharimu sio mabilioni wala kilo za dhahabu, bali ni amali njema. Iwapo ulimfanyia mzaha Mola, ukamkasirisha kwa kutenda maovu, ukashirikiana na wanafiki pamoja na makafiri katika kuudidimiza Uislamu, basi utamkuta Mola Mwenyezi Akiwa Amekukasirikia.

 

Kumbuka kwamba lengo la kuishi duniani ni kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), sio kuanzisha vipindi vya komedi wala kuifanya runinga kuwa ndio Qur-aan. Balaa sivyo hivyo. Weka makini kabisa Aayah ifuatayo:

{{Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.}} [Tafsiri ya Suratu-Tawbah: 82]

 

Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole sana. Mwenye rehema mno. Mola wetu! Tumetegemea kwako, na tumegeuka kuja Kwako, na Kwako tu ndiko marejeo (ya viumbe wote). Tuswamehe makosa yetu na utuongoze katika njia iliyonyooka.

 

 

Share