Mume Mcheza Kamari, Mlevi Nini Hukmu Ya Ndoa Yake?

SWALI:

 

asssalm alaykum. swali langu ni kuhusu mume wangu mchezaji kamari mkubwa mpaka mwezi wa ramadhani. na nimeshawahi kumuapisha kwa kumshikisha msahafu akasema amewacha lakini kila nikimchunguza naona kama amerudia. na jee mtu kwa ndoa ya kiislam ahuku yake ni ipi? na tena mlevi na hana nguvu za kumuingilia mkewe


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mumeo ambaye ni ‘’aswi, mwenye kufanya maovu yaliyo makubwa tena. Hakika hili ni tatizo ambalo mara nyingi hutokea kwa mume kutochunguza mke anayekwenda kumuoa na mke naye pia kutofanya hivyo kwa mume aliyekuja kuposa.

 

Ikiwa hali ni hiyo ni wajibu na jukumu la mke kutafuta kila aina ya njia ya kuweza kumrekebisha mumewe kama alivyofanya kuhusiana na kamari lakini ikashindikana. Kufanya hivyo kumeuswia kiujumla na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Kuongoka mtu mmoja kwa tawfiki ya Allaah ni bora kwako kuliko ngamia mwekundu” (al-Bukhaariy). Katika njia unazoweza kutumia ni kuzungumza naye, kutumia watu kuzungumza naye, kumpatia vitabu na CD za mawaidha.

 

Ikiwa yote hayo yameshindiakana utakuwa huna budi ili kuiwasilisha kesi hiyo yako katika kikao ambamo utakuwepo wewe, mumeo, mwakilishi wako na wake ili kujadili tatizo hilo kubwa mlilo nalo. Wawakilishi hao ambao ni wazazi wenu na jamaa zenu wa karibu wenye busara na kutaka kutazama haki. Ikiwa wawakilishi hao watakuwa na ikhlaasw basi bila shaka ufumbuzi kwa tatizo hilo utapatikana.

 

Ikiwa hilo halikufanikiwa basi itabidi upeleke malalamiko yako kwa shaykh mwadilifu au kwa Qaadhi ikiwa yupo. Mahakimu hawa watasikiliza pande zote mbili bila ya upendeleo wowote na kuja na uamuzi. Kwa ajili ya maksoa aliyonayo mumeo atapatiwa muda wa kujirekebisha, ikiwa atajirekebisha itakuwa kheri na lau sivyo itabidi ndoa hiyo ivunjwe.

 

Ikishindikana katika njia zote hizo kutakuwa hakuna tena sababu ya wewe kuishi na mwanamme huyo na Qaadhi atakuwa ni mwenye uwezo wa kuivunja ndoa yenu na hilo ndilo litakalokuwa kheri kwako hapa duniani na Kesho Akhera.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

 

Mume Mlevi, Anazini Mpaka Na Mayaya, Ananitukana Matusi Makubwa, Hakuna Mapenzi, Haswali: Na Anawazuia Watoto Wasiswali

 

Mume Mlevi, Mtusi, Anaiba Vitu Vyangu Na Ananipiga Nimeamua Kumfukuza. Je, Nimekosea?

 

Mume Mzinifu, Haswali, Hapendi Kusikiliza Mawaidha, Mshirikina – Nifanyeje Kuhifadhi Dini Yangu?

 

Analewa Sana Ila Mwezi Wa Ramadhaan Anaacha Kisha Anarudia Tena Nini Hukmu Yake?

 

Mume Mzinifu, Haswali, Nilipokasirika Naye Kanitenga Nifanyeje?

 

 

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Alete masikilizano na Amjaalie mumeo ni mwenye kubadilika na kuwa Muislamu mzuri kabisa. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share