Kufanyia Biashara Pesa Za Amana Haifai?

 

SWALI:

JE PESA ZA AMANA NNAWEZA KUFANYIYA BISSNES NA LAZIMA MWENYEWE AJUE? NA FAIDA YAKE NNAHAKI KUCHUKUA NA KIASI GANI KTK 100? SHUKURAN

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Suala hili ni muhimu hasa katika wakati wetu wa leo ambao katika mambo yaliyoelezwa na Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kupotea kwa amana.

Kutunza amana ni miongoni mwa sifa nzuri ya Muislam na ukosefu wake unamuingiza mtu katika unafiki kulingana na muongozo wa kipenzi chetu al-Mustwafaa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokewa na 'Abdallah bin 'Amru bin al-'Aasw (Radhiya Allaahu 'anhuma), kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mambo manne mwenye kuwa nayo ni mnafiki kamili. Ikiwa mojawapo ya tabia hizo inapatikana kwa mtu, basi ana alama ya unafiki mpaka aiache. Anapoaminiwa hufanya khiyana, anapozungumza anasema uongo, anapoahidi anadharau (hatekelezi) na anapogombana haamuliki" (Imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim. Pia tizama Riyadhus Swalihiyn Hadiyth nambari 690).

 Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza: "Enyi mlioamini! Timizeni ahadi" (5: 1).

Ipo kanuni ya msingi ya Kiislam aMbayo inasema: "Waislamu wapo katika masharti waliyowekeana". Hivyo, ni jambo linaloeleweka kuwa ukiacha amana, sahibu wa amana hiyo anaacha na maagizo yake ambayo wewe unakubali au unakataa. Ukikataa amana hiyo haibaki kwako bali mwenyewe ataichukua na kutazama sehemu nyingine ya kuihifadhi. Ukikubali kufanya hivyo inamaanisha mumekubaliana kwa hayo masharti na ikiwa mumeafikiana haitofaa kabisa kisheria kwako kuitumia kwa njia yoyote nyingine kama kuifanyia biashara au kwa matumizi mengine.

Mara nyingi mtu anaweka amana na agizo, nikiitaka wakati wowote nitakuja kuichukua. Mfano ikiwa sharti ni hilo nawe ukaanza kuitumia katika biashara zako na mara mwenyewe akaja kuitaka, utafanyaje? Ikiwa amekupatia ruhusa ufanye chochote unachotaka kwa amana hiyo nawe ukaitumia kwa biashara ukipata faida utaangalia kiwango muafaka umpatie mwenye amana, lakini ukipata khasara utamrudishia amana yake kikamilifu.

Ikiwa amana iliyotolewa ni makhsusi kwa biashara kwa kuwa mmoja anatoa rasilmali na mwengine anatumia ujuzi na nguvu zake inabidi waandikiane mkataba baina yao. Katika shughuli hii ya kibiashara, faida inayopatikana watagawana kulingana na mapatano yao hayo na wakipata khasara pia watagawana baina yao.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share