Zingatio: Kuwa Bwana Wa Nafsi Yako

 

Naaswir Haamid

 

Nafsi ni kama mtoto mdogo, haichoki wala hailali kutamani mambo. Na kawaida ya nafsi ni yenye kutamani maovu. Mfano mdogo tu, ni namna inavyopenda pumbazo za kidunia kama vile pombe, zinaa, ugomvi na kadhalika. Utaikutia nafsi ipo nyepesi kuyaingia mambo haya lakini ni nzito kujiweka mbali nayo.

 

Nafsi ni toto lisilosikia, kutwa lahitaji pembea.

Haijui halali kuhitajia, daima haramu huindea.

Nafsi Shaytwaani aipalilia, yeye machafu hukuwekea.

Yahitaji vita kuipigania, haramu usije kuyapendelea.

 

Nafsi sio rahisi kuilea kama alivyo mtoto. Mtoto haachi kudai utamu wa peremende, biskuti na vifaa vya kuchezea. Halikadhalika, nafsi nayo haiachi kukuamrisha kuangalia mambo yasiyofaa ili kutumbukia kwenye maasi. Inaamrisha kuyaacha yaliyo halali ili kuingia kwenye haramu.

 

Nafsi yahitaji kulelewa kwa kutenda ‘Ibaada. Na vile vile kupigana nayo ili kujiepusha kwenye kutenda maasi. Kwani kutenda ‘Ibaada sio kazi rahisi, ni kazi yenye kuhitaji subira ya hali ya juu. Lakini hakuna njia rahisi ya mafanikio ila ni kujihimiza kwenye yale mashurti yaliyowekwa ili kufanikiwa na kile unachokitafuta. Hivyo yahitaji juhudi ili nafsi izowee kutenda mema.

 

Tumechagua wetu Uislamu, njia nzuri muafaka.

Njia isio na pekee matamu, inadai jasho kukutoka.

Ndivyo waliopita Waislamu, muda kupoteza hawakutaka.

Maisha yao hatamu, ni damu machozi kuwatoka.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema kwa wale wenye kujitahidi:

 

{{Na anayejitahidi, bila shaka anajitahidi kwa ajili (ya maslaha) ya nafsi yake; Kwa hakika Mwenyezi Mungu si Muhitaji) wa walimwengu}} [Al-‘Ankabuut: 6]

 

Daima tukumbuke kwamba tunapojikubalisha, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atatuonesha njia insha Allaah. Kasema Mtukufu wa Mbingu na Ardhi:

 

{{Na wale wanaojitahidi kwa ajili Yetu, kwa yakini Tutawaongoza kwenye njia Zetu. Na bila shaka Mwenyezi Mungu Yu pamoja na wafanyao wema}} [Al-‘Ankabuut: 69]

 

Tukirudi nyuma kwenye Taariykh ya Uislamu, tunaona kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) na watangu wema walikuwa hawana masikhara kwenye ‘Ibaada, ama kuswali, kufunga na kujishughulisha kwenye elimu na Ijtihaad nyenginezo. Muda mrefu wa usiku ulikuwa ukitumika kwa kuomba toba au kutafuta elimu.

 

Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa maisha ya Muislamu na ndivyo kufuzu katika Dunia hii kwa kutarajia kunufaika na maisha ya milele kesho Akhera insha Allaah.

 

Tumuombe Allaah Atujaalie tuwe katika wale mabwana wa nafsi zao, sio watumwa wa matamanio yao. (AAMIYN).

 

 

 

Share