Amali Itakayokupatia Thawabu Kama Za Hajj Na 'Umrah Kila Siku!

 

‘Amali Itakayokupatia Thawabu Kama Za ‘Hajj na Umrah’ Kila Siku!

 

Alhidaaya.com

 

 

Ukitaka kupata thawabu za Hajj na ‘Umrah bila ya safari, gharama na tabu zake, bakia kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya kuswali Jamaa Alfajiri ukiwa Msikitini hadi jua lichomoze kisha swali Rakaa mbili za Sunnah kutokana na Hadiyth:

 

عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الفَجْرِ في جَماعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ الله تَعالى حتَّى تَطْلُعَ الشَمْسُ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ كانَتْ كأجْرِ حَجَّةٍ وَعُمْرَةٍ تامَّةٍ تامةٍ تامةٍ)) أخرج الترمذي وصححه الألباني

 

Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa kisha akakaa anamdhukuru Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Rakaa mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy].

 

Tanbihi: Hadiyth hiyo wamekhitilafiana ‘Ulamaa usahihi wake, kuna waliosema ni dhaifu na wengineo wameipa daraja ya Hasan kama Imaam Al-Albaaniy.  

 

 

 

Jitahidi ndugu Muislamu kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma bila ya kusafiri. Mwanamke anaweza pia kujichumia thawabu hizo akiswali nyumbani kwake.

 

Hata hivyo, pamoja na ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa kumetengua wajibu wake wa kufanya Hajj au ‘Umrah.

 

 

Juu ya hivyo imethibiti katika Swahiyh Muslim kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani kutokana na Hadiyth:  

عَنْ صَخْرٍ الْغَامِدِيِّ رَضِيَ الله عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((اللَّهُمَّ بَارِكْ لِأُمَّتِي فِي بُكُورِهَا))  الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن ماجه 

Kutoka kwa Swakhar Al-Ghaamidiyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameomba: ((Ee Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuwd, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy].

 

 

Wakati huo wa baada ya Swalaah ya Alfajiri hadi kuchomoza jua, ni wakati wenye Baraka tele kwani Swahaba walikuwa wakibakia kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na wakitumia wakati huo kwa kuanzisha shughuli zao mbali mbali. Pia imesimuliwa kutoka Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa) alimkataza mtu kulala nyakati hizo kwa vile ni wakati wa kugaiwa rizki.

 

Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema: "Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"   

 

Pia, wakati huo wa baada ya Swalaah ya Alfajiri kabla ya kuchomoza jua, pamoja na baina ya Swalaah ya Alasiri na kuzama jua ni nyakati ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameamrisha kumsabbih kama Anavyosema:

 

وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾

“Subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.” [Qaaf: 39].

 

 

Tujitahidi kutekeleza hayo tukimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atupe tawfiyq na Atutakabalie.

 

 

 

 

 

Share