Je Inafaa Mwanamke Kuvaa ‘Abayah Zenye Vito Na Marembo Japokuwa Amejifunika Vizuri?

 

SWALI:

 

Asalamy aleikum kwanza nawashkuru kwa ku2elimisha allaah subhana wa taala) atawalipa mimi nilikuwa naomba munifafanulie kuhusu vazi analotakiwa kuvaa mwanamke wakiislam je haya mabaibui 2nayoyavaa yanafaa je kati ya jilbab na haya mabaibui ambayo yana vito vinavyowaka pamoja mitandio mifupi naomba u2eleweshe mana vaz la baibui sasa limekuwa kama ni fashen nategemea majibu mazuri yatakayo2fundisha inshaalla

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uvaaji wa vazi la mwanamke.

Vazi la mwanamke Muislamu kuwa ni la sawa ni lazima litimize masharti kadhaa. Ikiwa vazi hilo litatimiza basi litakuwa la Kiislamu la, sivyo basi itakuwa mwanamke huyo amevaa nguo lakini si ya Kiislamu. Kabla ya kuingilia masharti, hebu tutazame Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anavyosema:

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (al-Ahzaab 33: 59).

Tufahamu kuwa vazi hilo ni amri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka, hivyo hatuwezi kuvaa tunavyotaka.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)  Anasema tena:

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au …” (an-Nuur 24: 31).

 

Ama kuhusu masharti kwa vazi la kike kuitwa la Kiislamu ni kama yafuatayo:

 

1.     Vazi la mwanamke wa Kiislamu ni lazima lisitiri mwili mzima: Wanachuoni wametofautiana kuhusu viganja vya mkono na uso kwa kauli mbili – wapo wanaosema ni lazima vifunikwe na wanaokubali kuwa vinafaa viachwe. Wengine wameunganisha kauli hizo kwa kusema hadi ya chini ni kuacha vitanga vya mkono na uso kuwa lakini vikifunikwa ni bora zaidi. Kuhusu kusitiri tayari tumenukuu aayah mbili – Suratun Nuur Aayah ya 31 na Suratul Ahzaab Aayah ya 59.

 

2.     Vazi lenyewe lisiwe ni pambo: Hii ni kwa kauli ya Aliyetukuka: “Wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika” (an-Nuur 24: 31). Na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina tatu hata usiwaulize: … Na mwanamke ambaye mumewe hayupo lakini amemtosheleza na mahitaji yake yote ya kidunia, naye akafanya Tabarruj” (Ahmad na al-Haakim). Tabarruj ina maana mwanamke kuonyesha pambo lakena uzuri wake ambao unatakiwa usitiriwe, ambavyo vinamfanya mwanamme awe na matamanio. Na kusudio ya amri ya kuvaa Jilbaab ni kusitiri pambo la mwanamke, hivyo haingii akilini iwe Jilbaab lenyewe liwe ni pambo.

 

3.     Vazi liwe zito, kisionekane kilicho ndani yake: Hii ni kwa kauli yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Watu aina mbili wa Ummah ni wa Motoni nami sijawaona… na wanawake waliovaa nguo lakini wapo uchi. Hao hawatoingia Peponi wala hawatopata harufu yake japokuwa harufu yake inafika masafa kadhaa na kadhaa” (Muslim). Lengo ni kwa wale wanawake wanaovaa nguo hafifu ambayo inatoa sifa kamili na wala haisitiri. Hao kwa jina wamevaa lakini kwa uhakika wako uchi.

 

4.     Vazi liwe pana, sio la kubana: Kwani vazi likimbana mwanamke itamtoa umbile lakelote hivyo kumfanya kama kwamba hajajisitiri. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhuma): “Muamuru mkeo ajaalie Ghulaalah (shuka inayovaliwa chini ya nguo), kwani nakhofia isije ikasifu ukubwa wa mifupa yake” (Ahmad na Abu Daawuud).

 

5.     Vazi lisitiwe manukato: Hii ni kutokana na kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke yeyote anayejitia manukato, akawapita mbele ya watu ili wapate harufu yake, basi yeye ni mzinifu” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).

 

6.     Vazi lisifanane na vazi la Kiume: Huku ni kwa kule kulaaniwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanaume wanaoshabihiana na wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanaume (al-Bukhaariy, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah). Na pia amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelaaniwa mwanamme mwenye kuvaa nguo za kike, na mwanamke mwenye kuvaa nguo za kiume (Ahmad na Abu Daawuud).

 

7.     Vazi lisifanane na vazi la kikafiri: Shari’ah imekariri kutojuzu kwa Waislamu wanaume kwa wanawake kujifananisha na makafiri sawa katika ‘Ibaadah, au sherehe, au katika mavazi yao na kadhalika. Ama kuhusiana na kivazi, ni ile Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: Alimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa amevaa nguo mbili za njano, akamwambia: “Hakika hizi nguo ni za makafiri kwa hivyo usivae” (Ahmad, Muslim na an-Nasaa’iy).

 

8.     Vazi lisiwe ni la kujionyesha: Hii ni kwa kauli yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwenye kuvaa nguo ya umaarufu na kujionyesha hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya udhalili Siku ya Qiyaamah, kisha Atamuingiza Motoni” (Abu Daawuud na Ibn Maajah).

 

Haya ndio masharti ambayo yanafaa yawepo katika vazi la mwanamke ili lijulikane kuwa ni la Kiislamu. Ikikosekana sharti hata moja basi litakuwa basi lenyewe ni la Kiislamu. Kwa ajili hiyo, ma ‘Abaaya mengi hayatimizi masharti haya wala yale mabaibui ya fesheni. Nasaha kwa dada zetu waepukane na hayo.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Mwanamke Anavaa Hijaab Lakini Anavaa Suruwali Ya Kubana Anaposwali, Inakubaliwa Swalah Yake?

 

Kuvaa Niqaab Ni Fardhi? Nini Hukmu Ya Mwanamke Kuvaa Suruwali?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share