Anaweza Kufunga Ndoa Na Mwanaume Mshirikina Bila Ya Kitendo Cha Ndoa Hadi Asilimu? Hapati Waume Wa Kiislamu Naye Anataka Sitara

SWALI:

 

NIMESHAKUA MKUBWA NA NINATAMANI SANA KUWA KTK NDOA KWANI NAPATA SANA MITIHANI NA NAJIZUIA SANA NA KUIKARIBIA ZINAA, NASHINDWA KUVUMILIA KWANI SASA HIVI NIKO KTK HALI NGUMU SANA KIMAWAZO, LKN BAHATI MBAYA KILA ANAETAKA KUNIOA AMBAE NI MUISLAM WANATOA AHADI KISHA WANAISHIA KUNITESA ROHO YANGU HAWATIMIZI AHADI LKN KAJITOKEZA MWINGINE AMBAE NI MUSHRIKINA YEYE ANANIPENDA KIDHATI LKN NASHINDWA KUOLEWA NAE NINA IMANI NIKIOLEWA NAYE NAWEZA MSHAWISHI AINGIE KTK UISLAM NA PIA MIMI SIWEZI KUBADILIKA KUMFUATA, SWALI LANGU NI KUWA NIKUBALI TUFUNGE NDOA ILA NISIRUHUSU KITENDO CHA NDOA HADI ABADILIKE? YAANI LENGO LANGU NIPATE UHALALI WAKUWA KARIBU NAE KUWEZA KUMSHAWISHI KWANI KAMA TUNAVOJUA KUONGEA TU PASIPO NDOA NI KUKARIBIA ZINAA MNANISHAURI NINI MASHEIKH NIKO KTK WAKATI MGUMU NAUNGULIA ROHO KWANI HUYU NI MTU MZURI ANANIPENDA KIDHATI NA KUNITHAMINI, KAMA HAIFAI NIOMBEENI DUA NA MIMI NIPATE NIMPENDAE WA DINI YANGU NIOLEWE NIPATE STARA NA UTULIVU WA NAFSI NAPATA SHIDA SANA.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu hamu yako ya kupata mume Muumini atakayekujali.

Hakika ni kuwa hayo unayopitia, wewe si wa mwanzo wala hutakuwa wa mwisho. Mitihani kutoka kwa Allaah Aliyetukuka inakuja kwa njia nyingi sana. Mojawapo ni hiyo yako, kwa kuposwa lakini kisha ndoa kuharibika kwa sababu moja au nyingine.

 

Katika mtihani huu mgumu na mzito inatakiwa ufaulu kwa kuupita, la si hivyo basi utakuwa umekhasirika hapa duniani na kesho Akhera. Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo kuhusu mitihani:

Hapana shaka Tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri” (al-Baqarah [2]: 155).

Na pia:

Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? Hakika Tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na Atawatambulisha walio waongo” (Al-‘Ankabuut [29]: 2 – 3).

Inatakiwa dada yetu ujiytahidi uuvuke mtihani huu mbali na vishawishi vyote vinavyokukabili.

 

Ama wewe kufunga Nikaah tu na mshirikina Allaah Aliyetukuka Amekataza kabisa na hiyo si njia njema wala nzuri. Anasema Aliyetukuka:

Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanaume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Allaah Anaitia kwenye Pepo na maghfira kwa idhini Yake. Naye huzibainisha Aayah Zake kwa watu ili wapate kukumbuka” (Al-Baqarah [2]: 221).

 

Pia, unasema anakupenda, hakika ni kuwa pendo baina ya mume na mke linadhihirika baada ya watu kuoana kwa njia ambayo ni ya halali iliyokubaliwa na Allaah Aliyetukuka. Kwa hiyo, hakuna Nikaah hiyo katika Uislamu, na mbali ya kuwa unasema huwezi kushawishika lakini wapo wengi ambao wameshawishika kwa sababu eti anamvutia Mushrik katika Uislamu. Hivyo, kaa mbali naye na Allaah Aliyetukuka kwa sababu ya kusubiri na kumuomba kwako Atakupatia mume Muumini, mwema na mcha Mungu ili muishi katika hali iliyo nzuri.

 

Na kwa sasa kwa kuwa una matamanio yaliyo ya juu inabidi ufuate taratibu na maelekezo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kufunga ili kupunguza matamanio hayo. Na pia jishughulishe na mambo mengine ya halali ili ikutoe katika matamanio mpaka utakapopata mume.

 

Nasi tuko pamoja nawe katika kukuombea kwa Allaah Aliyetukuka ili Akuletee mume huyo atakayekuwa na kheri nawe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share