Kumpenda Kikweli Nabiy (صلي الله عليه وسلم)

Kumpenda Kikweli Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

عَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اللّه عَنْهُ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((لا يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى أَكونَ أحَبَّ إِلَيْهِ مِنْ وَالِدِهِ وَوَلَدِه وَالنَّاسِ أَجْمَعينَ )) متفق عليه

Imesimuliwa na Anas bin Maalik. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Sallam): “Hatoamini mmoja wenu mpaka niwe (mimi Muhammad) kipenzi chake kuliko mwanawe na wazazi wake na kuliko watu wote waliobakia.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mada hii ya kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ina umuhimu wake mkubwa katika kukamilisha imani ya mja, na Waislamu wengi hawafahamu vyema maana halisi ya kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Neno محبة   ni neno la Kiarabu kilugha lina maana ya; Hisia za kumili kwa moyo. Na katika Shariy’ah, ni kumili kwa moyo kunako ambatana na kiwiliwili, hisia, akili, matakwa, na matendo ya moyo yanayothibitishwa na matendo ya viungo. Na hiyo ndio Imani.

 

Imani kwa mtazamo wa Ahlus-Sunnah wal Jama’ah ni kauli na matendo, yaani kauli ya moyo na ulimi, na matendo ya moyo na viungo. Kwa maana hii ya ki- Shariy’ah, mapenzi huwa na uhusiano moja kwa moja na Imani ya mtu.

 

Lakini kama mtu atatafsiri mapenzi kwa maana ile ya kilugha, yaani kumili kwa hisia za moyo tu, mapenzi ya mtu huyu yatakuwa na dosari kubwa, na yatakuwa yanahukumiwa na matamanio zaidi kuliko Imani, na huu ndio mtihani uliowasibu wengi katika Ummah wetu, wa kutotofautisha baina ya mapenzi ya kiimani, na mapenzi ya kumili kwa hisia za nyoyo.

 

Mtu anaweza kumpenda mtu mwengine kwa hisia hizo za kumili kutokana na vigezo vyake, lakini akawa bado anatofautiana naye katika mambo mengi, na wakati mwingine hakubaliani nae katika mitazamo yake na kauli zake, lakini bado moyo wake ukawa unamili kwa mtu huyo, tafsiri kama hii ya mapenzi ndio iliyowapotosha wengi miongoni mwa Waislamu kwa kudhani kuwa mapenzi ya aina hii, ni mapenzi yenye uhusiano na Imani.

 

Moja miongoni mwa misingi mikuu ya Imani ya Dini yetu ni kumpenda Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)    kuliko tunavyozipenda nafsi zetu na ukimuuliza Muislamu yeyote duniani atakuthibitishia mapenzi makubwa aliyonayo kwa kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini tunatofautiana katika uelewa wa jinsi ya kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mujibu wa tafsiri tulizozitaja hapo juu.

 

Wapo miongoni mwetu ambao ukimtaja tu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kububujikwa na machozi kwa hisia kali alizonazo juu ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mwengine atatoa sauti kali ya kumtakia rehma na amani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema kwa vishindo “Allaahumma salim alayhi.” Wengineo waliozuka siku hizi na kuleta itikadi yao ya kutukana Swahaba, utawakuta anapotajwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huitikia kwa vishindo “Allaahumma Swalli ‘alaa Muhammad wa aali Muhammad.” Lakini ndio hao hao wanautukana wake zake na Swahaba zake!  Na si ajabu ukawakuta watu hao pamoja na mapenzi makubwa wanayoyaonyesha kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawatimizi Swalaah tano kwa siku, wake zao na mabinti zao hawajisitiri, wana vimada nje, nyumba zao zimejaa taarabu za rusha roho, zimepambwa na vinyago na mapicha, wavuta sigara, wala mirungi, wakaa mabarazani kusengenya, panapoadhiniwa na kukimiwa hawasimami kwenda kuswali na Waislam,  achilia mbali kupuuza kwao baadhi ya Sunnah muhimu kama vile kufuga ndevu n.k. Watu hawa wana mapenzi makubwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini ni mapenzi ya aina gani ? je, haya ndio mapenzi ya kiimani?

