Kwenda Haja Ndogo Wima Imethibiti Katika Sunnah?

 

SWALI:

 

Assalam Alykum Warahmatullah Wabarakatuh. Swali langu ni kwamba Niliskia kuna Hadith ya Aisha radhiya llahu anha kwamba amesema sijapato kumwona mtume swalla llaahu alyhi wasallam akikojoa wima, na niliwahi kusikia kuwa imethibiti katika hadith kuwa mtume swalla llaahu alyhi wa sallam alionekana akikojoa wima. Naomba kujua nifuate ipi. Jazaakum llaahu Khayrah

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kwenda haja ndogo wima kishari’ah.

Hakika katika mas-ala haya zipo Hadiyth tano kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) – tatu sahihi na mbili dhaifu. Moja ni kukataa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama, ya pili ni kuonyesha kuwa alikojoa kwa kusimama na ya tatu akiwa ameketi. Na katika hizo Hadiyth dhaifu ni kukataza kwake kukojoa kwa kusimama na ya pili ni kukemea kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kukojoa kwa kusimama ni katika kukengeuka. Hapa twazitaja zote kwa faida ya kila mmoja wetu:

 

1.     Hadiyth ya ‘Aa’ishah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: Yeyote anayekuhadithieni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikojoa kwa kusimama msimsadiki. Alikuwa hakojoi ila kwa kuketi (Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

2.     Hadiyth ya Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda kwenye jaa la taka la watu, akakojoa kwa kusimama. Mimi nikaondoka, akasema: “Njoo”. Nikarudi mpaka nikasimama kwenye mabega yake, akatawadha na kupangusa juu ya viatu vyake (Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

3.     Hadiyth ya ‘Abdur-Rahman bin Hasnah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Alitoka kwetu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa mkononi mwake ana ngao ya ngozi, akaiweka, kisha akaketi nyuma yake akakojoa kuielekea… (Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah).

 

Na hizi ni Hadiyth mbili zilizo dhaifu:

 

4.     Imepokewa na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa kusimama. Akaniambia: Ewe ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama. Akasema: Sikukojoa tena kwa kusimama baada ya hapo (Ibn Maajah, al-Bayhaqiy na al-Haakim lakini ni Hadiyth iliyo dhaifu).

5.     Imepokewa na Buraydah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Vitu vitatu ni katika kukengeuka: Mtu kukojoa kwa kusimama, kupangusa mgongo wake kabla ya kuondoka katika Swalah na kupuliza katika sijdah yake (Ameinukuu al-Bukhaariy katika Taariykh yake, al-Bazzaar, na akaikanusha al-Bukhaariy na at-Tirmidhiy. Na hii imethubutu kuwa ni kauli ya Ibn Mas‘ud [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

 

Kwa ajili ya Hadiyth hizi, wanachuoni wametofautiana kuhusu kukojoa wima. Kwa ajili hiyo zikapatikana kauli tatu”

 

1.     Inachukiza pasi na udhuru wowote: Hii ni kauli ya ‘Aaishah, Ibn Mas‘ud, ‘Umar (katika riwaya yake moja) [Radhiya Allaahu ‘anhum], Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhum), ash-Sha‘biy, Ibn ‘Uyaynah, Abu Haniyfah na ash-Shaafi‘iy.

2.     Inajuzu daima dawamu: Hii ni kauli ya ‘Umar (katika riwaya yake ya pili), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar, Sahl bin Sa‘d, Anas, Abu Hurayrah, Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhum) na ni kauli ya Ahmad bin Hanbal.

3.     Ikiwa ni katika sehemu ambayo hairudishi (hauruki) mkojo kwake inajuzu na ikiwa unarudi basi haifai: Hii ni kauli ya Maalik, na Ibn al-Mundhir akaiona ni sahihi.

 

Baada ya hayo yaliyo juu, twafupisha maneno kwa kusema kuwa hakuna uharamu wowote wa kukojoa kwa kusimama ikiwa mkojo hautarudi au kumrukia mwenye kukojoa ila ni bora kukojoa kwa kuketi. Imaam an-Nawawiy akizungumzia mas-ala haya amesema: “Kukojoa kwa kuketi inapendeza zaidi kwa rai yangu, lakini kufanya hivyo kwa kusimama wima kunaruhusiwa. Matendo yote mawili yamepatikana kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share