Skip navigation.
Home kabah

Zidisha Uzito Mizani Yako Siku Ya Qiyaamah

 

((فَأَمَّا مَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ))    ((فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ))  

 

((Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito))

((Huyo atakuwa katika maisha ya kupendeza))

[Al-Qaari'ah:6-7]

 

Allaah سبحانه وتعالى Anatujulisha kwamba yule mwenye kuwa na mizani nzito ndiye atakayekuwa na maisha ya kumridisha siku ya Qiyaama ambayo ni Pepo.   

Kuifanya mizani kuwa nzito ni kwa kufanya mambo mema yote tuliyoamrishwa na Allaah سبحانه وتعالى na Mtume wake Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم na kujiepusha na mabaya yote tuliyokatazwa.  

Mambo mema kama kutekeleza fardhi zote, yaani, Swalah, Zakah, Swawm, Hajj. Vile vile kufanya 'Umrah, kutoa Swadaqah, kuwafanyia wema wazazi wawili, kuunga undugu, kuwafanyia wema jirani, kumsaidia anayehitaji, kulea yatima, kuwa na moyo msafi usio na husda, wala chuki,  kuwa na  tabia njema, na mengi mengineyo yote yaliyo mema. 

 

Jambo muhimu baada ya hapo ni ni kuhifadhi hizo amali ili zisipotee bure akaja mtu siku ya Qiyaamah akaona kwamba hana lolote jema alilolifanya. Na kuhifadhi huko ni kwa kuhakiksha Muislamu amehifadhi haki za Muislamu mwenzake. Yaani kutokumdhulumu mtu hakki yake, kutokumsema nyuma yake na kumsengenya, kutokumtukana mtu au kumuonea kwa njia yoyote  kwani atakyefanya hivyo atakuta siku ya Qiyaamah mambo mema yote aliyotenda yamejazwa katika mizani ya yule aliyemdhulumu na yeye mizani yake ya mambo mema imekuwa aidha nyepesi au haina lolote. 

 

Vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ametufundisha vipi kuzijaza mizani zetu kuwa nzito kama ilivyokuja katika Hadiyth ifuatayo:

 

  قال النبي صلّى الله عليه وسلّم :  ))كلمتان خفيفتان على اللسان ثقيلتان في الميزان حبيبتان إلى الرحمن : سبحان الله وبحمده ، سبحان الله العظيم  ((رواه البخاري ومسلم

Amesema Mtume صلى الله عليه وسلم ((Maneno mawili ni mepesi mno juu ya ulimi, mazito mno katika mizani, yanapendeza mno mbele ya Ar-Rahmani (Mwenye kurehemu) nayo ni:

سُبْحانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ  سُبْحَانَ اللهِ العَظِيمِ

Subhaana-Llahi Wa-Bihamdihi Subhaana-Llahi-l-'Adhwiym)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

“Ametakasika Mwenyezi Mungu  na sifa njema zote ni zake, Ametakasika Mwenyezi Mungu Aliye Mtukufu”

Basi ndugu Waislamu, tujishughulishe ndimi zetu kwa kumtaja Allaah kwa maneno hayo mara nyingi iwezekanavyo, ikiwa kila baada ya Swalah, au wakati wa mapumziko, au hata wakati mtu yuko katika shughuli zake nyumbani au kwenye biashara.

Tujitahidi  tuzidishe uzito wa mizani zetu ili tuje kupata maisha ya kuturidhisha siku ya Hesabu (Qiyaamah) ambayo ni kupata Pepo kwa Rahma Yake Allaah سبحانه وتعالى . Aamiyn.

 

 

************