Zingatio: Krismasi 4: Zetu Ni ‘Iydul-Fitwr Na ‘Iydul-Adhw-haa

 

Zingatio: Krismasi 4: Zetu Ni ‘Iydul-Fitwr Na ‘Iydul-Adhw-haa

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mwenye huruma kwa Ummah wake. Lolote aliloliamrisha basi linatokana na ukarimu wake. Wala hakuwa akifanya jambo kutokana na matamanio yake, bali alifikisha ujumbe kwa mujibu wa maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Watuletee wale wenye ushahidi kwamba Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuadhimishe uzawa kwa kuifanya kuwa ni siku maalumu ya kusherehekea. Kinyume cha hivyo, bado tunashikilia msimamo kwamba Uislamu una sikukuu zake mbili tu za kuziadhimisha. Nazo ni ‘Iydul-Hajj na ‘Iydul-Fitwr basi, haipo ya tatu wala haipo moja, ni mbili tu. ‘Iydul-Hajj huja baada ya kumalizika ibada ya Hijjah na ‘Iydul-Fitwr huja baada ya kumalizika Swawm ya mwezi wa Ramadhwaan.

 

Ndiyo sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, baada ya kuona watu wa Madiynah walipokuwa na sherehe mbili wakizisherehekea kabla ya kuja Uislaam: (Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ameshakupeni nyinyi kilicho bora kuliko vyote (sikukuu):  ‘Iydul-Adhw-haa (ya kuchinja) na ‘Iydul-Fitwr”.)) [Imepokelewa na Imaam Ahmad, Abu Dawuud na An Nasaaiy].

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia ametuamrisha katika hutuba zake nyingi kuwa tujitofautishe na Mushrikiyn, na hizi ‘Iyd mbili ni miongoni mwa sikukuu zile ambazo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuchukue tahadhari kubwa ya kujitofautisha sana nao (Mushrikiyn). Hii ni kwa mujibu wa mafundisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwamba washirikina wanafanya juu chini kutuingiza katika matendo yao:

وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ

Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao [Al-Baqarah: 120]

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kujishabihisha na makafiri. Iwapo Waislamu watashiriki kwenye sikukuu zao, tofauti zao hazitaonekana. Ndio maana wameweza kuacha kuvaa hijabu ingawa ni maamrisho ya vitabu vyao na Waislamu hivi leo ndio wanaoendelea kuivaa. Anasema Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Mtafuata desturi (mwenendo) za waliokuwa kabla yenu shibri kwa shibri na pima kwa pima hata wakiingia katika shimo la mburukenge (yaani ndani ya shimo lenye mnyama anayeweza kukudhuru) mutaingia nao.” Wakauliza: “Je, unakusudia Mayahudi na Manasara?” Akasema: “Ni nani wengine ikiwa si wao”. [Imesimuliwa na Al Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Sa‘iyd al-Khudriy].

 

Ndio hali ambayo tunaishuhudia hivi leo. Wapo Waislamu hadi hii leo hawataki kuelewa tofauti yao na makafiri. Hata wakiwekewa dalili zilizo wazi, wanatoa hoja zisizokuwa na mashiko. Inafikia hatua Muislamu anasema: (mbona hizo dalili ulizotoa sioni maneno kwamba ‘Krismasi ni haramu’)). SubhaanaAllaah, yaani Muislamu anatafuta kisingizio cha kujifananisha na makafiri badala ya kutafuta njia nyepesi ya kuzipata radhi za Allaah. Anasahau kwamba Qur-aan ndio mwongozo wa Uislamu na inatoa dalili zake kwa mifano iliyo wazi:

 

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٧﴾

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Rabb wetu. Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal-‘Imraan: 7]

 

Tunaendelea kuwanasihi Waislamu kushikamana na mafundisho sahihi ya Uislamu. Halikadhalika, tutambue kwamba kila hatua ambayo tutaichukua hapa duniani itaenda kuulizwa mbele ya Hisabu. Sasa ni vyema Muislamu akatafuta ibada sahihi za kufanya badala ya kutafuta nyudhuru za kujifananisha na makafiri.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atughufirie madhambi yetu na Atuongoze njia iliyonyooka.

 

 

Krismasi 1: Jiweke Mbali Na Ghadhabu Za Allaah

Krismasi 2: Nabii ‘Iysaa ('Alayhis Salaam)

Krismasi 3: ‘Sala’ Zake Zimezidiwa Na Matamanio Ya Nafsi

 

 

Share