Mume Amekasirika Na Amenitelekeza Miezi Sita Bila Talaka Kwa Sababu Nimemkataza Asifanye Ushirikina. Na Haswali

SWALI:

 

Asalaam alaikum warahmaa tullaah wabarakatuh! Ama baada ya salaam Allaah awape kheir nyingi duniani na akhera. Mie swali langu nina mume alokuwa haswali kabisa, ktk maisha yetu ya ndoa tumepata mitihani mingi lakini kutokana imani na dini                                                        yangu ya kiislam naamini mitihani hii anayoipata ni kutokana na dhulma nyingi anayoifanyia familia yake ambayo ni mie (mkewe na mwanae) basi akaanza kutumia dawa za waganga kwa siri eti mambo yamwendee vizuri nikamwambia huo ni ushirikina awache amuabudu Allaah.

 

Asalaam alaikum warahmtullaah wabarakatuh! Ndugu zangu swali langu mie mume wangu ambae haswali kabisa na anatumia dawa za waganga kwasiri za kujifukiza na kuogea nikagundua nikamwambia huo ni ushirikina na dhambi namwambia aswali: amuabudu Allaah! Anasema namtukana je niseme vipi huo kama si ushirikina?

Naomba mnijibu swali langu please! Kwani huyu mume kishahama bila kutoa talaka (kanitelekeza) miezi sita sasa. hii ya kumwambia ukweli ni sababu mojawapo ilomfanya aondoke.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mumeo ambaye ni mshirikina na haswali.

 

Hakika hili ni tatizo sugu katika jamii yetu popote ilipo. Ni masikitiko makubwa kuwa wenye kuathirika na kutatizwa wengi ni dada zetu katika Imani na Uislamu. Na hiyo yote ni kushindwa kufuata maagizo ya kisheria ya Dini yetu tukufu. Hayo ya kumshirikisha Allaah Aliyetukuka na kutoswali ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa Muislamu kuwa nayo.

 

Na Muislamu mwanamke hafai kuolewa na mwanamme mwenye sifa hizo mbili na kinyume chake pia ni sawa. Kwa kuwa ametoka mwenyewe ni kheri kwako wala usihuzunike kwa hilo, na Allaah Aliyetukuka Atakupatia badali ya kheri kuliko huyo. Hata hivyo, mume huyo ametoka bila ya kutoa talaka hivyo wewe ni mkewe. Sasa inatakiwa ufanye yafuatayo:

 

1.      Ikiwa una namba yake mpigie simu umuulize kule kutoka kwake amekusudia nini. Je, amekusudia ni talaka au la?

 

2.      Uwasiliane na wazazi wako na wazazi wake ili kuja kuwasuluhisha nyinyi na huenda kukawa na kheri. Kufanya hivyo naye kuja katika kikao huenda akarudi katika njia ya sawa na kuacha madhambi yake na hapo utakuwa na thawabu nyingi kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

3.      Ikiwa hukufanikiwa kwa njia hii ya pili itabidi uende kwa Qaadhi au Imaam mwaminifu mcha Mungu wa eneo hilo, na kumshitakia kuhusu hayo. Na Qaadhi ana uwezo wa kuwaachanisha ikiwa mumeo hatokubali kuacha madhambi aliyo nayo.

 

Tunakutakia kila la kheri katika kupata ufumbuzi wa hilo tatizo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share