Kaka Amempiga Dada Yake, Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalaam aleykum

Kaka kampiga dada yake (wote wawili ni watu wazima). Mama ana uchungu sana kwa hicho kitendo. Je kisheria hili tatizo litatuliwe vipi? Tafadhali nipe dalili kutoka Quran na sunnah

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kaka kumpiga dadake.

Inatakiwa tufahamu kuwa yule anayefaa kupigwa ni mtoto mdogo kabla hajafika umri wa miaka kumi kwa mujibu wa wanachuoni kuichukua Hadiyth ifuatayo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameusia:

Wafundisheni watoto wenu Swalah wakiwa na miaka saba na wapigeni wakiacha kuswali wakiwa na miaka kumi” (Abu Daawuud).

Hivyo, mtu akishapita miaka kumi haifai kupigwa ila awe ni mke wa mtu aliyekengeuka na maamrisho ya Uislamu. Hata hivyo, haifai kumpiga hata mtumwa kipigo cha kumuumiza wala kulenga uso.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametabiri kuwa kutakuja wakati ambapo wanaume watakuwa wanawapiga wanawake, nao watakuwa ni watu wa Motoni. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Watu aina mbili ni katika wakaazi wa Motoni ambao sijawaona: Watu wenye viboko kama mikia ya ng’ombe nao watakuwa wanawapigia watu…” (Muslim).

 

Jambo ambalo linatakiwa lifanywe na familia sasa, baba akiwepo achukue jukumu la kuwakutanisha wahusika ili kufanywe suluhu ili jambo hilo lisitokee tena. Na katika suluhu lazima kupatikane chanzo cha tatizo lenyewe, na kutoka hapo upatikane ufumbuzi. Hata ikiwa dada ni mkosa inatakiwa huyo kaka aelezwe kuwa hatua ya kupiga imepita mipaka ya kishari’ah. Na Allaah Aliyetukuka Anasema:

Na suluhu ni bora”.

Pia,

Hakika Waumini wote ni ndugu, suluhisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa” (al-Hujuraat [49]: 10).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share