Tendo la Ndoa kwa Utumiaji wa Sauti

SWALI:

 

Naomba kuuliza suala hili.

 

Tunajua kwamba, Kufanya tendo la ndoa ni haramu kwa mwanaadamu yoyote isipokuwa katika ndoa, na ndoa iliyokusudiwa ni ndoa ya Kiislam.

Katika kufanya tendo la ndoa katika ndoa ya Kiislamu, Mja hupata thawabu na hivyo ni kusema kwamba, tendo la ndoa ni Ibada.  Suala langu ni hili, Je ni halali kufanya tendo la ndoa kwa ishara ya sauti kwa wanandoa wa Kiislamu ambao hawapo pamoja. Yaani, kwa mfano, Mke yuko Kenya na Mume yuko Uganda ama wapo nchi moja lakini sehemu tofauti ama wapo sehemu moja, nyumba moja na chumba kimoja, Jee, inafaa kuigiza na kuashiria tendo hilo kwa njia ya simu huku wakiigiza milio mbali mbali ya tendo hilo (Sex sounds).  kwa kufanya hivi, wanandoa waha hujisikia kama wapo pamoja na hupelekea mara nyengine, mwanamme kutokwa na shahawa na mwanamke vile vile.

Je nini hukumu yake katika Uislamu?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu   kwa swali lako kuhusu tendo la ndoa kupitia kwa njia ya sauti.

Msingi wa Uislamu ni kuwa mume kumfurahisha mke kwa njia ambayo inaruhusiwa ni ‘Ibaadah na kinyume chake pia. Ikiwa katika kutoa sauti hiyo kweli mume na mke watakuwa wanahisi kuondoa shahwa basi hakuna makatazo tuliyoyapata katika kishari’ah.

 

Hata hivyo, watafanya jambo hilo kwa muda gani? Wanandoa wanatakiwa kwa kiwango kikubwa wawe ni wenye kuishi pamoja ndio kupatikane maingiliano ya sawa sawa. Ndio kwa ajili hiyo ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuwa ni mwenye kumuacha mwanamme katika Jihaad akae huko kwa muda mrefu wa zaidi ya miezi 4 bila ya kurudi na kukutana na mkewe.

 

Kisha utafiti uliofanywa ni kuwa utoaji wa manii kwa njia ya mkono, sabuni na njia nyengine yoyote isiyokuwa ya kujamiiana na mkeo au kuota inadhoofisha maume ya mwanamme. Huenda kuepuka kuzini kukampelekea mwanamme kudhoofika kwa kiasi ambacho hata akija kukutana na mkewe hatoweza kufanya lolote.

 

Hivyo, mazungumzo baina ya mume na mke kwenye simu na wakastarehe kwa sauti hadi mmoja akamaliza haja yake bila mwanamme kutumia mkono kujichua au mwanamke kujisugua utupu wake, hilo halikatazwi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share