Uongofu (Alhidaaya)

 

KULINGANIA KWA ALLAAH (AD-DA’WATUL ILAA ALLAAH)

Haja ya Watu katika Dini ni sawa na haja ya mwili kwa roho, kama ambavyo ikikosekana roho mwili unaharibika, hivyo hivyo Ummah utakapokosa Dini utaharibika.

Rehma ya Allaah imeenea katika kila kitu, na rehma Zake kwa waja Amewatumia Mitume na Akawashushia vitabu ili wawafundishe watu wamjue Mola wao mwenye kuwaruzuku, wawabainishie Anayoridhia na wawalinganie katika kumtii na kumuabudu Yeye peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote. Pia wawafahamishe Aliyowaandalia Mola katika Thawabu (ujira) kwa atakayemtii na adhabu kwa atakayemuasi.
 
Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Basi wako miongoni mwao ambao Allaah Amewaongoa na wako miongoni mwao ambao upotofu umethubutu juu yao.” An-Nahl: 36

Kila walipodhoofika watu na kuingia katika shirki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alituma Mitume wanaowalingania katika Tawhiyd na kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) peke Yake.

Walifuatana kuja Mitume na kila mmoja alitumwa kwa watu wake maalum, mpaka alipotumwa mwisho wa Mitume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Alitumwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini ya haki kwa watu wote, akafikisha ujumbe, akatekeleza amana, akanasihi Ummah, akapigana katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), akaacha Ummah katika sehemu ya wazi hapotei ila mpotevu.

Alilingania Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) miaka 23 alianzia bara Arabu kulingania mwanzo nyumbani kwake, kisha ndugu wa karibu kisha kabila lake, kisha watu wa Makkah na pembezoni, kisha watu wote. Wakaingia watu katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) makundi kwa makundi.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

“Na hatukukutuma (hatukukuleta) ila kwa watu wote, uwe mtooaji wa habari nzuri na muonyaji, lakini watu wengi hawajui.” Saba-a: 28

 
“Nasi Hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu (wote)” Al-Anbiyaa: 107

 

SABABU ZA UONGOFU

Watu waliingia katika Uislam enzi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuathirika na sababu nyingi, miongoni mwazo:

 

1. ULIMI

Kulingania kwa ulimi, kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomlingania Abu Bakr, Khadiyjah, ‘Aliy, na wengineo wakasilimu.

 

2. ELIMU

Kama alivyoongoka ‘Umar bin Al-Khattwwaab alipoathirika na Qur-aan aliyoisoma katika nyumba ya dada yake Faatwimah alipowakuta wanasomeshwa na mumewe Sa’iyd bin Zayd.

 
3. ‘IBAADAH

Alivyosilimu Hind bint ‘Utbah alipoona Waislamu wanaswali mwaka wa ufunguzi (‘Aamu Fat-h Makkah).

Na kama alivyosilimu Thumaamah bin Athaal Al-Hanafiy katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoathirika na ‘ibaadah.

 

4. KUTOA NA UKARIMU

Kama alivyompa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ‘Aaamul Fat-h Swafwaan bin Ummayah, Mu’aawiyah na wengineo mali nyingi, wakasilimu. Pia aliyepewa mbuzi baina ya majabali mawili ikawa sababu ya kusilimu yeye na watu wake.

Kwa wakati wetu wa sasa kuna njia nyingi za kufikia Uongofu mfano: Mtandao; tovuti za kila Lugha, Kanda za Mawaidha, Darsa, Mihadhara, Semina, Vitabu, Magazeti, Majarida n.k.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ameukirimu Ummah huu kwa kuwapa wadhifa wa Mitume na Manabii wa kulingania (Da’wah) katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) mpaka itakaposimama Qiyaamah.

Alijitahidi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) mpaka walifikia mambo mawili:

1. Kusimamisha Dini katika maisha yao.

2. Kusimamisha Dini katika maisha ya watu.

 
Walikuwa wanaelewa kuwa Da’wah ni jukumu la Ummah, na kila Muislamu, atahesabiwa kwa kuaacha majukumu yake binafsi ya ‘ibaadah, na majukumu ya kijamii ya Da’wah.

 
Anasema Allaah (Subhanahu wa Ta’ala):

“Nyinyi ndio Ummah bora kuliko Ummah zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu, na mnamuamini Allaah.” Aal ‘Imraan: 110

“Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri Uislam na wanaoamrisha mema na wakakataza maovu. Na hao ndio watakaotengenekewa.” Aal ‘Imraan: 104

 
“Sema hii ndio njia yangu, ninaita (ninalingania) kwa Allaah kwa ujuzi wa kweli, mimi (nafanya hivi) na (kila) wanaonifuata. Na Allaah Ametakasika na kila upungufu, wala mimi simo miongoni mwa wanaomshirikisha (Allaah).” Yuusuf: 108

 

UONI (BASWIYRAH) NI KATIKA MAMBO MATATU

1. Elimu kabla ya Da’wah (Ulinganiaji)

2. Ulaini pamoja na Da’wah

3. Subra baada ya Da’wah

Walipokea Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) majukumu ya Da’wah na njia zake, wakaacha matamanio na raha zao, wakajitolea nafsi, mali na wakati wao kueneza Dini Ulimwenguni.

Ukaenea Uislamu mashariki na magharibi, miji ikafunguliwa, Tawhiyd ikaenea shirki ikaondoka. Wakadhihiri Maulamaa na Walinganiaji. Hao ni kheri ya karne Amewasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

“Na wale waliotangulia wakawa wa kwanza katika (Uislam) Muhaajiruun na Answaar, na wale waliowafuata kwa mwendo mzuri, Allaah Amewaridhia, nao wamemridhia (Allaah kwa hayo mazuri Atakayowapa) na Amewandalia Mabustani yapitayo mito mbele yake, wakakae humo milele. Huku ndiko kufuzu kukubwa.” At-Tawbah: 100

Ili Uongofu uenee inabidi waliobeba jukumu la Da’wah wawaige wema waliopita.

