Adhana Ya Alfajri Huwa Ngapi? Na Ni Ipi Huongezwa ‘Asswalaatu Khayrum-minan-nawm?

SWALI:

Assalaam aleikum warahmatulahi taala wa barakatuhu.

Shukran kwa kazi nzuri. Nauliza juu ya adhana ya Alfajri. Adhana ya Afajir huwa ni ngapi? Ni adhana ipi ya kuweka Assalaatul khairu minna naum? Nijibu tafadhali.


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Adhana zinazotolewa kwa Swalaah ya Alfajiri.

Adhana hizo kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mbili. Ya kwanza ilikuwa inatolewa kabla ya kuingia Alfajiri kwa muda ili watu wapate kujitayarisha kwa ajili ya Swalaah hiyo. Ya pili ni ile iliyokuwa ikitolewa kuwajulisha watu kuwa wakati wa Swalah umeshaingia au kuwapasha habari wenye kutaka kufunga kuwa wakati umekwisha na hawawezi kula wala kunywa tena.

 

Adhana ya kwanza ndio ya kuwatayarisha na kuwaamsha watu ili wawe tayari kwa ajili ya Swalah. Hivyo, kulingana na Hadiyth kadhaa imekuja kuwa maneno ya nyongeza yanayosemwa, “Asw-Swalaatu Khayrum-minan-nawm" (Swalaah ni bora kuliko usingizi) ni katika Adhana ya kwanza lakini kutokana na ufafanuzi wa Wanachuoni katika ufahamu sahihi wa Hadiyth hizo, ni kuwa, wao wanafafanua hizo Hadiyth kuwa makusudio ya Adhana ya kwanza ni ile ambayo Swalah imefika wakati wake na baada ya hapo inafuatiwa na Adhana ya pili ambayo ni Iqaamah kama inavyojulikana kwenye Hadiyth nyinginezo kuwa Mtume  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposema "Katika kila baina ya Adhana mbili  kuna Swalah" akikusudia Adhana na Iqaamah. Hivyo hapo Wanachuoni wanaeleza makusudio ya Adhana ya kwanza ni hiyo ambayo hujulikana kama ni Adhana ya pili ambayo hufuatiwa na Iqaamah.

Na hivyo ndivyo walivyoeleza Wanachuoni wa Fataawa al-Lajnah ad-Daa’imah lil-Buhooth al-‘Ilmiyyah wal-Iftaa, 6/63

 

Kwa hivyo, kauli yenye nguvu kwenye suala hili, ni kuwa Maneno hayo " As-Swalaatu khayrum-minan nawm ni kwenye hii inayojulikana na watu kuwa ni Adhaana ya pili.

 

 

 

 

Na Allaah najua zaidi

 

 

Share