 

Neno mapenzi katika Uislaam lina maana nzito sana, haifai kulichukulia kwa maana nyepesi nyepesi kwani lina uhusiano mkubwa na ‘Aqiydah ya Dini yetu; Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema katika Qur-aan:

 

 وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ..﴿١٦٥﴾

“Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah.” [Al-Baqrah:165]

 

Kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni katika alama za Tawhiyd, kama ilivyobainisha Aayah, na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndio msingi wa kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Huwezi kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kabla hujatimiza mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Na huwezi kumpenda Allaah kwa kumkwepa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Vigezo Vya Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

 

1-Kuthibitisha Shahada Ya Unabii Wake

 

 

Ni kuthibitisha Unabii wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni Rasuli aliyetumwa kwa waja wote, kuthibisha kivitendo yote aliyoyaamrisha, na kujiepusha na yote aliyoyakataza na kuyakemea, kwa maana nyingine ni kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Alivyofundisha na kuelekeza Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Allaah Anathibitisha hayo kwa kusema:

                                                                                                   

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Al-'Imraan: 31] 

 

Allaah Anathibitisha kuwa, ili mja awe na Tawhiyd iliyokamilika ya kumpenda Allaah, basi ni lazima amfuate Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndio kisha Allaah Atampenda mja huyo na kumghufuria madhambi yake. Hivyo basi, mapenzi ya kweli yanakuwa kwa kumfuata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika yote aliyokuja nayo na kumtii na ndipo Allaah Atampenda mja huyo, na atakayebahatika kupendwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), hakika huyo amefaulu kufaulu kulikokuwa kukubwa.

 

 

2-Kumuiga Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)     

 

Mapenzi ya kweli ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanakuwa ni kwa kumuiga kwa yote aliyokuja nayo, kumuiga katika tabia zake, katika maisha yake, katika nyumba yake, katika ibada zake, katika mahusiano yake na majirani, na katika maisha yake kwa ujumla, kama Anavyotuambia Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا ﴿٢١﴾

“Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi.” [Al-Ahzaab: 21]

 

Kumuiga Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumfanya kuwa ruwaza njema ndio mapenzi ya dhati ya kumpenda Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumsifu tu, na akawa hana nafasi katika maisha yako na maisha ya familia yako, basi huko si kumpenda bali ni kujifanya kumpenda na inawezekana ikawa ni kumcheza shere.

 

Katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Abdu-Rahmaan bin Quraad (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anatawadha, na Swahaba wakaanza kukinga maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka katika wudhuu wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakijifutia katika miili yao kutafuta baraka za wudhuu ule kutoka kwa Nabiy. Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza: “Kwa nini mnafanya hivi?” Wakasema; ni kwa ajili ya kumpenda Allaah na Rasuli Wake. Nabiy  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia: “Anayetaka kumpenda Allaah na Rasuli Wake, au kupendwa na Allaah na Rasyli Wake, basi aseme ukweli anapozungumza, na atekeleze amana yake anapoaminiwa, na awe jirani mwema kwa jirani yake.” [Al–Albaaniy -‘Mishkaatul Maswaabiyh’]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  amewaelekeza Swahaba zake, na ndio anatuelekeza sisi jinsi ya kumpenda mapenzi ya kweli, mapenzi yenye tija na yenye kuleta mabadiliko katika tabia za mja, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anawaelekeza Swahaba kuwa kumpenda kwa kugombea maji yake ya wudhuu peke yake ili kupata baraka, hakutoshi, na kutakuwa hamna maana kama watu hao watakuwa waongo katika mazungumzo yao, hawatekelezi amana zao, wanaudhi majirani zao, mapenzi hayo ya kutafuta baraka tu na kuacha kumfuata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yatakuwa ni mapenzi ya kumcheza shere Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

3- Kumfanya Hakimu Katika Mizozo Yote

 

Na katika dalili za kumpenda Nabiy ( Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumfanya hakimu katika mizozo yetu yote, na kuridhika na hukmu yake, na katika zama tulizonazo ambazo Nabiy ( Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hayupo nasi, basi Qur-aan na Sunnah zake ndizo zitakazotumika katika kutatua mizozo yetu, na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuambia katika Qur-aan:

 

 فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا﴿٦٥﴾

“Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu.” [An-Nisaa: 65]

 

Katika kutafsiri Aayah hii, Imam Ibnul-Qayyim katika kitabu chake cha Sharhu Al-Manaazil anasema: “Aayah hii imekusanya ngazi tatu za Dini, amabzo ni: Uislaam, Iymaan na Ihsaan  na atakayeikanusha na kuacha kuitekeleza basi atakuwa amekanusha ngazi zote za Dini.”