 

KUKOSEKANA UONGOFU

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipotanguliza Juhudi na Da’wah kuliko kuchuma na kutafuta vitu vya halali, yalipungua katika maisha yao vitu na mali. Lakini Imani yao ilizidi na matendo mema, ikadhihiri uhakika wa Tabia njema, miji mingi ikafunguliwa (ikawa chini ya Uislam).

 
Waislamu wa leo walipotanguliza kutafuta mali (kuchuma) kuliko Da’wah, ikawazidia vitu na mali wakadhoofika katika imani na matendo yakapungua.

Yakaja mambo mawili katika maisha yao.

1. Kukazana (kufanya) bidii katika kukusanya mali kama Mayahudi.

2. Kufuata matamanio kama Manaswara.

Ilipobadilika makusudio, ikapata nguvu upande wa Dunia, ikadhoofika Dini na roho, ikawa pupa ni ya dunia sio ya Dini. Dini ikawa Yatima apitaye kwa watu hapati wa kumlea kwani watu wameshughulishwa na dunia na matamanio.
 
Dini hii itabaki mpaka siku ya Qiyaamah, wanasimamia kundi Umati Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka itakapokuja amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Imekuja katika Hadiyth kutoka kwa Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, nimemsikia Mtume (Swalla Alaahu ‘alayhi wasallam) akisema:

“Halitoacha kundi katika Ummah wangu unasimamia jambo la Allaah, haitawadhuru wenye kuwapinga mpaka ije amri ya Allaah nao bado wapo wazi kwa watu.” Al-Bukhaariy na Muslim

 

FADHILA ZA KULINGANIA KWA AJILI YA ALLAH MTUKUFU

Kila mwenye kuamini na akasimamia ‘Ibaadah na kulingania kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), basi Allaah Atamkirimu, miongoni mwazo kutukuzwa hata kama hana sababu za kutukuzwa mfano Bilaal na Salmaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma), na Atajaalia matendo ya Dini yote ni yenye kupendeza kwake anayatekeleza na kulingania, na Atajaalia Allaah mapenzi katika nyoyo za viumbe (wampende), na Atamuunga mkono, Atamjibu du’aa zake, Atamjaalia haiba, Atampa ujira mfano wa Aliowalingania na wakaongoka kupitia Kwake, Atamruzuku Msimamo (istiqaamah) na uongofu (alhidaaya).

Anasema Allaah (Subhanahu wa Ta’ala):

“Na ni nani asemaye kauli bora zaidi kuliko aitaye (viumbe) kwa Allaah, na (mwenyewe) akafanya vitendo vizuri na husema (kwa maneno yake na vitendo vyake):Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu,(kwa hivyo niko pamoja nao kwa kila jambo.” Fuswswilat: 33

 
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa wasallam) amesema:

“Mwenye kulingania kheri atapata ujira mfano wa ujira wa wenye kufuata bila kupungua ujira wao chochote, na mwenye kulingania katika upotevu atapata madhambi mfano wa madhambi ya watakaomfuata bila kupunguziwa madhambi yao chochote.” Muslim

 
Amepokea Sahl bin Sa’ad (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuambia ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) siku ya Khaybar:

“…nenda taratibu mpaka uwafikie uwanjani mwao, kisha uwalinganie Uislam, na uwafahamishe yaliyo wajibu kwao katika haki za Allaah. Naapa kwa Allaah Akikuongozea Allaah mtu mmoja ni bora kwako kuliko kumiliki Ngamia mwekundu (waarabu zamani walikuwa wanaona ni mali ya thamani sana ni utajiri kuwa na ngamia).” Al-Bukhaariy na Muslim

 

WATU KATIKA MATENDO NI NAMNA MBILI

1. Miongoni mwao yuko aliyejitahidi katika Dunia kisha akaondoka na kuiacha.
 
2. Na yuko mwengine aliyejitahidi katika Akhera yake na akaikuta. Nao ni namna mbili:

 
a. Aliyejishughulisha na ‘Ibaadah na Da’wah kwa ajili ya Allaah akajitolea kueneza neno la Allaah, huyu matendo yake ni yenye kuendelea, kwani kila aliyeongoka kwa sababu yake anapata ujira mpaka siku ya Qiyaamah.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

“Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuuamirisha Msikiti Mtukufu ni sawa na (kazi ya) wale walioamini Allaah na siku ya mwisho na wakapigania Dini ya Allaah? Hawawi sawa mbele ya Allaah. Na Allaah Hawaongozi watu madhalimu.”

Wale walioamini na wakahama na wakaipigania Dini ya Allaah kwa mali zao wana cheo kikubwa mbele ya Allaah na hao ndio watakaotengenekewa (sio hao wanaoshughulika na hayo wanayoshughulikia Maquraysh).”

 
Mola wao Anawabashiria (Anawapa habari njema za) rehema zitokazo Kwake,na radhi (Zake) na mabustani ambayo humo watapata neema zitakazodumu.”
 
Watakaa humo milele. Hakika Allaah Kwake kuna malipo makubwa kabisa.”
At-Tawbah: 19-22

 

b. Aliyejishughulisha na ‘Ibaadah pekee, yanakatika matendo yake ila matatu:
Sadaka yenye kuendelea, elimu yenye manufaa, mtoto mwema anayemuombea du’aa baada ya kufa.

 
WabiLlaahi At-Tawfiyq.

 

Share