Mume Hamtizimizii Tendo La Ndoa Ipasavyo – Na Anatambua Kuwa Ni Kosa; Je, Mke Afanyeje?

SWALI:

 

Asalam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu, Hongera ndugu alhidaaya kwa kazi yenu ngumu Mungu atawabariki. SWALI LANGU ni mume wangu tumeowana miaka 3 alhamdullilah sina shida kabisa ya aina yoyote ila ikifika wakati wakujamiana mume wangu hutoa kila pingamizi na sikuwa ni mgonjwa wala hana matatizo ya uwume na yuwajua kama nimakosa anayofanya sababu humueleza mimi sipendezwi na hivo unavofanya hunijibu ndio hata mungu hapendi basi siku hiyo atanifurahisha baada ya hapo nitaisabu tena miezi. Naomba munifahamishe niko kwenye dhiki.

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu mumeo kutokutekelezea vilivyo na ipasavyo tendo la ndoa.

Hili ni tatizo kubwa sana ambalo huwakumba wanandoa, ima mume au mke anakuwa na ajizi au basi kutotaka tu kumtimizia mwenziwe kwa sababu moja au nyengine.

 

Ikiwa mume hana tatizo lolote basi tu anakuwa ni mwenye kumuudhi mkewe kwa kutomkidhia mkewe, mume huyo atakuwa anadhulumu na hivyo kupata madhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka. Tatizo hili hupelekea kwa wanandoa kuachana kwani mmoja wao huwa anadhulumika. Hivyo hakuna budi kupatikana njia za kuweza kutatua tatizo hilo.

 

Jaribu kutumia njia zifuatazo ili kumrekebisha mumeo:

 

1.     Jaribu kuzungumza naye tena kwa njia nzuri na wakati unaofaa kwa suala hilo ili mfikie suluhisho muafaka kwa tatizo lenu hilo.

 

2.     Kujaribu kumbadilisha kwa kumpatia vitabu au CD zinazo zungumzia suala hilo.

 

3.     Itisha kikao baina yako na yake pamoja na wawakilishi wenu ambao wanaweza kuwa ni wazazi wenu au jamaa zenu wa karibu ili kulijadili suala hilo.

 

4.     Ikiwa hakutapatikana ufumbuzi wa aina yoyote itabidi uende kwa Qaadhi au Shaykh anayetegemewa ambaye anaweza kuwasikiliza nyote na kutoa ufumbuzi wa matatizo yenu.

 

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Ikiwa Hawaridhiani Katika Kitendo Cha Ndoa Wafanye Nini?

 

Mume Kahama Chumba Kwa Miezi 3 Hafanyi Tendo La Ndoa, Akiulizwa Anasema Anachoka Kazini

 

 

Mume Hamtoshelezei Matamanio Yake Ya Tendo La Ndoa, Anaomba Ushauri

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awatatulie tatizo hilo ili muishi kwa njia iliyo bora baina yenu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share