Amekuwa Mbali Na Dini, Matatizo Yanamwandama Na Hajui La Kufanya

SWALI:

 

Assalamualeikum warahmatullahi wabarakatuh rehma za Allaah subhanahu wataala ziwe juu yenu.amin.

 

mimi ni mwanamke,nilikua nimeshika dini sana wakati nlipokua sijapata kazi,saivi nimepata kazi najitahidi nipate muda wa kusoma quran na kufanya ibada zangu nyingi lakini naposhika quran au kutaka kusoma tasbihi naingiwa na usingizi..wallah najitahidi kuongea na watu maneno mazuri anayopenda allah subhanahu wataala bado naambiwa mie mjeuri kwa kua watu wengi hawaapendi uwaendee kinyume na wanavotaka wao uende...nalia na naumia sana kuwa mbali na dini yangu na najiona nateseka sana sijui nifanyeje! nataka niwe nauliza maswali yangu humu kwa wingi lakini yanachelewa kujibiwa basi huwa sina mwengine wa kumwambia please nawaomba musichelewe kunijibu ndugu zanguni napata shida sana...

 

ahsante.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako la kutafuta ufumbuzi wa kurejea kuwa karibu na dini.

 

Ndugu yetu, ni vyema tuelewe kuwa Qur-aan iko wazi kuwa mwenye kushikamana na mambo kama haya ya kuwaeleza watu kufanya mema na kuachana na mabaya kama hivi:

 

“Ewe mwanangu! Simamisha Swalah, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayokupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa” Luqmaan: 17.

 

 

Hivyo basi, kama kweli uko kama hivyo ulivyojieleza basi ushauri wa Qur-aan ndio kama huo hapo ‘subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa’ na tarajia malipo kutoka kwa Allaah na usiwe na haja ya kutaka kuwaridhisha watu kwani huna uwezo huo hata kama utaona kuwa unaweza hiyo ni ndoto ya mchana.

 

 

Hivyo basi huna haja ya kulia wala kuumia, huna haja ya kujiweka mbali na dini wala huna haja ya kujiona kuwa unateseka; kwani hakuna baya litalokugusa, na hakikisha kuwa unafuata yanayomridhi Allaah; uliyonayo hayo yote ni mawazo anayoyapandikiza Shaytwaan katika nafsi yako ili ujione hivyo unavyojiona, hivyo basi unachotakiwa kushikamana nacho kila yakikujia mawazo kama hayo ni kurudi kwa Mola na kumtaka msaada Wake Akuepushe na Shaytwaan na kumuomba Akuwafikishe kushikamana na kauli Yake kama hii:

 

“…. Allaah Anatutosha, naye ni Mbora wa kutegemewa. Basi wakarudi na neema na fadhila za Allaah. Hapana baya liliowagusa, na wakafuata yanayomridhi Allaah. Na Allaah ni Mwenye fadhila kuu. Hakika huyo ni Shaytwaan anawatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini.” Aal-‘Imraan: 173-175.

 

 

Pia soma Du'aa zifuatazo zikusaidie kuthibitisha iymaan yako Inshaa-Allaah.

 

 

 اَللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك

Allaahuuma Yaa Muqallibal-Quluub Thabbit Qalbiy 'Alaa Diynik

(Allaahuumma, Ewe Mgeuza nyoyo, thibitisha  moyo wangu katika Dini Yako(

اّللَّهُمَّ ياَ مُصَرِّفَ الْقُلُوب صَرِّف  قُلُوبَناَ عَلَى طَاعَتِك         

Allaahuumma Ya Muswarrifal-quluub Swarrif Quluubana 'Alaa Twaa'atik

(Allaahumma, Ewe Muelekezaji wa nyoyo, Elekeza nyoyo zetu katika Twa'aa Yako

 

Na  Adhkhaar za asubuhi na jioni, na pamoja na Du'aa nyingi mbalimbali zilioko katika kitabu cha Hisnul Muslim kilochoko Alhidaaya. Bonyeza kiungo kifuatacho:  Hiswnul Muslim

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share