Mashairi: Nisikupende Kwa Nini?

 

Nisikupende Kwa Nini?

 

Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)

 

 

Ukiyaonja mapenzi

utaujuwa utamu

Ndipo utapoyaenzi

ukayaona adhimu

Nakupenda Mwenye enzi

Ilahi Mola Karimu

Nisikupende kwa nini

Nawe Umenikirimu

 

 

Nisikupende kwa nini

Ya Ilahi ya Karimu

Nawe umenithamini

kuniumba mwanadamu

Ukaniongeza shani

Kwa dini ya Isilamu

Nisikupende kwa nini

Nawe Umenikirimu

 

 

Meniumba insani

Mwanadamu alo huru

Ukanipa Qur ani

Ili iwe yangu nuru

Sasa nina kheri gani

Kama sijakushukuru

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Rasuli ukamtuma

Ili aje nifundisha

Kila jambo lilo jema

Yote kanifahamisha

Akafanya kila hima

Risala kukamilisha

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Akujuwaye yakini

Hawezi kuwa mjinga

Akamfwata shetani

Na Wewe akakutenga

Kwani vyote ardhini

Asili yake mchanga

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Umetuletea maji

Twanywa tukiona raha

Hujayafanya ujaji

Machungu yenye karaha

Ya Rabi ewe Mpaji

Tuzidishie furaha

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Mbingu ukaziumba

Kwa nyota ukazipamba

Na kisha ukaziremba

Zikapangika sambamba

Kama zimefungwa kamba

Hapana kinachoyumba

Nisikupende kwa nini

Nawe Umenikirimu

 

 

Wallahi tukiperemba

Kutizama utukufu

Tunaelewa ya kwamba

Ni kazi yako Latifu

Ni kazi yako Muumba

Ilo timu kamilifu

Nisikupende kwa nini

Nawe Umenikirimu

 

 

Neema zako ni nyingi

Ya Rabbi l arbabu

Umetupa mambo mengi

Hayana hata hesabu

Ewe Mpaji kwa wingi

Ewe wangu Mahabubu

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Hewa hii tuvutayo

Moja ya Zako neema

Neema ambayo kwayo

Kukupenda ni lazima

Lau kama hatunayo

Uhai ungeyoyoma

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Vyote ulitayarisha

Hata bado kutuumba

Mahitaji ya maisha

Bila hata kukuomba

Ukarimu usokwisha

Kutoka kwako Muumba

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

 

Ninakupenda Wallahi

Na Wewe Ndiye Shahidi

Pendo kwako likisihi

Ndipo nitapofaidi

Ninakupenda Ilahi

Na Mtume Muhamadi

Kwa nini nisikupende

Nawe Umenikirimu

 

Share