Kufupisha Thanaa: Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”

 

Kufupisha Thanaa: Ufafanuzi Wa Kiburi Na Mas-ala Ya

Bid’ah Katika Jibu La “Hukmu Ya Kufupisha Thanaa”   

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Baada ya kusoma jibu katika kiungo kifuatacho:

 

Hukmu Ya Kufupisha Kumtukuza Allaah Na Kumswalia Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam Na Maamkizi Ya Kiislam

 

Nakubaliana ni vizuri kuandika kirefu. Ispokuwa   Rasul   hakukataza  wala hakusherehesha kuhusu  kufupisha  ila  kwenye salaam  nayo wapata thawabu hata kidogo.  Lakini nanukuu kipande cha mwisho cha fatwa hiyo:

 

"Hivyo basi haifai kufupisha kwani ni kujikosesha thawabu na fadhila zinazopatikana katika kumtukuza na kumhimidi Allaah na kumswalia Mtume na pia kutoa Salaam kwa ukamilifu, na pia ikiwa mtu atafikiwa na ufafanuzi huu na akaendelea kuifanya hayo, basi ni alama ya kiburi na huenda asikose tu thawabu za kuandika, bali huenda akapata na dhambi za kufanyia kiburi haki".

 

Nakbaliana na karibu na maelezo yote na ushahidi uliotolewa. Lakini ushahidi uliotolewa kwa hadith wote umetolewa kuhusu hukumu ya salaam. Fatwa zilizotolwa ni kuhusu Nabiy Swalla Allaahu 'alaiyhi wa salaam hakulifanya. Je mangapi mtume hakuyafanya na halali kuyafanya sasa. Mfano, Sasa tuko kwenye karne ya 21 mambo mengi hayakuwapo wakati wa Rasul Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam mfano mdogo vipando. Wakati ule walikuwa wakipanda Ngamia na farasi huchukua muda mrefu na sasa twatumia Ndege nayo watu hutumia muda mfupi.  Hata vita ya sasa haipiganwi na mapanga tena yapiganwah na mabomu kutumia satalite. Na mengi mengineyo  yote haya twakubali ni Elmu aliyotupa Allaahu Subhaanahu wa Ta'aalaa na ni halali kuyatumia.  Sasa  wasiwasi  wangu  ni huu  wa  fatwa  hii  ya  kumtia  mtu  Alama  ya Kibri Imetoka Wapi Kama Ilivyo Katika  maneno  hayo  hapa  juu     "na pia  ikiwa  mtu  atafikiwa  na  ufafanuzi  huu  na  akaendelea kuifanya    hayo, basi ni alama ya kiburi"
 

 

Nakumbusha kuwa si pingi hiyo Fatwa ninacho kuwa na wasiwasi nacho nihukmu ya kupewa mtu kuwa na Kibri. Ikiwa hilo jambo limepitishwa (fatwa) na viongozi waliopo sasa je wakipita hao wakija wengine wakisema yafaa itakuwaje.Tukumbuke mwenye sifa hiyo ni Allaahu Subhaanahu wa Ta'aalaa Peke Yake.

 

 

Wabillahi Tawfiq.
 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tuanze kwanza kukujibu kuhusu  suala la kiburi katika majibu tuliyoyaweka.

 

 

Baada ya kubainika kwa hoja zilizotolewa kwenye majibu hayo ya 'ulamaa ambao wamechambua mas-ala kwa hoja zenye kufahamika na zenye egemezo na Sunnah, kisha mtu akayasoma na kuendelea kufanya kinyume, basi hiyo ni dalili ya kiburi, kwani kiburi ndugu yetu ni kukataa haki. Na haki ni kuwa tayari yashatolewa maelezo kuhusu ubaya wa kumkatia Allaah na Nabiy Wake heshima zao na utukufu wao na hali wewe ni Muislamu ambaye unadai unawapenda na kuwaheshimu. Bila shaka si heshima kumkatia Rabb wako au Nabiy wako hadhi zao wanazostahiki na kufanya hivyo baada ya kukumbushwa, basi itakuwa ni alama ya kiburi ila kwa yule aliyesahau ambaye atasamehewa na shari'ah.

 

Na kusema kiburi ni nafuu kuliko kumwambia mtu kuwa: 'Wewe unamchukia Allaah au unamchukia Mtume kwa sababu unawavunjia heshima'! Au kumtuhumu mtu kuwa hampendi Allaah au Nabiy kwa kuwakatakata hivyo! Au kumwambia mtu: “Hakika wewe una dharau kwa Rabb wako na Nabiy Wako!”  Na yote hayo yanaweza kusemwa na watu lakini sisi tumechagua neno muwafaqah ambalo tunahisi ni mahali pake na wala hatujahalalisha haramu hapo au kuharamisha halali kama ulivyofahamu wewe katika maelezo yako.

 

Na vizuri ufahamu kuwa hatujamtia mtu alama ya kiburi bali tumesema ikiwa mtu ataendelea kufanya hayo kinyume kwa kumkata heshima Allaah na Nabiy Wake na baada ya kubainishiwa madhara na kukosa fadhila kwa kufanya hivyo, basi itakuwa ni alama ya kiburi; yaani kwa kukataa kwake haki. Na hakuna asiyefahamu au asiyekubali kuwa katika hayo mawili ya kufupisha na kukata na kurefusha heshima hizo, kuwa ya pili ya kurefusha ni bora na yenye thawabu. Sasa kwa mwenye akili, atawezaje kuliacha lililo bora na thawabu na kulifuata lisilo bora wala lenye thawabu?

أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ ۚ

... Kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora? [Al-Baqarah: 61]

 

 

 

Ama kuhusu nukta yako nyigine ya pili, tunatakiwa tufahamu nini maana sahihi ya bid'ah kwanza na ndio utata ulionao utaweza kuondoka:

 

Bid'ah katika istilahi ya kisheria  ina maana njia iliyoanzishwa katika dini, inayoshabihiana na ile njia ya kisheria (lakini kwa hakika si hivyo, yaani inakwenda kinyume na sheria), hivyo wanazua bid'ah kwa kusudi ya kuwa na ada ya kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka (hii ni kuwa haiwatoshelezi yale yaliyokuja katika sheria na hivyo wanataka kuongeza juu yake kama kwamba wanakamilisha yaliyopungua)”. [Imaam Abu Ishaaq ash-Shaatwiby, al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 37]

 

Naye Shaykh Abdulla Saleh Farsy amesema, “Bidaa iliyokusudiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukatazwa ni kutiwa katika Dini – na kuitakidiwa kuwa ni Ibada jambo ambalo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema litiwe katika Dini wala hakulifanya, na hali ya kuwa anao uweza wa kulifanya”. [Bid-a, Dibaji].

 

Imaam Maalik amesema: “Yeyote atakayeanzisha katika Uislamu bid'ah akiona kuwa ni nzuri amedai ya kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya khiyana katika kufikisha risala, kwani Allaah Amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.  [Al-Maaidah:3]

 

 

Na kwa yule ambaye hakuwa na dini siku hiyo basi hatakuwa na dini leo” [al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 49 ya Imaam ash-Shaatwiby]

 

 
Imaam Ahmad amesema: “Misingi ya Sunnah kwetu sisi ni kushikamana na yale waliyokuwa nayo Swahaba wa Nabiy, kuwafuata na kuacha bid'ah kwani kila bid'ah ni upotevu” [Ibn Ya’la al-Fara’, Twabaqaatul Hanaabilah, Mj. 1, uk.241]
 

 

Ibn Rajab naye anasema: “Maana ya bid'ah ni yale yaliyoanzishwa ambayo hayana asili katika sheria yenye kuwafikiana nayo, na ama yale ambayo yana asili katika sheria basi sio bid'ah, japokuwa ni bid'ah kilugha (kumaanisha kuwa kwa matumizi ya lugha ya Kiarabu inafahamika hivyo lakini kisheria inakuwa ni kinyume na hayo matumizi ya kilugha)” [Jaamiul ‘Uluum wal hikam, uk. 233]

 

Katika maelezo hayo yameweka mipaka ya kwamba bid'ah sehemu yake ni katika dini na wala si katika mambo ya kidunia, na hiyo ni kuwa "ni njia iliyoanzishwa". Na dalili katika hili ni kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

"Mwenye kuzua katika dini yetu hii lisilokuwamo humo litakataliwa" [Al Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na katika baadhi ya riwaya nyengine:

 

 

"Yeyote atakayezua katika hili jambo letu – na makusudio pia (jambo letu la dini) lisilokuwamo humo, litakataliwa". [Al Bukhaariy, Muslim, Abu Dawuud na Ibn Maajah]  Yaani itakataliwa kutoka kwa mwenye kufanya kama zinavyorudishwa hela mbaya kwa mwenyewe.

 

Hivyo bid’ah haiwi isipokuwa katika dini. Na hapa wengi tunakosea kwa kudhania ya kwamba bid’ah inaingia katika mambo ya ada. Vitu vya kawaida haviingii katika bid'ah. Haiyumkiniki kusemwa kuwa: jambo hili katika mambo ya kimaisha ni bid'ah kwa sababu ma-Salaf miongoni mwa Swahaba na Tabiina hawakufanya. Inawezekana kuwa ni jambo jipya lakini haichukuliwi kuwa ni bid'ah kisheria na kama si hivyo basi tungechukua mengi ambayo tuko nayo leo kuwa ni bid’ah: kama hivi vipaza sauti, mazulia (carpets), hii meza, na hivi viti ambavyo tunakalia, vyote havikuwepo kwa wale Waislamu wa mwanzo na havikufanywa na Maswahaba. Je, hizi zinachukuliwa kuwa bid'ah?

 

 

Na hivyo hukosea wengi katika watu katika jambo hili mpaka wanapoona, kwa sikitiko, minbar yenye zaidi ya vidaraja vitatu wanasema: ‘Hii ni bid’ah’. Hapana! haiingii bid'ah katika jambo hili. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihutubu mwanzoni juu ya kigogo cha mtende lakini watu walipokuwa wengi aliambiwa, “Je, hatukufanyii kitu ambacho utasimama kwayo mpaka watu wakuone?” Wakaja na fundi seremala ambaye alikuwa Mrumi na kumtengezea minbar yenye vidaraja vitatu na lau jambo hili lingehitajia zaidi ya vidaraja vitatu wangefanya. Mambo haya hayaingii katika bid'ah. Na hizi ni katika ada ambazo kwamba zinatofautiana kwa kutofautiana kwa watu, mazingira na hali. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akila kufuatia ada za kaumu yake na hasa yenye kuafikiana na maumbile yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), maumbile ya usahali (wepesi), unyenyekevu na kujinyima. Hivyo haichukuliwi kuwa kula juu ya meza au kula kwa kijiko kuwa ni bid'ah katika dini.

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho na usome ‘Hoja Ya Tisa Ya Watetezi Wa Maulidi’ ambayo imefafanuliwa zaidi kuhusu mas-ala haya na hasa uliyoyataja ya kuwa Nabiy (Swalla-Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda ngamia sasa vipi sisi tupande gari, ndege n.k.

 

 

Hoja Za Wanaosherehekea Mawlid Na Majibu Yake

 

Tunadhani  tutakuwa tumefafanua kiasi cha kufahamika vizuri inshaAllaah

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share