Zingatio: Krismasi 1: Jiweke Mbali Na Ghadhabu Za Allaah

 

Zingatio: Krismasi 1: Jiweke Mbali Na Ghadhabu Za Allaah

 

Naaswir Haamid

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameikamilisha Diyn kwa kututaka tumuabudu Yeye peke Yake. Yeyote atakayechagua njia isiyoelekea kwa Muumba wa mbingu na ardhi haitakubaliwa.

 

 

Wala hakuna njia iliyokamilika isiyokuwa na mashaka kama ya Uislamu. Waislamu wanajivunia kwa Uislamu wao sio kwa yale yanayozushwa ndani ya Diyn wala nje ya Uislamu. Wanaoiona tofauti baina ya Waislamu na wasio kuwa Waislamu ni wale waliousoma vyema na wakatekeleza maamrisho ya Uislamu. Diyn tukufu ya Uislamu haitaki makubwa kuyasukumiza wala madogo kuyachopoa. Naapa kwa Muumba Aliye kuwa Mmoja wala Asiyekuwa na mshirika kwamba Uislamu umekamilika.

 

 

Basi tutambue kwamba Uislamu wetu umekamilika na upo wazi kabisa kabisa. Atakayechagua njia nyengine isiyokuwa ya Uislamu, anajikaribishia ghadhabu za Muumba. Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba njia ya Uislamu ipo wazi:

 

Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Tulikuwa tumekaa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), akachora mstari mbele yake, akasema: ((Hii ni njia ya Allaah)). Kisha akachora mistari miwili upande wa kulia (wa huo mstari mkuu) na miwili upande wa kushoto yake, kisha akasema: ((Hizi njia za Shaytwaan)) Kisha akaweka mkono wake katika njia ya katikati akasoma Aayah hii:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam:  153; Imepokelewa na Imaam Ahmad na Ibn Maajah]

 

 

Katika mambo yaliyozushwa ndani ya Waislamu ni kuifanya siku ya kuzaliwa ni siku maalumu ya kusherehekea. Hali hiyo ikazoeleka hadi wakaanza kuiweka siku maalumu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Sio hayo tu, wakaifanya kuwa ni sikukuu, wakaiweka kwa kula na kunywa na wakajiweka mbali na kufanya kazi. Suala linakuja kwani hata sikukuu alizoziweka Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiziadhimisha kwa starehe tu? Balaa, sivyo hivyo, bali alikuwa akijikurubisha zaidi kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa ibada.

 

 

Sikukuu za Kiislamu zinakuja kutokana na kukamilisha nguzo kuu za Diyn tukufu. Ama iwe ya Swawm katika mfungo mtukufu wa Ramadhwaan ama ni kutokana na kukamilisha kisimamo kitukufu cha ‘Arafah. Kwa mwenye akili, atatambua kwamba Uislamu sio Diyn ya kuchezewa, inakwenda kwa malengo na mipango maalumu.

 

 

Mambo hayo ya kusherehekea uzawa wa mtu ndio yaliyopelekea Waislamu kutoona tofauti baina yao na wasio kuwa Waislamu. Wakaanza kujikurubisha na makafiri katika kila hali, sasa tunashuhudia mialiko na salamu za kheri zikitoka kwa Waislamu zikipelekwa kwa makafiri. Miongoni mwa masikitiko makubwa ni kule kupelekeana salamu za Krismasi. Wakaendelea kwa kujumuika nao katika kula, kunywa, mavazi na wengine basi wanafurutu ada hadi kwenda kusali pamoja nao Kanisani. 

 

 

Sherehe zina taathira kubwa katika akili na tabia ya mwanaadam. Ni lazima Waislamu kuacha kushirikiana katika maovu haswa kwenye mambo ya uzushi kama Krismasi. Naye Sayyidna ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Msijifundishe lugha ya Mushrikiyn – bila ya kuwa kuna umuhimu ndani yake – wala Msiingie makanisani wakati wa sherehe zao kwa sababu Hasira za Allaah huteremka juu yao.” [Al-Bayhaqiy].

 

 

Tunawanasihi kwa wale Waislamu waliojitayarisha kusherehekea siku hii isiyo eleweka asili yake hata kwa Wakristo wenyewe, kuachana na fikra hizo moja kwa moja. Kwa namna yoyote itakayokuwa, sisi ni Waislamu tusiotaka kuengezewa siku za kusherehekea, sikukuu zetu mbili zatutosha. Tuangalie huko mbele tumemfungia zawadi gani Rabb wetu Mtukufu.

 

 

Share