Ameniapia Kuwa Hakuoa Mke Mwingine Nami Nimesikia Kuwa Kaoa Kisiri Sasa Inafika Miaka Miwili - Nishike Yepi?

 

SWALI:

 

kuolewa siri na kufichwa mke aliekuwepo ndani ya ndoa mpaka yule mke apate habari na watu wengine ni sheria? kwani mume wangu ameoa na mimi hajaniambia lakini nimepata habari sio za kubuni bali ni za uhakika. Lakini mpaka hii leo hajanambia na sasa inakaribia miaka 2 na huyo mwenzangu tunaishi vizuri bila matatizo. kwa kuwa mwenzangu tunaishi vizuri hajaniambia cha kushangaza mimi nilimuuliza kwa kuwa tayari tupo pamoja miaka 50 nilipomuuliza amenambia hajaowa ila alitaka kuowa kwa shinikizo la ndugu zake na amaapa kwa Mnyezi MUNGU kuwa hajaowa je sasa mimi nishike yepi kwani nakosa raha na ndoa yangu.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu ndoa ya siri na uke wenza.

Hakika ni kuwa katika Uislamu hakuna ndoa ya siri kwa maana ya mume na mke mtarajiwa wakubaliane kisha imalizike hivyo. Bali ndoa kama ‘Ibaadah nyengine ina masharti yake. Miongoni mwa masharti ni:

 

1.     Kuwepo kwa walii wa msichana.

2.     Kuwepo mashahidi wawili waadilifu.

3.     Kukubali kwa mume na kumpatia mahari mke.

4.     Kukubali kwa mke mwenye kuolewa.

 

Kwa jinsi hiyo hakutakuwa na siri yoyote. Ila hii ndoa ya siri inavyoeleweka Afrika Mashariki na haswa Tanzania na Kenya upande wa Pwani ni kuwa mume anakwenda kuoa bila kualika wala kumuambia mkewe ingawa anatimiza masharti yote. Ndoa kama hiyo haina tatizo bali ni vyema kwa ndoa kutangazwa na kualikwa watu kama alivyotushauri Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na mume kuoa mke wa pili si lazima amtake shauri, au amwambie mke wake wa mwanzo, yeye anaweza kuoa bila ya kufanya hayo lakini ni katika wema na ihsani kumwambia mkewe haswa ikiwa wameishi kwa muda mrefu kama mlivyo nyinyi.

 

Jambo la wewe kuamini ni kuwa ikiwa mume amekuambia kuwa hajaoa muamini yeye wala usipeleleze peleleze kwani kufanya hivyo kutakuingiza wewe katika haraam. Allaah Aliyetukuka Anasema:

Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi” (al-Hujuraat [49]: 12).

 

Hivyo jiepushe na kusikia maneno ya nje kwani mara nyingi maneno ya nje huharibu ndoa nyingi. Na kama unahisi kama hayo uliyoyasikia ni kweli, basi ungehifadhi moyoni mwako na kama ni kweli yatadhihirika na yatakapodhihirika basi hapo unaweza kuuliza kwa njia nzuri maana kama tulivyoeleza nyuma, kuwa mume hashurutishwi wala kulazimishwa na shari’ah kuomba rukhsa yako au kukutaka ushauri anapotaka kuongeza mke. Lakini kwa kujenga mapenzi, heshima na mahusiano mazuri baina ya wanandoa, ni bora na uzuri mume kumjulisha mke wake kama anataka kuoa mwanamke mwengine.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share