Hilaal: Kuonekana Kwa Mwezi Sehemu Tofauti Na Kuanza Swawm

 

 

Hilaal: Kuonekana Kwa Mwezi Sehemu Tofauti Na Kuanza Swawm

 

 Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalamu alakum, asanteni sana kwa mawaidha yenu yanayotujia mara kwa mara. Nimeona tangazo la mwezi katika alhidaaya kua mwezi haukuonekana. Tafadhali nataka kuuliza na nitafurahi pindi nikijibiwa wakati mtapoipata email hii Inshalla. Mimi naishi Ireland, jana misikiti ya hapa imetangaza Ramadhani inaanza leo, sijui wanafuata mwezi wa wapi isipokua nimekutana na mtu amenambia mwezi umeonekana Libya na Uturuki. Jee niendelee kufunga kama wanavyofunga watu wa hapa au nikamilishe 30 ya Shaaban. Sikua na simu zenu kutaka kuwauliza ili nipate jibu la haraka. Shukran wa jazakumullah khair

 

Nduguyo katka Uislamu

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Katika suala hili zipo rai mbili – moja ni kufunga unapoanza kuonekana popote ulimwenguni na ya pili mpaka uonekane nchi unayoishi.

Hata hivyo, rai yenye nguvu kwetu ni unapoonekana popote ulimwenguni.

 

Tukija katika suala lako la kufuata wapi? Hujui ufuate tangazo la Alhidaaya au mwandamo wa Uturuki na Libya?

 

Tunavyojua ni kuwa Libya na Uturuki ni nchi ambazo zinasemwa kuwa zinatumia mahesabu ya falaki katika kutangaza mwezi na si kuuona mwezi! kwa hivyo, nchi hizo mbili haziwezi kutegemewa na Muislamu kwa kufunga Ramadhwaan au kufungua kwa sikukuu ya 'Iyd.

 

Shariy'ah imetutaka tufunge kwa kuonekana mwezi na kufungua kwa kuonekana mwezi na si kwa mahesabu ya falaki! 

 

Suala la hesabu ya falaki kwa kufuata mwezi ni suala ambalo linapingana na mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani yeye katuamrisha kufunga kwa kuonekana mwezi na kufungua kwa kuonekana mwezi. Hivyo kufuata nchi inayotegemea hesabu ya falaki (astronomical calculations) itakuwa haifai kwa Muislamu kufuata kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Sunnah.

 

Ikiwa kuna taarifa sahihi za kuaminika kuwa mwezi umeonekana sehemu fulani duniani, basi itakuwa ni wajibu kwako na Waislamu wengine kuanza kufunga.

 

Kwa kweli katika ufuatiliaji ni kuwa Uturuki wala Libya hawakuona mwezi bali walianza kwa kufuata mahesabu waliyofanya. Ndio kwa ajili hiyo alhidaaya wakaweka tangazo la kuanza kufunga siku ya pili yake kwa sababu hakuna taarifa zozote za kuonekana mwezi zilizopatikana popote duniani.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share