Ndugu Aliyezaliwa Naye Matumbo Tofauti Hamjali Mama Yake; Amnasihi Vipi?

SWALI:

 

Asalaam Alaikum! 

Maswali kuhusu Kaka yangu mie na Kaka yangu tomezaliwa Mama tofauti, Mama yake aliwachika yeye akiwa na Umri wa miaka 2, Mama yangu alipoolewa na Baba yangu akachukuliwa kulelewa ana Umri wa Miaka 3, alilelewa Tuliishi vizuri mpaka alipofika Miaka 15 akaenda kuishi kwa Bibi yake Sababu Secondary sio mbali na hapo alipofika 20 mie na Kaka yangu tukaenda Kusoma UK, Kaka yangu Allaah akamjalia kuowa nikaamuwak utoka kwenye nyumba Baadae Mama yangu mzazi akaja kukaa na mie, Toka Mama yangu amekuja tulikuwa tunaenda Kwakwe ila yeye Haji kwangu namuuliza anasema Kazi nyingi hampigii kumjulia Mama yangu hali mie kwao Nampigia Mama yake na Bibi yake nikienda nawatembelea, hajawahi kumleta Mkewe kwa Mama nasikia wanakuja wanaishia kwa Aunty yake mkewe basi. Mama yangu anajisikia Vibaya kwa nini anafanya hivyo. Je Azabu yake ni nini mie nimsaidie haraka.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu ndugu yako ambaye hamjali mama yako.

Mas-ala haya ambayo umeyaelezea ni vigumu sana kuweza kuamua bila kusikia na upande wa pili, wa nduguyo.

 

Kwa kila hali jazaa ya ihsani haiwi ila ihsani kama alivyosema Aliyetukuka: “Hayawi malipo ya ihsani ila ihsani” (ar-Rahmaan 55: 60).

Hata hivyo, mara nyingine au nyingi watu hawafanyi ihsani kama walivyofanyiwa. Na kufanya hivyo ni dhulma mbele ya Allaah Aliyetukuka. Na mwenye kudhulumu anakuwa katika kiza siku ya Qiyaamah.

 

Linalotakiwa kufanywa ni:

 

1.     Wewe ukabiliane na nduguyo, mkae pamoja wakati unaouona yuko katika hali nzuri ili uzungumze naye kuhusu hilo kwa uwazi kabisa. Na wakati huo kila kitu kitabainika kwa dhahiri.

 

2.     Ikiwa wewe hukuweza kupata ufumbuzi jaribu kutumia marafiki zake wa karibu ili waweze kutatua tatizo hilo.

 

3.     Ikiwa imeshindikana basi jaribu kwenda kwa Imaam wa Msikiti mnaoswali au wa karibu nanyi, au naye, kwa Shaykh au wapenda kheri wenye busara ili muweze kutatuliwa tatizo lenu.

 

 

Ikiwa yote yameshindikana basi itabidi uachilie hapo wala usikate undugu kwani kwa wema unaomfanyia huenda akakumbuka na kurudi nyuma kwa kuomba msamaha kwa mama yako. Pia usikate uhusiano na jamaa zake, kama mama yake na bibi yake kwa ajili hiyo kwani Allaah Aliyetukuka Anasema:

Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki wa karibu wa kukuonea uchungu. Lakini hawapewi wema huu ila wanaosubiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa” (Fusw-swilat 41: 34 – 35).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share