Skip navigation.
Home kabah

Sikilizeni! Kwa Kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى Nyoyo Hutulia

16 Rabiy'ul Awwal 1427 -14-04-2006

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

((الَّذِينَ آمَنُواْ وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللّهِ أَلاَ بِذِكْرِ اللّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ))

((Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!)) [Ar-Ra'ad 28]

 

Fadhila za kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى ni nyingi sana zilizotajwa katika Qur'aan na Sunnah, mojawapo ni utulivu wa moyo kama ilivyo katika Aayah hiyo tukufu. Vile vile Hadiyth kutoka kwa Abu Musa Al-Ash'ariyyi  رضي الله عنه kwamba  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema :

   ((مثل الذي يذكر ربه والذي لا يذكر ربه مثل الحي والميت))

((Mfano wa anaemtaja Mola wake na asiyemtaja ni mfano wa aliye hai na maiti)) [Al-Bukhaariy]

Kisha Anasema Allaah سبحانه وتعالى kuwa tukimkumbuka na Yeye Atatukumbuka:

 (( فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُواْ لِي وَلاَ تَكْفُرُونِ ))

 ((Nitajeni Nami Nitawataja, na nishukuruni na wala msinikufuru)) [Al-Baqarah: 52]

Na pia Ametuamrisha tumkumbuke sana:

  ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّهَ ذِكْراً كَثِيراً))

 ((Enyi mlioamini mtajeni Mwenyezi Mungu sana))[Al-Ahzaab: 41]

Kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى ni katika kitendo bora kabisa kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:

 قال صلى الله عليه وسلم : (( ألا أنبئكم بخير أعمالكم وأزكاها عند مليككم، وأرفعها في درجاتكم ، وخير لكم من إنفاق الذهب والورق ، وخير لكم من أن تلقوا عدوكم فتضربوا أعناقهم ويضربوا أعناقكم؟)) قالوا بلى .قال : ((ذكر الله تعالى))  أحمد  و غيره 

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Hivi niwaambieni khabari  ya matendo yenu bora, na ambayo ni masafi mno mbele ya Mola wenu, na ambayo ni ya juu mno katika daraja zenu, na ambayo ni bora kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, na ambayo ni bora kuliko  kukutana  na adui zenu, mkawapiga shingo zao?)).  Wakasema Maswahaba: Ndio. Akasema  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : ((Ni kumtaja Allaah)) [Ahmad na wengineo]

Ukumbusho bora kabisa ni kusoma maneno Yake Allaah سبحانه وتعالى nayo ni Qur'aan. Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha aina nyingi za kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى  zenye fadhila nyingi kabisa, chache zifuatazo:

Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    ((Mwenye kusema:

سُبْحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ

 Subhaana Allaahi Wa Bihamdihi 

 Ametakasika Allaah na sifa njema zote ni Zake

…… kwa siku mara mia, atafutiwa madhambi yake hata kama yalikuwa mfano wa povu la bahari)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  

Na amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   ((Kusema kwangu :

 سُبْحَانَ اللهِ، والحَمْدُ للهِ،  وَ لاَ إِلَهَ إلاَّ اللهُ واللهُ أَكْبر   ُ

Subhaana Allah Wal-HamduliLLah, Wa La Ilaaha Illa Allah, Wa Allaahu Akbar

Ametakasika Allaah na sifa njema zote ni za Allaah na hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Allaah na Allaah ni Mkubwa,

……….. ni bora kwangu kuliko kila kilichoangaziwa na jua))  [Muslim]

 

Na amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم : ((Atakayesema:

لا إِلهَ إِلَّا اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْد، وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قدير ٌ

Laa ilaah Illa Allahu Wahdahu Laa Shariyka Lahu Lahul-Mulku Wa Lahul-Hamdu Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr.

 Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa peke Yake Hana mshirika ni Wake Ufalme na ni Zake kila sifa njema na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.

….. mara kumi, ni kama (thawabu za mtu) aliyeacha huru nafsi nne katika wana wa Ismaa'iyl)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

Na amesema Mtume صلى الله عليه وسلم :  ((Hivi anashindwa mmoja wenu kuchuma kila siku thawabu elfu?)). Mtu mmoja miongoni mwa waliokaa akamuuliza “Atachuma vipi mmoja wetu thawabu elfu?  Akamjibu ((Aseme :

 

سُبْحَانَ اللهِ

 Subhaana Allaah

 Ametakasika Allaah

……. Mara mia moja, basi ataandikiwa thawabu elfu moja,  au atafutiwa madhambi elfu moja)) [Muslim]

 

 

 

************