Kunywa Maji Wima Imethibiti Katika Sunnah?

SWALI:

 

Assalm alykum Waramatullah Wabarakatuh. Swali langu nikwamba nilimskia shekh maaruf anaitwa .......ambae pia inasemekana ni mwanafunzi wa Shekh Albaniy Rahimahu llaah ametoa hadith kwamba amesema mtume swalla llahu alyhi wasallam alimwona swahaba mmoja sikumbuki jina lake akinywa maji wima akamwambia upo tayari kunywa pamoja na paka swahaba akasema hapana, mtume swalla llahu alayhi wasallam akamwambia basi unaekunywa nae hapo ni mbaya kuliko paka na huyo ni shaytwaan. Pia akasema anaekunywa wima basi ajitapishe kile alichokunywa. Na pia nilishawahi kusikia kua mtume swalla llaahu alayhi wasallam alionekana akinywa wima. Je tufuata ipi. Jazaakum llah khayr

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kunywa maji wima (ukiwa umesimama).

Hakika zipo Hadiyth zinazokataza kunywa maji kwa kusimama na zipo nyingine zinazoruhusu.

 

Hadiyth zenyewe ni kama zifuatazo:

 

1.     Imepokewa kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kunywa kwa kusimama. Amesema Qataadah: Tukamuuliza Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Je, kula?” Akasema: “Hiyo ni mbaya zaidi au ni chafu zaidi” (Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Na katika riwaya yake nyengine: “Hakika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekemea kunywa kwa kusimama”.

 

2.     Na imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asinywe mmoja wenu kwa kusimama, na anayesahau basi ajitapishe” (Muslim).

 

3.     Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Nilimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maji ya Zamzam akanywa huku amesimama (Al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaaiy).

 

4.     An-Nazzaal bin Sabrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Alikuja ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenye mlango wa Rahbah (sehemu pana iliyopo Kufah) na akanywa akiwa amesimama, na akasema: “Hakika mimi nimemuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya kama munavyoniona nikifanya” (Al-Bukhaariy, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

 

5.     Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: Tulikuwa tukila katika zama za Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nasi twatembea na tukinywa nasi tumesimama (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh. Pia imenukuliwa na Ahmad, Ibn Maajah na ad-Daarimiy. Isnadi yake ni Hasan).

6.     Na imepokewa kwa ‘Amru bin Shu‘ayb kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambaye amesema: “Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinywa kwa kusimama na kwa kukaa” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh. Na imenukuliwa na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Hasan. Pia ipo kwa Ahmad kwa njia nyengine kutoka kwa Ibn ‘Umar. Hivyo Hadiyth ni Sahihi).

 

Kulingana na Hadiyth tulizozitaja hapo juu ni wazi kabisa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekataza baadaye akaruhusu watu kufanya hivyo kwa matendo yake ya kunywa akiwa amesimama. Imaam an-Nawawiy amejaribu kuoanisha baina ya Hadiyth hizi katika kitabu chake “Riyaadhw asw-Swaalihiyn” kwa kuweka mlango alioupatia jina “Kubainisha kujuzu kunywa kwa kusimama lakini ubora ni kunywa kwa kuketi”

Na hiyo ndio rai ya Maulamaa wengi kuwa kunywa kwa kukaa ni bora zaidi kuliko kunywa kwa kusimama, ingawa hakuna uharamu wa kunywa kwa kusimama. Na ndiyo huenda Shaykh uliyemtaja amelisisitiza hilo la kunywa kwa kusimama kwa kumweka mtu katika usalama na ubora zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share