 

Jambo la kuhuzunisha ni kuwa, Waislaam tulio wengi ambao tunasema tunampenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini haturudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kutatua mizozo yetu, bali kila mtu, kila kundi linarudi kwa sheikh wake, kwa madh-hab yake au kwa kutumia rai zao, na unapotoa ushahidi wa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu suala lenye mzozo basi unaweza kuambiwa mbona Imaam ash-Shaafi’iy, au Maalik kasema hivi, na mtu huyu huyu anapotajwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) humtakia rehma kwa kishindo kudhihirisha mapenzi yake kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na unapochelewa wewe kumtakia rehma Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi hudiriki kukutuhumu kuwa humpendi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Katika Aayah nyingine Allaah Anasema:

 

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا﴿٥٩﴾

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. “[An-Nisaa: 59]

 

Aidha Allaah (‘Azza wa Jalla) Anatuamrisha katika Aayah  nyingine kurejesha mizozo yetu Kwake na kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini asilimia kubwa ya Waislaam hawaitekelezi Aayah hii, na kwa bahati mbaya hata wale wanaojinasibisha kutetea Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenendo wa As-Salaf As-Swaalih baadhi yao wameshindwa kuitekeleza Aayah hii, na wanaona bora kuhukumiwa na mahakama za kitwaaghuut kuliko kukaa na kuyamaliza matatizo yao kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.

 

Hali ya Ummah inahuzunisha, wako wanaotosheka kumsifu tu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuridhika kuwa wameonyesha mapenzi yao kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku wakipinga Sunnah zake zizlizo dhahiri kwa utashi tu wa nafsi zao, na kuwatanguliza masheikh wao, na wakati mwingine kwa ajili tu ya kuwaonyesha Waislamu wenzao ukaidi wao na ubishi wao wa ushindani.

 

Bado hatumtendei haki Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bado hatujafikia daraja ya kumpenda kwa dhati kuliko nafsi zetu, kuliko maslahi yetu, kuliko masheikh zetu, kuliko wafuasi wetu, na kuliko majina ya taasisi na makundi yetu.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anawasifu Waumini wa kweli kwa kusema:

 

 إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾

“Hakika kauli ya Waumini (wa kweli) wanapoitwa kwa Allaah na Rasuli Wake ili Awahakumu baina yao; husema: “Tumesikia na Tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.” [An-Nuwr: 51]

 

 

4-Kutotanguliza Jambo Mbele Yake, Na Kuinamisha Sauti

 

Katika kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kutotanguliza jambo lako, au rai yako, au kauli ya sheikh wako, au madh-hab yako, mbele ya kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutonyanyua sauti yako, na fikra zako mbele ya mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), katika uhai wake na hata baada ya kifo chake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuheshimu mafundisho yake na kuyaweka mbele na juu ya mafundisho yote, na kutonyanyua sauti yako juu ya kauli na hukmu ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Siku moja Imaam Ash-Shaafi’iy (Rahimahu-Allaah) alijiwa na mtu na akamuuliza mas-ala katika mas-ala ya Dini, Imaam akamwambia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kadha, na akamsomea kipengele cha Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yule muulizaji akamuuliza tena Imaam Ash-Shaafi’iy; na wewe Imaam unaonaje? Imaam Ash-Shaafi’iy akakasirishwa sana na yule mtu, na akamwambia: “Je unaniona mimi nipo kanisani hapa? Nakwambia amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kadha unaniuliza rai yangu?” Huku ndio kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukweli wa kumpenda.

