Anapata Matatizo Na Meneja Wake Kazini Nchi Za Kigeni

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum swala langu leo, ilikuwa naomba kupata maoni kutoka kwenu, maoni yenyewe ni kuhusu kazi ninayofanya, mimi niko London na ndiko nnako fanya kazi, sasa basi huko kazini yuko mzungu mmoja ambae yeye ndio manager lakini ananichukia sana mimi sijui kwa nini ananifanyia madharau sana hanifanyi usawa kama anavyo wafanyia wengine, na mengineo baya, sasa naomba maoni yenu nifanye nini ahsantum.     

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupata matatizo kazini.

Hakika ni kuwa kazi nyingi hapa duniani zina matatizo na mitihani. Wewe si wa kwanza kupata matatizo hayo wala hutokuwa wa mwisho. Na ni hakika wapo Wazungu ambao ni wazuri kwa muamala wao na wafanyakazi walio chini yao na wengine ni waovu na wabaguzi.

 

Nasaha ambazo tunaweza kukupatia ni kama zifuatazo:

 

1.     Huenda Mzungu huyo ana nadhariya zake kukuhusu wewe. Ima hajakuelewa vyema au anaona hutekelezi kazi yako inavyohitajika, au unazembea au sababu nyingine yoyote. Hivyo, unatakiwa uwe na ujasiri wa kuweka miadi naye ili umueleze unayohisi akilini mwako. Kwa kumuelezea kinaganaga huenda yakajitokeza mengi katika hayo mazungumzo. Huenda akakuelezea anayoona ni makosa kwa upande wako au kukiri kuwa kweli amefanya makosa hivyo ajirekebishe.

2.     Mripoti kwa Meneja mkuu, au waone Jumuiya ya Wafanyakazi kama mnayo hapo kazini waweze kuzungumza naye ili akupe haki zako kama wafanyakazi wengine.

3.     Kuomba Du’aa katika kila nyakati ambazo du’aa inakubaliwa kama unapoamka usiku kwa ajili ya Tahajjud, unapokuwa umefunga, baina ya Adhaan na Iqaamah na nyakati nyingine. Muombe Allaah Aliyetukuka Akutengenezee mambo yako na Akuepushe na shari hizo.

4.     Swali Swalah ya Istikhaarah utake ushauri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa jambo ambalo linafaa wewe ufanye katika tatizo hilo ulilo nalo.

5.     Huenda kazi hiyo ikawa haina kheri nawe, kwako binafsi au kwa dini yako kwa zote mbili. Hivyo, kitu ambacho unaweza au unatakiwa kufanya ni kutafuta kazi sehemu nyingine. Pindi tu utakapopata, basi aacha hiyo uende kufanya huko kwengine.

 

 

Twataraji kuwa kwa kufanya hayo ufumbuzi utapatikana kwa njia ambayo utapata furaha, na kuondoka katika shida usisahau kumkumbuka Allaah Aliyetukuka kwa kuswali inavyotakiwa, kufunga, kutoka Zakaah na Sadaqah na kuleta Adhkaar za kila wakati.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share