Zingatio: Mwili Una Haki Zake

 

Naaswir Haamid

 

 

Kiwanda cha gari kinazalisha mahitaji ya usafiri kwa wanaadamu ili wapate urahisi wa maisha yao hapa duniani. Gari inayotoka hapo ni kawaida yake kuwa na maelezo ya kina kama kwenye ‘catalogue’. Wala hakuna wasiwasi wowote kwamba iwapo itatumika kinyume na maelezo ya kiwanda hicho, gari hiyo itahamia gereji.

 

Mwanadamu ameletwa hapa duniani kuja kumuabudu Mola Mlezi. Ni wajibu wake kufuata yale Anayoyataka Mola wa mbingu na ardhi. Na wala hakuna mwengine apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mlezi wa viumbe vyote.

 

Mwenyezi Mungu Ameiteremsha Qur-aan ili iwe ni muongozo sahihi kwa viumbe vyote. Sunnah nayo ipo bega kwa bega pamoja na Qur-aan ikitoa maelezo ya kina na masuala mbali mbali yakifafanuliwa humo. Huu ndio uteremsho ambao ni msingi mkuu wa maisha yetu hapa duniani. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema ndani ya Qur-aan Tukufu:

 

{{Na Tumekuteremshia mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri.}} [Suratun-Nahl: 44]

 

Waislamu tunaamini kwamba Qur-aan na Sunnah ndio miongozo mikuu ya maisha yetu hapa duniani. Njia nyengine yoyote itakayofuatwa itampelekea mwanaadamu kupotea kwenye udhalilifu mbaya kabisa.

 

Mengi tumeyasikia na kuyasoma; ya kwamba Uislamu umeharamisha kukaribia na kutenda zinaa, kulewa, kuiba, kutembea utupu na mengineyo mengi. Sasa yawa hakieleweki pale linapoibuka kundi moja linalodai kutetea haki za wanaadamu likasema: 'kulewa rukhsa' ama 'zinaa rukhsa'. Wengine wamefurutu ada hadi kudai kwamba 'adhabu ya kifo ifutwe' ukweli wa hili ni kusema: 'kuua rukhsa'. Hizi rukhsa rukhsa hazina kikomo wala kikwazo?

 

Cha kusikitisha zaidi ni kuona dada na kaka zetu walio wengi wakishabikia na kutetea hizo zinazodaiwa haki za binaadamu. Sasa cha kujiuliza kwani mwili nao hauna haki zake? Kama mwili leo utapewa nafasi ya kujitetea, utasema hautaki kupenyezewa pombe wala sigara. Hizi ndimi na nafsi zetu tumezipa nafasi ya juu tukisahau kwamba mwili nao wataka haki zake!

 

Ulimwengu umekosa dira kutokana na kuidharau Qur-aan pamoja na Sunnah yake. Ingawa ukweli ni kwamba mengi wanayoyavumbua walimwengu yameshaelezwa ndani ya vyanzo hivyo vya Uislamu. Alichotufunza Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hatuna budi kukifuata. Hiyo sio khiari, bali ni wajibu. Ajabu ya Waislamu ndio wa mwanzo kukimbilia kwa makafiri kutaka misaada au wakiomba kusuluhishiwa matatizo yao. Mbio hizi zinafanywa bila ya kugonga mlango  wa Qur-aan na Sunnah.

 

Kuna kisa ambacho kinatudhihirishia kwamba kufuata kile alichokiamrisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio wajibu wetu. Kuna yahudi mmoja alikuwa na mgogoro pamoja na Muislamu. Yahudi akataka kusuluhishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati huyo Muislamu alitaka kwenda kwa Ka'b bin al-Ashraf ambaye ni Yahudi adui Mnafiki mkuu. Hatimaye ukapelekwa kwa Mtume na ikaamuliwa kwamba yahudi ndie mwenye haki. Muislamu hakuridhika akaenda kulalamika kwa Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Alipotambua kwamba Mtume amekwishatolea uamuzi mgogoro huo, Sayyidna 'Umar alitoka na upanga wake na kumpiga nao wa shingo huku akisema: "Hivi ndivyo ninavyomuhukumu yule ambaye hakuridhika na amri ya Allaah na Mtume Wake."

 

Tunachojifunza hapa ni kwamba Waislamu wenyewe hawazipi kipaumbele kanuni zao na badala yake wanakimbilia kwa wanafiki na makafiri. Pia ni wajibu wa Waislamu kufuata yale ambayo Ameyaamrisha Mola Mlezi pamoja na Mtume Wake. Hapo mjadala umefungwa kwa kudai kwamba ni haki ya mwanaadamu kuzini, kulewa, kuiba ama kuua.

 

 

Share