 

 

 

5-Kuwapenda Na Kuwaheshimu Watu Wa Familia Yake

 

Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuipenda familia yake, wakiwemo wake zake na kuwapenda Swahaba zake, huwezi kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ukawa unawachukia wakeze na Swahaba zake, bali kwa kuwachukia wake za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na Swahaba zake utakuwa unamchukia Nabiy mwenyewe, na ukiwatukana utakuwa umemetukana Nabiy mwenyewe

 

 

 

6-Kutomsifia Kwa Sifa Asizostahiki

 

Kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwi kwa kumsifia kwa sifa ambazo hastahiki, au ambazo zimepetuka mipaka ya Unabii wake. Wapo Waislaam ambao wanadai kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wanampachikia sifa ambazo zinakaribia kufikia sifa za Allaah (Subhaanahu w Ta’aalaa), na unapohoji juu ya uzushi huo na shirki hizo, basi utatuhumiwa kuwa wewe ni adui wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na humpendi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitabiri hali hii na akautahadharisha Ummah wake usije ukawa kama Manaswara waliomsifu ‘Iysaa bin Maryam mpaka wakamgeuza kuwa ni mwabudiwa. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

 لا تُطْرُونِي كَمَا أَطْرَتْ النَّصَارَى ابْنَ مَرْيَمَ فَإِنَّمَا أَنَا عَبْدُهُ فَقُولُوا عَبْدُ اللَّهِ وَرَسُولُهُ

 “Msinitukuze kama walivyomtukuza Manaswara ‘Iysaa mwana wa Maryam hakika mimi ni mja, niiteni mja wa Allaah na Rasuli Wake.”

 

Lakini pamoja na tahadhari hizo za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bado baadhi ya Waislaam hawaoni kuwa wamempenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka wamsingizie sifa ambazo hana, na baadhi yao wamefikia hata kubadilisha Aayah ya Qur-aan ili ikubaliane na upotofu wao, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliposema kupitia ulimi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuthibitisha kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bin-Aadam kama bin-Aadam wengine isipokuwa yeye huteremshiwa wahyi, alisema:

 

 قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ ﴿١١٠﴾

 “Hakika Mwabudiwa wa haki wenu ni Ilaah Mmoja Pekee. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake.” [Al-Kahf: 110]

 

Wapotoshaji hao waliona wamkosoe Allaah kwa kumshusha cheo Nabiy, wao wakaona waiandike upya Aayah ili isomeke...

 قُلْ إِنَّ ما أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ..  ﴿١١٠﴾

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mtu kama nyinyi,

 

Hii ni kufru ya wazi kabisa ambayo inafanywa kwa jina la kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

 

Na wengine wanadai kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anajua elimu ya ghayb na anajua lini itakuwa Qiyaamah, na kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameumbwa kutokana na nuru ya Allaah, kama isemavyo kauli inayonasibishwa na ‘Abdul-Qaadir Al-Jaylaaniy katika kitabu cha ‘Sirr  Al-Asraar’ anasema: “Elewa Allaah Akuwafikishe kwa Anachokipenda na kuridhia, Allaah Aliumba roho ya Muhammad kwanza kutokana na nuru yake na uzuri wake, kama alivyosema Allaah: Nimeumba roho ya Muhammad kutokana na nuru ya uso wangu…”

 

Na huo ni uongo dhahiri na kumsingizian Allaah ambacho Hajakisema. 

 

Aidha wanadai kuwa siku ya kuzaliwa kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni siku bora kuliko hata usiku wa Laylatul-Qadr, na wanadai kuwa roho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huhudhuria katika maulidi na huwa anazungumza na mawalii.

 

Kwa ujumla, mambo mengi yamezushwa katika Dini hii kwa kumzushia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mambo ambayo mengine tumeshindwa kuyaandika katika safu hii kutokana na kutunza heshima ya kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Ndugu zetu Waislaam, tumpende Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukweli wa kumpenda, tumuingize katika maisha yetu, awe ni kiongozi wetu, ruwaza yetu, mshauri wetu, hakimu wetu, mwalimu wetu, tuyafundishe mafundisho yake kwa walimwengu wote, na tuuthibitishie ulimwengu kuwa, Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Rasuli wa Allaah  aliyetumwa kwa watu wote na ni rehma kwa walimwengu wote. 

 

Tunayo dhimma kubwa ya kuhakikisha kuwa mafunzo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanafahamika vyema kwa Waislaam na wasiokuwa Waislamu, na njia nyepesi ya kufanikisha hilo ni sisi wafuasi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumpenda Nabiy wetu ukweli wa kumpenda, na kuyaingiza mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku.

 

 

 

Share